Naziona dalili za Kinana, Mangula wakijiuzulu CCM Mayage S. MayageToleo la 413 8 Jul 2015 CHAMA cha Mapinduzi (CCM), ambacho nje ya mipaka ya Tanzania kina sifa na historia ya kutukuka ikilinganishwa na kinavyoonekana ndani ya jamii ya Watanzania, wiki hii kinaingia kwenye wakati mwingine wa kuendelea kuandika historia yake, iwe chanya au hasi. Kwa CCM, hii ni wiki ya kuamua hatma ya chama chenyewe hicho, ya kuendelea kushika dola kwa miaka mingine mitano ijayo, lakini pia kuamua hatma ya uongozi wa Tanzania hii. Si siri, kwa mwezi mzima uliopita wa mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba nafasi ya urais ndani ya chama hicho, ulioanza Juni 3 na kuhitimishwa Julai 2, mwaka huu, macho na masikio ya Watanzania walio wengi vilikuwa vimeelekezwa mjini Dodoma yaliko Makao Makuu ya chama hicho kwa lengo la kufuatilia mchakato huo. Baada ya mchakato huo wa kuchukua na kurejesha fomu kukamilika, sasa wiki hii yote, macho na masikio hayo vitaelekezwa katika mchakato wa mwisho na muhimu zaidi kwa mustakabali wa CCM na Taifa hili, unaohusiana na uteuzi wa wagombea utakaofanywa na vikao vikuu vitatu vya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na hatimaye Mkutano Mkuu. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba vikao vyote hivyo vikuu vitatu sivyo hasa vinavyoamua hatima ya CCM na Uongozi wa Taifa hili, bali ni vikao tu vya kutekeleza misingi ya demokrasia ya ndani ya chama hicho, kwa sababu kazi ya kutafuna mifupa, kumpiga rungu nyani bila kumtazama usoni na hatimaye kuamua ni nani na nani, inakuwa imeshakamilishwa na vikao vya utangulizi, ambavyo kiutaratibu na kikanuni, ni vikao muhimu sana. Hivyo ni vikao vya Baraza la Wazee wa CCM, kinachoongozwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi na Katibu wake, Makamu Mwenyekiti Mstaafu (Bara), Pius Msekwa; kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kinachoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa sasa (Bara), Philip Mangula pamoja na kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili, kinachoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete akisaidiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana. Kwenye vikao vitatu hivyo vya utangulizi, humo ndimo mnafananishwa na chumba cha kufanyia mtihani wa mwisho kwa mwanafunzi anayehitimu ngazi yake muhimu ya elimu. Yeyote anayefaulu mia kwa mia ndani ya vikao hivyo, ni rahisi jina lake kufikiswa Kamati Kuu, NEC na hatimaye Mkutano Mkuu kwa uamuzi wa mwisho! Kwa maneno mengine, pamoja na uzito wa kikao cha Kamati Kuu au Halmashauri Kuu, kwa utaratibu wa ndani ya CCM, hakuna haja ya vikao hivyo vikuu vya uamuzi kukutana na majina kama ya makada muhimu sana wa chama hicho, mfano wa Idelphonce Bihole, mkulima mwenye elimu ya darasa la saba kutoka Mkoa wa Kigoma au Maliki Marupu, mwanafunzi wa Chuo Kikuu mwenye umri wa miaka 34, sifa mbili ambazo hazitambuliwi si tu na Katiba ya CCM bali pia Katiba ya Nchi. Hao wanakutana na kuishia kwenye kikao hicho cha Usalama na Maadili! Mada kuu ya makala haya hapo juu, nimesema naziona dalili za Kinana na Mangula wakijiuzulu CCM. Kinana ni Katibu Mkuu wa CCM wakati Mangula ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara. Wawili hawa, pamoja na Rajabu