MAJALIWA: MARUFUKU WANAFUNZI KUTUMIA VIBERITI, MISHUMAA MABWENINI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na hita za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.
“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Waziri Mkuu amesema kwa namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema yakavunjwa na kujengwa upya ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga madarasa mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, mama Salma Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na wanafunzi waliosoma shule hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali nchini kufunga vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia pindi ajali za moto zinapotokea.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, JULAI 14, 2016
No comments:
Post a Comment