Sunday, February 14, 2016

CUF kususia marudio ya uchaguzi Zanzibar

CUF kususia marudio ya uchaguzi Zanzibar


Seif
Image captionChama hicho kimesema uchaguzi halali ulishafanyika mwaka jana
Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza kwamba hakitashiriki uchaguzi wa marudio ambao umepangiwa kufanyika Machi 20.
Viongozi wa chama hicho wamesema uchaguzi halali ulishafanyika mwaka jana.
Chama hicho kimesisitiza kwamba mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba anafaa kutangazwa.
“Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani uchaguzi halali ulishafanyika,” taarifa ya chama hicho baada ya mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa inasema.
“(Baraza la CUF) linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.”
Chama hicho kimesisitiza msimamo wake wa awali kwamba haikuwa halali kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi.
Chama hicho pia kinaonekana kutoridhishwa na mchango wa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli katika kuutafutia ufumbuzi mzozo wa uchaguzi Zanzibar.
“Baraza Kuu linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anajiweka vipi na kutoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama vya CUF na CCM ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu,” imesema taarifa hiyo.
Mapema mwezi huu, chama hicho kilitahadharisha kwamba huenda kukazuka fujo uchaguzi ukirudiwa.

No comments:

Post a Comment