CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo kimemkabidhi Ilani Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob ili imuongoze katika utendaji wake. Anaandika Rorya Maendeleo
Akikabidhi ilani hiyo katika Ofisi za Manispaa kwa niaba ya chama, Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Kasmil Mabina amesema, anamkabidhi meya ili aweze kutekeleza ahadi za Chadema kwa wananchi kwa kuwa yeye ndiye muwakilishi wao.
Ilani hiyo imeorodhesha vipaumbele vya chama ikiwa ni pamoja na kushuhulikia suala la bomoabomoa, maji, elimu. Pia Chadema kimemtaka kuwaagiza madiwani kufuatilia na kuhakikisha waliobomolewa wanapata haki zao ikiwemo kulipwa fidia.
Mabina akisoma Ilani hiyo amesema, Jacob pia anajukumu la kushugulikia elimu katika Manispaa yake na kuhakikisha anakusanya mapato ya kutosha kama chama kilivyokuwa kinaahidi.
“Inatakiwa tujitahidi ili tuoneshe mfano kwa CCM na tuwaaminishe wananchi kwamba upinzani pia unaweza kuongoza vizuri. Ilani hii tuliyompa Jacob imetokana na katiba ya chama inayomtaka Meya na Madiwani kuisimamia manispaa na kuanda mipango kazi yake na kuwasilisha utekelezaji wake katika kikao kikuu cha chama,” amesema Mabina.
Jacob baada ya kukabidhiwa Ilani hiyo ameahidi kutekeleza yote aliyoagizwa na chama chake huku akiwataka wananchi kuendelea kumuamini katika utendaji wake.
“Nataka niwatoe hofu wananchi wangu kwamba, kukabidhiwa Ilani ya chama haimaanishi kwamba nitakuwa Meya wa wana Chadema au Ukawa tu, bali nitayachukuwa mazuri yote kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote,” amesema
No comments:
Post a Comment