WATATU WATIWA MBARONI JIJII DAR ES SALAAM KWA TUHUMA ZA MAUAJI
Mnamo tarehe 02/02/2015 majira ya saa za mchana mtoa taarifa alifika kituo cha Polisi na kueleza kwamba marehemu ANNA D/O MIZINGI aliondoka tangu tarehe 26/12/2014 majira ya saa 1:00hrs akiwa na mmoja wa watuhumiwa wakitumia gari dogo aina ya Toyota Verosa ambayo namba zake hazikufahamika mara moja iliyokuwa inamilikiwa na marehemu na tangu wakati huo hakuwa ameonekana tena.
Kutokana na taarifa hizo Jeshi la Polisi lilifungua jalada la uchunguzi na kuanza uchunguzi mara moja. Wakati uchunguzi ukiendelea zilipatikana taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa hao huko Uchira Miwaleni, Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Watuhumiwa walipokamatwa na kuhojiwa mtuhumiwa mmoja kati ya hao watatu amekiri na kutoa maelezo kuwa siku ya tukio aliondoka na marehemu kuelekea katika shule ya Mt. Zion. Kwamba walipofika shuleni hapo walivamiwa na watu wapatao wanne na kuanza kupigwa lakini yeye alifanikiwa kutoroka na kujificha katika uzio wa shule hiyo. Amesema akiwa katika uzio huo aliwaona watu hao wakiendelea kumpiga marehemu ANNA D/O MIZINGI na kisha kumtupa katika shimo la choo. Baada ya kitendo hicho watu waliotenda uhalifu huo waliondoka na gari la marehemu na kutokomea kusikojulikana.
Tarehe 22/06/2015 mabaki ya mwili wa marehemu ANNA D/O MIZINGI yalipatikana eneo la Ununio baada ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zima moto kubomoa shimo la choo cha shule hiyo.
Watuhumiwa waliokamatwa ni hawa wafuatao:1. DANIEL S/O RANADHANI MKILINDI @ ABDALLA @ DULLA, Miaka 25, Mganga wa kienyeji, Mkazi wa Uchira Moshi – Kilimanjaro.
2. SAID S/O RASHID OMARY @ SAID NTIMIZI au DUVII, Miaka 34, Mfanyabiashara, Mkazi wa Mbweni JKT.
3. ERICK S/O MZIRAY, Miaka 40, Mfanyabiashara, Mkazi wa Kurasini.
Watuhumiwa hawa wanaendelea kuhojiwa ili kupata undani wa tukio hili ikiwa ni pamoja na kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaohusiana na tukio hili. Mara baada ya uchunguzi kukamilika jalada la shauri hili litapelekwa kwa mwanasheria wa serikali kwa hatua zake za kisheria.
S. H. KOVAKAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUMDAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment