Udogo si hoja bali dhamira ya utumishi -Kigwangalla
Dk Kigwangalla alikamilisha ziara yake wilayani Mbeya kwa kupata jumla ya wadhamini 30 waliofika kwenye ofisi za CCM wilaya ya Mbeya zilizopo Sabasaba jijini hapa.
Akizungumza na wanachama waliojitokeza kumdhamini, Dk Kigwangalla aliwataka Watanzania kutombeza kwa umri wake na pia uzoefu mdogo alionao katika siasa bali wajikite katika dhamira yake ya kuwatumikia kupitia nafasi ya urais.
Alisema kati ya watia nia waliochukua fomu ndani ya CCM kuwania nafasi ya urais ni makada wanne tu walio na uzoefu mkubwa, lakini na akasisitiza kuwa kiongozi anayetakiwa sasa ni mwenye fikra mpya nguvu mpya na watu wapya.
Mbunge huyo alisema ingawa anatambua kuwa chama kitatengeneza ilani ambayo mgombea atakayepitishwa atainadi pamoja na wagombea wa ngazi zote lakini yeye binafsi anayo nafasi ya kukishauri chama kuhusu vipaumbele vinavyotakiwa kwenye ilani hiyo.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni uchumi ambao kama akipewa ridhaa na hatimaye kuwa Rais atahakikisha anatengeneza uwezo wa wananchi kuweza kujiajiri wenyewe na kipaumbele kikubwa katika ajira kitakuwa kwenye kundi kubwa ili kupunguza pengo la wenye nacho na wasio nacho.
Jambo la pili ni huduma za kijamii kama vile afya, elimu na maji ambazo atawekeza nguvu zaidi katika kuboresha shule na vyuo vya serikali ili kuleta usawa.
Dk Kigwangalla aliongeza kuwa kipaumbele cha tatu ni ataboresha utawala bora kwa kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kusimamia nidhamu ya kazi kupambana na ubadhirifu, ufisadi na rushwa kwa kuiongezea nguvu Takukuru ili iweze kuwafikisha mahakamani wala rushwa bila kupitia njia zingine.
No comments:
Post a Comment