Rorya maendeleo Blog 1 hour ago
VIONGOZI wa kada mbalimbali nchini, wametahadharishwa kuwa makini na watu wanaofanya vitendo vya utapeli kwa kutumia majina na picha za viongozi wa juu, wakiwamo mawaziri ili kujipatia fedha..
Tahadhari hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Selemani Jafo, alipokuwa akifunga mafunzo ya viongozi hao kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo ni ya awamu ya pili kutolewa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na ofisi ya Rais Tamisemi na yamejumuisha viongozi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Jafo alisema kumeibuka wimbi la utapeli wa kutumia majina ya viongozi kuwalaghai viongozi mbalimbali kwenye wilaya kutuma fedha.
“Kumekuwapo na watu wanatumia picha na majina ya viongozi kutuma ujumbe mfupi wa kuwataka wakuu wa wilaya au mikoa na wakurugenzi kutuma fedha wakidai kuwa kiongozi fulani amepatwa na jambo fulani la dharura. Naomba mjiepushe na watu hawa kwa kuwa ni matapeli,” alisema Jafo.
Alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa ngazi za juu serikalini kwa madai kwa wanauguliwa au wamepata shida mbalimbali wawapo safarini jambo ambalo si kweli.
“Nataka kuwapa angalizo kuweni makini. Kama mtu atakuwa na shida kama ni waziri atampigia katibu wake au atatumia nafasi yake kutoa taarifa ili kupatiwa huduma lakini si kwa kupigiwa simu au kutuma ujumbe mfupi,” alisema Jafo.
Aidha, aliwataka kusimamia mipango ya maendeleo iliyopo kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha na kuhimiza wafanye kazi kwa manufaa ya Taifa na siyo kwa manufaa yao.
Jafo aliwataka wakatumie mafunzo hayo kama chachu ya kuwafanya kuwa na weledi mkubwa zaidi tofauti na ilivyo kuwa hapo awali.
Nabu Waziri Jafo aliwataka wakurugenzi kutozalisha madeni ya watumishi katika halmashauri zao.
“Hakuna sababu yoyote ya halmashauri kuwa na madeni ambayo hayana msingi na msiwahamishe watumishi bila kuwa na maandalizi ya malipo,” alisema.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Denis Rweyemamu, alisema mafunzo yanalenga kuwajengea uwezo ili kufanya kazi kwa malengo ya maendeleo.
Alibainisha kuwa licha ya viongozi hao kufanya kazi vizuri, bado walitakiwa kupata mafunzo ili kuongeza weledi katika utendaji kazi.
No comments:
Post a Comment