Saturday, April 11, 2015

WAGOMBEA UBUNGE RORYA 2015

ADVERTISEMENT
Wakati vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka huu likiendelea nchini, Tasnia ya michezo nayo imeanza kupata msukumo kwa wanamichezo kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kwenye uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Tayari wanafamilia wa michezo wanne, wametangaza nia ya kuhakikisha wanachukua majimbo kwenye uchaguzi huo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wanamichezo hao ni: Wilhelm Gidabuday (anagombea kupitia Chadema)
Huyu ana kumbukumbu nzuri katika tasnia ya michezo hasa riadha kwani alikuwa mstari wa mbele kukosoa maandalizi waliyopewa wanariadha wa Tanzania walioshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka jana nchini Scotland.
Gidabuday amejitosa kuwania ubunge wa Jimbo la Hanang kwa tiketi ya Chadema, jimbo linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Mary Nagu wa CCM.
“Kwa kuamini kwamba kugombea nafasi yoyote ni haki ya msingi kikatiba, mimi kabla ya kujitathmini mwenyewe nimefanyiwa tathmini na watu wa rika tofauti ndani ya jamii, makundi hayo yakiwakilisha watu wenye busara katika jamii na kuniweka katika orodha ya watu wenye sifa stahiki,” anasema Gidabuday.
Ataitetea michezo bungeni
“Wananchi wa Hanang pia wameridhishwa na harakati zangu za kutetea wanamichezo, hususan riadha kitaifa, Watanzania wengi wananifahamu kwa jina la (mwanaharakati wa michezo Tanzania). Harakati zangu michezoni zimenifanya kuaminiwa na wadau wa michezo kote Tanzania,” anasema Gidabuday.
“Sheria namba 12 ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ya mwaka 1967 licha ya kukosa meno, lakini pia imedharauliwa na viongozi wa wizara, BMT wenyewe na taasisi zilizokusudiwa kusimamiwa na sheria hiyo, na matokeo ya udhaifu huo umesababisha ufisadi ndani ya vyama vya michezo, ndiyo maana Tanzania tumekuwa watalii katika viwanja vya michezo kimataifa.
 Ili kuondoa hali hiyo nitatoa hoja binafsi sheria hii ibadilike sambamba na kuikumbusha Serikali umuhimu wa kuwa na kijiji cha michezo,” anasema Gidabuday.
Mada Maugo (anagombea kupitia Chadema)
Bondia huyu anajitosa kwa mara ya kwanza kuwania ubunge wa Jimbo la Rorya kwa tiketi ya Chadema, jimbo hilo sasa linaongozwa na Lameck Airo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Sijaingia kugombea ubunge kwa bahati mbaya, nimedhamiria kuwatumikia wananchi wa Rorya ambao kwa kiasi kikubwa wameonyesha imani na mimi,” anasema Maugo bondia namba tatu kwa ubora nchini kwenye uzani wa super middle.
Ataendelea na ngumi?
ADVERTISEMENT
“Ngumi siwezi kuacha hata kama nitapewa ridhaa ya kuwa Mbunge wa Rorya, nitakachofanya ni kutenga muda wa kufanya mazoezi na kupunguza idadi ya mapambano kwa mwaka na kutenga muda mwingi wa kuwatumikia wananchi wa Rorya,” anasema Maugo.
Anasema kikubwa atakachokifanya bungeni ni kuwapigania Wanarorya hasa katika huduma muhimu za kijamii kama afya, barabara, maji na kunufaika na rasilimali walizonazo.
“Katika sekta ya michezo, hasa ngumi nitahakikisha unakuwa na usimamizi mzuri ili kuwafanya mabondia wa Tanzania kupiga hatua kimataifa kwani kuna madudu mengi yanafanywa na viongozi wanaosimamia ngumi ambayo yanadidimiza mchezo huu na kuufanya usisonge,”anasema Maugo.
Frederick Mwakalebela (Anagombea kupitia CCM)
Kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, Mwakalebela ambaye hivi sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe amejitosa tena kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwani mwaka 2010 alitoswa kwenye kura za maoni ndani ya CCM hivyo kushindwa kugombea kiti hicho.
Jimbo hilo sasa lionaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.
Mwakalebela ambaye kabla ya kujiingiza katika siasa, alipata kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anasema atatumia muda mwingi kuwatumikia Wanairinga katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya jimbo lao endapo atapata ridhaa hiyo.
“Pamoja na kuwatumikia wananchi wa jimbo langu, sitaipa kisogo michezo, nitahakikisha Iringa haibaki nyuma katika soka la Tanzania na hata michezo mingine, sioni cha kutushinda katika hilo kama nimeweza kuhamasisha vijana kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani, hakuna shaka kuwa tutapiga hatua pia kwenye michezo.
Innocent Melleck (Anagombea kupitia CCM)
Melleck anasema ameshawishika kuwania ubunge wa Jimbo la Vunjo ambalo sasa Mbunge wake ni Agustino Mrema wa Chama cha TLP, baada ya kushinikizwa kufanya hivyo na wazee wa jimbo hilo na atagombea kupitia CCM.
Anasema kama atapata ridhaa ya Wanavunjo kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu atatimiza ndoto yake ya siku nyingi ya kuwa mtetezi kwa wananchi wa Vunjo, sambamba na kuipigania sekta ya michezo nchini ambayo tayari ameanzisha mbio za Uhuru marathoni zinazolenga kutangaza amani ya Tanzania na kuwasaidia wanariadha nchini.
Wanamichezo walioonyesha njia
Wakati wanamichezo hao wakitia juhudi kuingia bungeni kwenye uchaguzi wa mwaka huu, tayari wapo wanamichezo bungeni kama Juma Nkamia ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, pia ni Mbunge wa Kondoa Kusini ambaye amewahi kuwa Katibu Mwenezi wa Simba.
Pia yupo Mohamed Dewji ambaye ni Mbunge wa Singida Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ni Waziri kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mbunge wa Mbeya Mjini, yupo Ismail Aden Rage aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Simba ambaye sasa ni Mbunge wa Tabora Mjini.

No comments:

Post a Comment