Balozi wa Kampeni ya Kili Challenge Msanii Mrisho Mpoto amekonga nyoyo za mashabiki na wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwenye mnada maalumu wa bidhaa mbalimbali za kuchangia fedha za Kampeni ya Kili Challenge kwenye ukumbi wa Lapa Mchauru Mkoani Geita.
Kili Challenge ni mfuko unaochangisha fedha kila mwaka kwa kudhamini watu kupanda mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kupambana na janga la ukimwi Tanzania. Mfuko huu unaratibiwa na Mgodi wa Geita (GGM) kwa ushirikiano na Taasisi ya Kupambana na Ukimwi Tanzania (TACAIDS) pamoja na wadau wengine mablimbali. Hadi sasa zaidi ya Taasisi 30zinazojihusisha na Ukimwi zimenufaika na mfuko huu wa Kili Challenge na watu zaidi ya 500 kutoka duniani pote, wamepanda mlima Kilimanjaro kupitia mfuko huu.
Akiimba kwa hisia Mrisho Mpoto pamoja na Msanii mwenzake Mwimbaji wa mziki wa “Live” Ibrozama Mkungwe maarufu kwa jina la “Beka” walitumbuiza wimbo wa “Sauti Nenda” remix ikiwa ni mahususi kuwakumbusha watanzania kwamba Ukimwi bado upo na ni jukumu la kila mmoja wetu kuchukua hatua dhaditi katika mapambano hayo.
Msanii Mrisho Mpoto “Mjomba” akiwa na Msanii Ibrozama Mkungwe “Beka” wakiimba kwa hisia wimbo “Sauti Nenda” kwenye mnada wa Kili Challenge uliofanyika katika mgodi wa GGM mjini Geita kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia serikali katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Balozi wa Kili Challenge Mrisho Mpoto maarufu kama “Mjomba”akitumia mtindo wake wa kughani mashairi kwa kuongea kwa hisia ametoa wito kwa jamii yote Tanzania kuendelea kupambana na janga hili ili Kufikia sufuri 3 – Zero ya Maambuki, Zero ya Unyanyapaa na Zero ya vifo vitokanavyo na Ukimwi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Bw Terry Mulpeter(kushoto) akifurahia jambo na Mkuu wa Wilaya ya Geita anayemaliza muda wake Bw Omar Mangochie(kulia) wakati wa hafla ya mnada wa Kili Challenge uliofanyika Mgodi wa dhahabu GGM ili kuchangisha fedha katika mapambano dhidi ya Ukimwi Tanzania.
“Sauti nenda,usipitie masikioni kama tulivyozowea,pitia kwenye moyo na uwaambie tumechoshwa na majina ya unyanyapaa tunayoitwa, waambie hatupendi kuitwa..ana ngoma,…….ana miwaya……kanasa……….”Alisikika balozi wa Kili Challenge Mrisho Mpoto kwenye mashairi ya Wimbo wake mpya wa “Sauti Nenda” wimbo aliouimba “live” akishirikiana na msanii “Beka”.
Akizungumzia Kampeni ya Kili Challenge, Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGM) Bw Terry Mulpeter alisema kuwa mwaka huu Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kushirikiana na tume ya kudhibiti na kupambana na UKIMWI(TACAIDS) na wadau wengine wanatarajia watu zaidi ya 100 watashiriki katika kupanda mlima Kilimanjaro na kuuzunguka kwa kutumia baiskeli kwa jumla ya siku 7 ili kuchangisha fedha na kuisaidia serikali katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Zoezi rasmi la kupanda Mlima Kilimanjaro litaanza tarehe 16 Julai ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mh. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Bw Terry Mulpter (katikati) akiwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Geita Mh.Omar Mangochie na Balozi wa Kili Challenge Msanii maarufu Afrika Mashariki na Kati bwana Mrisho Mpoto “Mjomba” kwenye picha ya Pamoja na watoto na walezi wa kituo cha watoto Yatima “Moyo wa Huruma” mjini Geita ambapo wazazi wa watoto hawa wamepoteza maisha kwasababu ya janga la Ukimwi. Kituo hiki chenye watoto zaidi ya 100 kinaendesha shughuli zake kwa udhamini wa mfuko wa Kili Challenge na Mgodi wa dhahabu wa Geita GGM.
No comments:
Post a Comment