Ruhwavi, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara, ni sehemu ya viongozi wakuu wa chama hicho, wanaomsaidia Kikwete katika kusukuma mbele jahazi la chama hicho wakisaidiana na wenzao wawili wa Tanzania Zanzibar, Makamu Mwenyekiti na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai. Kila mwanachama wa CCM, kuanzia wa kawaida kijijini hadi kwa Mwenyekiti Taifa, anafahamu hali ya kisiasa ilivyokuwa ndani ya chama hicho katika kipindi cha kati ya 2006 na 2012, ulipoingia rasmi uongozi wa Kinana kama Mtendaji Mkuu wake. Kila mwanachama wa CCM, kuanzia mwanachama huyo wa kawaida kijijini hadi ngazi ya Taifa, anatambua kwamba katika kipindi hicho ilifika mahali, wajumbe wa vikao vya kamati tendaji za Chama na Jumuiya zake, hata wanapokwenda kwenye vikao muhimu vya chama chao hicho, waliogopa kuvaa sare rasmi za chama hicho na kupita katika mikusanyiko ya watu, hasa yenye vijana wa Chadema, wakihofiwa kuzomewa kwa kuitwa; “mafisadi hao, mafisadi hao”! Ushahidi wa hili la kutetereka na kuyumba kwa CCM kisiasa, ni wito maalumu wa Kikwete, katika maadhimisho ya kilele cha kutimiza miaka 34 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika mwaka 2011 mjini Dodoma, pale alipoagiza kila mwanachama na kila kiongozi wa chama hicho kujitathimini na kujiuliza ni kwanini chama chao kimepoteza kwa kasi ya ajabu haiba yake mbele ya umma wa Watanzania? Kwanini CCM ilifika huko kiasi cha Mwenyekiti wake kuagiza kila mwanachama na kila kiongozi kujitathmini na hatimaye kila mmoja ajivue gamba lake, hasa baada ya chama chake kuendeshwa mchakamchaka na Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2010? Ni wazi kwamba Kinana na Mangula wanafahamu vyema ni kwanini chama hicho kilikumbwa na hali hiyo, na ni wazi pia kwamba wawili hao wanayo majibu ya swali hilo, ndiyo maana chama kiliamua kuwaita huko walikokuwa wakifanya shughuli zao binafsi ili kuja kuokoa jahazi la CCM lililokuwa likielekea kuzama! Nimewahi kuandika huko nyuma, mwaka 2006 mara tu baada ya CCM kubadilisha uongozi wa Benjamini Mkapa kwenda kwa Kikwete, hata kama sikutaja majina ya wahusika wakuu, kwamba kilichofanyika mwaka 2005/2006 ndani ya CCM, yalikuwa ni mapinduzi, lakini yaliyofanyika kidemokrasia. Baada ya kuandika kupitia makala zangu mwaka huo, nakumbuka baadaye sana aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haroub Othumani (Mungu Amrehemu), katika moja ya mada zake kuhusu hali ya kisiasa iliyokuwa inaikabili CCM katika kipindi hicho, aliwahi kulitamka pia suala hilo la mapinduzi ‘matakatifu’ yaliyofanyika mwaka huo wa 2005/2006. Kwa wasomaji wangu wenye kumbukumbu, tangu miaka hiyo, niliendelea kuhoji juu ya ujasiri wa kauli ya aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, NEC na Mkutano Mkuu, Rostam Aziz, ya kwamba “Ndiyo maana tunataka kuiondoa mijitu hii”. Naiita kauli ya kijasiri kwa sababu wakati kiongozi huyo wa kitaifa wa CCM anatokwa na kauli hiyo mwaka 2005, mbele ya waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari vya nje na ndani, mbele ya mlango mkuu wa Ukumbi wa Chimwaga ulipokuwa unafanyika Mkutano Mkuu uliomchagua Kikwete kuwa mgombea urais, mahali hapo kulikuwa pia na maofisa wa Usalama wa Taifa, akiwemo Mzee wangu Kamalamo (Mungu Amrehemu) ambaye alikuwa katikati yetu waandishi. Kauli