Wednesday, February 17, 2016

Mrembo Abakwa na bodaboda

Mrembo Abakwa na bodaboda

By:roryamaendeleo / Posted: Wednesday 17th February 2016
IMG_2640Mrembo anayedaiwa kubakwa na bodaboda.

Hamida Hassan na Gladness Mallya, Risasi

DAR ES SALAAM: Mrembo mmoja (jina linahifadhiwa), mkazi wa King’ong’o nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, hivi karibuni alipata wakati mgumu baada ya vijana wawili kumbaka kwa zamu hadi kupoteza fahamu katika pori la Goba.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mrembo huyo aliwataja vijana anaodai walimbaka ambao pia ni wakazi wa King’ong’o kuwa ni Juma Bunju na Jack Pemba ambao ni marafiki.

“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni Jumapili Januari 31, mwaka huu, nilikuwa kazini kwangu nafunga mahesabu kama kawaida, nilipomaliza kulikuwa na pikipiki tatu zimepaki nje ya ofisi yangu, niliamini ni watu wazuri kwa sababu ni kawaida bodaboda kuja kupaki hivyo niliomba mmoja wao anipeleke nyumbani ambapo si mbali sana.


20160211_121242Mrembo huyo akiongea na mwandishi wetu (hayupo pichani).

“Nikiwa kwenye bodaboda nilishangaa kuona anapanda mwanaume mwingine kwa nyuma yangu, nikahoji kulikoni nikaambiwa huyo anashuka hapo karibu tu nisiwe na hofu, nilianza kukataa kwa kuwahoji kwa nini wanapakizana bila kuniambia ndipo wa nyuma akanifunika uso na shati kisha wakaniambia nitulie, wakanipeleka kwenye pori kubwa la Goba,” alisema.

Alidai akiwa huko porini, alijitahidi kupigana nao kwa muda mrefu, lakini walimzidi nguvu baada ya kumpiga usoni na kumuangusha chini na kumbana miguu.

“Baada ya hapo waliniingilia kimwili bila huruma hadi nikapoteza fahamu, nilizinduka kama saa kumi na nusu alfajiri, ndipo nikachukua lile shati na kulivaa kwani sikuwa na nguo, nikaanza kujivuta taratibu mpaka barabarani.

“Nakumbuka kuna mwanaume mmoja alipita, nikamuita na kumuomba msaada, alionekana kuniogopa, akakimbia lakini baada ya muda akaja na gari, wakanisaidia na kunipeleka nyumbani baada ya kuwasimulia mkasa mzima, ilikuwa rahisi kwa vile kazini kwangu walikuwa wanapajua na hata bosi wangu wanamfahamu,” alisema.

Mrembo huyo alisema alikwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi Kimara na kufunguliwa jalada namba KM/RB/484/2016 Kubaka kisha kwenda hospitalini kupima kama amepata maambukizi yoyote.

“Naiomba serikali inisaidie kuwakamata watuhumiwa hawa kwani wapo mtaani na siyo mara ya kwanza kubaka, wanafanya hivi kila siku, wakikamatwa wanaachiwa,” alisema.

Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, lakini simu yake haikuweza kupatikana na juhudi za kumtafuta ili kuzungumzia hatua zilizochukuliwa zinaendelea.

No comments:

Post a Comment