UCHAGUZI WA BUNGE BURUNDI WAAHIRISHWA
UCHAGUZI wa wabunge uliokuwa umepangwa kufanyika Juni 5 na ule wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika Juni 26 umeahirishwa na hakuna tarehe mpya iliyotajwa ya kufanyika tena uchaguzi huo.
Msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza, Willy Nyamitwe, amesema kuwa tume ya uchaguzi itapanga upya zoezi hilo kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mipaka ya katiba ya nchi na kisha kutangaza tarehe mpya ya kufanyika zoezi hilo.
Aidha kufuatia tangazo hilo la kuahirishwa uchaguzi wa bunge na rais, kambi ya upinzani nchini humo imesema kuwa iko tayari kukutana na upande wa serikali kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo Viongozi wa EAC waliokutana Dar es Salaam, Tanzania wiki moja iliyopita kujadili mgogoro wa Burundi, walipendekeza uchaguzi wa bunge na rais uahirishwe kwa siku 45 ili kutoa nafasi kwa hali ya mambo kutulia na wakimbizi kurudi nyumbani.
Aidha kitendo cha Rais Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa awamu ya tatu, ni kitendo kilichopingwa na watu wengi nchini humo na kusababisha mauaji ya watu wengi sana.
No comments:
Post a Comment