SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), leo linatarajia kuzindua jezi mpya za timu ya Taifa Tanzania, ambazo zitakuwa zinatumika katika michuano mbalimbali huku kukiwa na hafla ya kuwatunuku wachezaji na klabu mbalimbali.
Sherehe hiyo itafanyika katika hoteli ya JB Belmonte iliyopo eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto alisema jezi hizo zitakuwa zinatumika katika michuano mbalimbali hususani ya kimataifa pamoja na mechi za kirafiki.
Alisema wao kama TFF wameamua kuwa na jezi aina mbalimbali kwani kila nchi inakuwa na jezi zaidi ya moja.
"Mara baada ya mtu tuliyempatia kazi kukamilisha zoezi la kubuni jinsi gani jezi ikae tumeona bora tuzitambulishe ili kila mtu aweze kuzijua jezi mpya za timu ya Taifa," alisema Kizuguto.
Pia alisema katika hafla hiyo, TFF itawatunukia vyeti viongozi mbalimbali waliotoa mchango katika mpira wa miguu.
Alisema pamoja na hilo pia wadhamini, wahamasishaji pamoja na wachezaji waliochezea Taifa Stars ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 tangu Tanzania kujiunga na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Aliwataja baadhi yao kuwa ni Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wote wa kitaifa walioshika nyadhifa za juu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi wengine watakaotunukiwa ni wenyeviti wote wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) pamoja na wa TFF huku makatibu wakuu nao wakipewa tuzo zao.
Waamuzi pamoja na wachezaji waliosaidia katika kuinua soka la Tanzania watapatiwa nishani zao na shirikisho hilo baada ya kuwa mstari wa mbele.
Alisema timu ya Taifa ya mwaka 1979-1980 iliyokwenda Nigeria kushiriki michuano ya Mataifa huru barani Afrika ambapo kwa sasa Mataifa ya Afrika watapatiwa nishani zao huku wakiongozwa na nahodha Leodgar Tenga na kocha mkuu akiwa Slomir Wolk akisaidiwa na Joel Bendera.
Viongozi wengine watakaopatiwa nishani hizo ni mawaziri wote waliopita katika Wizara ya Michezo tangu kujiunga na FIFA na viongozi wote wa baraza la michezo (BMT).
Nao Wakurugenzi wote wa michezo hawakuachwa nyuma baada ya kuonesha mchango wao katika michezo ili kuweza kuinua nchi yetu upande wa soka.
Wadhamini nao hawakusahaulika kwa jitihada zao za kuinua soka la nchi yetu baada ya kuzisaidia timu mbalimbali pamoja na timu ya Taifa katika upande wa udhamini na hicho ni kitu pekee cha kuwashukuru.
Katika kuwakumbuka watangazaji wa zamani, TFF itawatunukia nishani za utangazaji bora wa mpira katika kipindi chote huku wakiwa katika mstari wa mbele kuwahabarisha wananchi habari kuhusu mpira wa miguu.
Waandishi wa habari za michezo, wahamasishaji watapatiwa nishani zao kama wadau wa mpira wa miguu na kuipa hamasa timu ya Taifa.
Mabingwa wa ligi na viongozi wa klabu tangu ligi inaanza ambapo hapo awali kulikuwepo na ligi ya Muungano wote watapatiwa nishani zao.
Alimalizia kwa kusema kuwa viongozi wote walioshiriki katika ujenzi wa viwanja watapatiwa nishani zao kama washiriki wakuu wa kuinua soka hasa upande wa miundombinu.
No comments:
Post a Comment