hiyo ya kijasiri ya Rostam ilimtoka baada ya kukuta waandishi wa habari wakiwa nje ya ukumbi huo badala ya kuwa ndani. Sababu ya waandishi hao kuwepo nje hapo ilitokana na kutokuwa na vitambulisho vinavyowaruhusu kuingia ndani ukumbini. Walikuwa wamepewa vitambulisho sawa na vya Mama na Baba Lishe au wahudumu wengine katika eneo hilo la ukumbi. Wakati waandishi hao wakipaza sauti wakilalamikia hali hiyo, hali iliyovuta maofisa wengi wa Usalama wa Taifa, mara aliibuka Rostam ikiwa ndiyo kwanza anakuja kwenye mkutano huo, kabla ya kupokelewa na malalamiko hayo ya waandishi, hali iliyomkera na kutokwa na kauli hiyo. Rostam aliagiza vitambulisho halisi vya waandishi viletwe haraka, na kweli ndani ya nusu saa tu, vitambulisho vikawa tayari, waandishi zaidi ya 50 waliokuwa nje wakafanikiwa kuingia ndani ukumbini. Sina uhakika kama waandishi wenzangu niliokuwa nao pale nje, tena wengine wakiwa ni wafanyakazi katika magazeti ya chama na serikali, waliingiwa na kauli ile ya Rostam ya “Mijitu hii”. Je; ndani ya ukumbi ule wa Chimwaga mwaka 2005, ambao ulikuwa umejaa wana-CCM na viongozi wao, ‘majitu haya’ walikuwa ni kina nani hasa? Mwenyekiti Mkapa, Katibu Mkuu wake, Mangula, au wajumbe wale wa Mkutano Mkuu? ‘Majitu haya’ walikuwa kina nani? Kwa juujuu sana, nafahamu vyema misimamo ya Kinana na Mangula katika suala zima la uongozi wa kisiasa ndani na nje ya CCM. Hawa ni makomredi kweli katika siasa za nchi hii na dunia nzima. Ni wanasiasa ambao kamwe hawawezi kukubali kugeuzwa kuwa viongozi washereheshaji (ceremonial) katika suala zima la kulinda, kutetea na kusimamia misingi ya chama chao, ambayo hadi sasa imeweza kurejesha taswira na haiba ya CCM iliyokuwa inapotea kwa kasi ya ajabu. Kila mwenye milango mitano ya fahamu inayofanya kazi sawa sawa ndani na nje ya CCM, bila shaka ataamini kwamba ndani ya miaka yao hii miwili na nusu tu ya uongozi wa makomredi hao, wamekataa katakata kuwa viongozi na watendaji washereheshaji. Ni kwa sababu ya misimamo yao hiyo ya kiuongozi, CCM hii ya sasa iko katika mikono salama, hasa baada kuwazima kisayansi vinara wakuu wa mapinduzi yale ya 2005/2006, yaliyokisababishia chama hicho kupata wakati mugumu katika ushindi wake wa 2010. Kwa sasa naziona dalili za baadhi ya vinara wa mapinduzi yale ya mwaka 2005 waliokuwa wamesambaratishwa kisayansi na kina Kinana na Mangula, wakirejea tena kupitia mlango wa nyuma. Miongoni mwa vinara hao, wapo waliojiapiza kwa viapo vikali vya kwamba wamechoshwa na siasa uchwara za ndani ya CCM, wakaamua kujivua nyadhida zao zote walizokuwa nazo ndani ya chama hicho, kuanzia ubunge hadi ujumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Naamini katika msemo wa kwamba kamanda kamili huwa hakimbii vita katikati ya uwanja wa mapambano. Kutokana na imani yangu hiyo, siwatarajii hata kidogo, Kinana na Mangula, kwa ukomredi wao usioyumba, wafike mahali wasalimu amri kirahisi dhidi ya vinara hao wa ‘mapinduzi’ waliorejea kupitia mgongo wa mmoja wa watia nia hiyo ya urais ndani ya chama chao. Hata hivyo, kama maji yatazidi unga, ikatokea viongozi wenzao wakaonyesha ukinyonga na ukondoo uliojivika ngozi ya chui, ni wazi watalazimika kujiuzulu nafasi zao hizo, hivyo kuwaachia wenye nguvu za fedha watekeleze dhamira yao ya kukiteka tena chama, safari