Monday, April 13, 2015

ACT TANZANIA; TAARIFA KWA UMMA.

Ndugu Watanzania,Wanachama wa ACT-Tanzania, Wapenzi wa ACT-Tanzania na wadau wote kwa ujumla; tunawasalimu kwa salamu inayoashiria mabadiliko na uwazi!
Chama kinapenda kuutaarifu umma juu ya mambo yafuatayo:-


1.Ofisi za chama:
Chama cha ACT-Tanzania, kinapenda kuutaarifu Umma kwamba sasa ofisi za chama za makao Makuu za muda (za muda kwa sababu mkutano mkuu wa chama unaweza kuamua kuwa makao makuu yawe nje ya Dar es salaam) zimeanza kufanya kazi pamoja na kuwa bado matengenezo yanaendelea.Hii ni kutokana na umuhimu na mahitaji makubwa walionayo watanzania ya kuendelea kupata huduma katika ofisi zetu pamoja na umuhimu wa chama kuendelea na shughuli zake za kila siku ili kufikia malengo.Hata hivyo matengenezo yanayoendelea kwa sasa hayaathiri sana huduma; hivyo yeyote anayehitaji kufika katika ofisi za chama kwa ajili ya huduma yeyote, anakaribishwa sana.

Ofisi za chama cha ACT-Tanzania (Alliance for Change and Transparency) zipo Ubungo mtaa wa NHC.Ukitaka kufika zilipo ofisi za chama, ukiwa barabara ya Morogoro, utaingilia bara bara ya shekilango hadi ilipo Hoteli ya Rombo utaona barabara ya vumbi inayoenda upande wa kushoto, utaenda nayo hadi unakapofika Hotel ya "Royal Njombe hotel" ambapo ofisi ya chama iko mkabala na hotel hiyo. Vile vile unaweza Ukatokea ilipo Bank ya NBC Ubungo na ukanyoosha moja kwa moja hadi ilipo Hotel ya Royal Njombe hotel ambapo hapo utaona ofisi ya chama.


2.Program ya kazi za Chama baada ya usajili:

Ndugu wanachama, wapenzi, mashabiki wa ACT-TANZANIA na watanzania kwa ujumla, Chama cha ACT-Tanzania kinawataarifu kwamba baada ya usajili wa kudumu, Kamati ya Taifa ya Uongozi ilikaa katika kikao chake cha kawaida Jumapili Mei 11, 2014. Moja ya mambo yaliyojadiliwa na kuamuliwa ni ratiba ya program ya utendaji kazi za chama kuanzia sasa. Safari ndefu ya chama hiki ya kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi hii, sasa inaanza rasmi. Kwa sababu hiyo, chama kinatoa ratiba ya matukio kwa miezi michache ijayo kama ifuatavyo:


Mei 18, 2014 – Kikao cha Kamati ya Uongozi taifa kupokea na kuridhia rasimu ya katiba kutoka kwa Kamati ya Katiba;


Juni 01, 2014 – Kikao cha Halmashauri Kuu ya muda taifa kupitia rasimu ya katiba na kuingiza mapendekezo yake;


Juni 02 – 12, 2014 – Kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali wanachama na wadau wengine wa ACT – Tanzania;


Juni 15, 2014 – Kikao cha Mkutano mkuu maalum kupitisha katiba na kuruhusu uchaguzi ndani ya chama uweze kuanza;


Juni 16 - Agosti 15, 2014 – Uchaguzi wa ndani ya chama kwenye ngazi za kuanzia Kijiji/Mtaa hadi Mkoa.


Agost 29-30,2014 - Uchaguzi wa viongozi wa chama ngazi ya taifa.


Septemba 01, 2014, -Uzinduzi rasmi wa chama.


3. Uenezi wa Chama:

Chama kinapenda kuwakumbusha wapenzi,viongozi na wanachama kwamba ratiba hiyo iliyopendekezwa na kikao cha Kamati ya Uongozi haimaanishi kazi za kujenga na kueneza chama zinasimama kusubiri ratiba hiyo. Kazi ya uenezi wa chama iendelee na ifanyike kwa nguvu zaidi kwenye wakati huu tunaposubiri kupitishwa rasmi kwa katiba ya chama ili katiba itakapokuwa tayari iwe rahisi kuanza uchaguzi kwa kuwa kutakuwa na wanachama wa kutosha tayari kwenye ngazi za chini kabisa. Uenezi ni kazi yetu sote viongozi, wapenzi na wanachama na tushirikiane kuifanya kwa nguvu moja ili kujenga chama chetu pamoja na hatimae nchi yetu kwa ujumla.

Pamoja na Taarifa hii: tunapenda kuileta kwenu misingi kumi (10) ya chama cha ACT-Tanzania.Tafadhali ipitie misingi hiyo kwenye kiambatanisho hapo chini.


Misingi ya ACT Tanzania-Final.pdf
ACT-Tanzania ni kwa taifa la leo na kesho.Tumedhamiria na Mungu atatusaidia.


ACT-Tanzania .......................Taifa kwanza!!!
Mabadiliko na uwazi...............Chukua hatua!!!

Kwa mawasiliano zaidi na uongozi wa chama wa muda, tuma barua pepe kwendaacttanzania@yahoo.com au acttanzania@gmail.com

KWAKWELI TUMEJIPANGA SANA TENA SANA KULINGANA NA SIFA ZA VIONGOZI WETU 

No comments:

Post a Comment