Kumi wakamatwa
Tanzania kwa ugaidi.
·
15 Aprili 2015
Watu 10 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya
kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi
inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja
anayesadikiwa kuhusiana na watu hao waliokamatwa aliuawa na wananchi wenye
hasira baada ya kumjeruhi kwa panga askari polisi aliyekuwa akipambana naye.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo
limetokea jana (Aprili 14) majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha
Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.Kamanda Paul alimtaja mtu
aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo ambaye umri wake haujafahamika ambaye ni
mkazi Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha alisema siku ya tukio polisi
walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa
kuwa wanajihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua
kufatilia nyendo zao.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema: “Polisi walipata
taarifa kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili kwenda kusikojulikana
na wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia ndipo walikutana na bajaji moja
ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo na kuisimamisha.”
Alisema kuwa bajaji hiyo
iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari mwenye namba
F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo
alichomoa jambia alilokuwa nalo na kumkata askari huyo eneo la shingoni.
Askari mwingine mwenye namba
E.9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu
mtuhumiwa huyo, ambapo alipoanguka chini wananchi wa eneo hilo tayari walifika
katika eneo hilo na kuanza kumshambulia marehemu huyo kisha kumchoma moto kwa
hasira.
Kamanda huyo alisema walianza
kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo
Kidatu.
“Polisi walipofika katika msikiti
huo waliuomba uongozi wa msikiti huo kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili
kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa mashaka.”
Alisema polisi walendelea na
ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.
Kamanda huyo alitaja vitu vilivyokutwa katika mabegi yaliyokuwa
ndani ya msikiti huo ni pamoja na milipuko 30, bendera nyeusi yenye maandishi
ya Kiarabu yakisomeka ‘Mungu Mmoja’, majambia, bisibisi, vinyago vya kuziba uso
(masks), nguo za jeshi, misumeno ya chuma na spana.
No comments:
Post a Comment