hii kwa lengo la kuiondoa ‘mijitu’ kama kina Kikwete, Kinana na Mangula. Tumemsikia mzee mmoja wa CCM, ambaye wakati mwingine angeweza kufikiriwa na chama chake hicho kupewa viatu vya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ili avivae, akijiapiza kwenye mikutano ya hadhara, akisema hatakubali kuona wala kusikia mtu wake akikatwa jina na kikao chochote cha juu cha CCM. Mwaka 1995, wakati wa mchakato kama huu ndani ya CCM, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyeree alikuwa anamuunga mkono zaidi Benjamin Mkapa miongoni mwa makada wote takribani 11 waliokuwa wamechukua fomu za kuomba nafasi hiyo. Mwaka huo, Mwalimu aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika hoteli ya Kilimajaro, Dar es Salaam. Kabla ya kuanza mkutano ule, kukawa na minongono ya hapa na pale kutoka miongoni mwa wanahabari, iliyokuwa ikitaja majina ya wagombea urais. Baada ya kusikia minongono hiyo iliyokuwa ikitaja majina ya wagombea urais ndani na nje ya CCM, mara moja Mwalimu alikasirika, akawaambia waandishi wale kwamba kama kuna yeyote amekuja pale kwa lengo la kumsikia akitaja jina la mgombea, achukue notebook yake aondoke. Akasema hakuja pale kuzungumzia majina, bali masuala ya kitaifa na sifa za rais ajaye wa kipindi kile! Leo hii, Kingunge Ngombare-Mwiru, mzee anayeheshimika ndani ya chama chake kiasi cha kuweza kufikiriwa kuvaa kiatu cha Mwalimu katika suala zima la ushauri wa kisiasa, amejitokeza hadharani na kujiapiza kwamba hatakubali kuona jina la mtu wake likikatwa. Kingunge, tofauti na ilivyokuwa kwa Mwalimu na Mkapa mwaka 1995, yeye bila haya wala soni ameamua kumtaja na kumpamba kwa kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa mtu wake, miongoni mwa wanachama wenzake 42 waliojitokeza. Nimeambiwa kwamba baada ya kauli hiyo, sasa anadai kuwa ulimi wake uliteleza. Ama kweli adui muombee njaa! Kingunge huyu aliyemchanachana vibaya Edward Lowassa mwaka 1995 ndani ya Kamati Kuu na mbele ya Baba wa Taifa, akisema hana hata chembe moja ya sifa za kuwa kiongozi mkuu wa nchi hii kupitia tiketi ya CCM, chama ambacho ni cha Wakulima na Wafanyakazi, leo hii anamuona anafaa kwa sababu tu Mwalimu yuko kaburini! Kweli? Halafu kesho? Hata hivyo, wakati nikiendelea kumtafakari Kingunge, mzee mwenzake, Pius Msekwa, amenifariji. Akihojiwa na Kituo cha Redio Clauds wiki iliyopita, Msekwa amesema: “Katika sifa hizo (za anayefaa kuwa rais kwa tiketi ya CCM), ipo sifa ya kukubalika. Lakini si kukubalika kwa maana ya kutumia njia mbalimbali hata zile zisizo halali. Sifa inataja kukubalika kwa maana unazo sifa za kukubalika. “Lakini kama binadamu unaiba, unafanya makosa, unapaswa kuadhibiwa tu...kila mmoja wao (watia nia), anapaswa kutii miiko ya chama, anapaswa kutii kiapo chake cha utii kwa chama chetu”. Nihitimishe kwa kusema kuwa kama mchakato mzima wa uteuzi ndani ya CCM utajazwa hekima hizi za Mzee Msekwa, za mwizi au fisadi kupewa haki yake hiyo, mvunja miiko na viapo kwa chama chake naye akapata haki yake stahiki, ni wazi kwamba hakutakuwa na sababu ya Kinana na Mangula kujiuzulu katika mchakato huu ulioko mbele ya chama chao, na ni wazi pia atateuliwa mtu chaguo halisi la Watanzania walio wengi. Kila la Kheri CCM, Mungu endelea kuibariki Tanzania
No comments:
Post a Comment