Tuesday, June 30, 2015

WALIMU WAPYA WAKAMATWA KENYA.

WALIMU wawili wapya wa Shule ya Msingi Sang’ang’a kata ya Pemba tarafa ya Inchugu wilayani Tarime, mkoani Mara wanashikiliwa nchini Kenya kwa kosa la kuingia nchini humo bila kuwa na kibali.
Walimu hao wawili ambao ni Ahedius Orio kutoka mkoa wa Kilimanjaro na mwenzake Elias Nandi kutoka Lindi wanashikiliwa na polisi nchini Kenya walipokwenda nchini humo kwa matembezi.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Sweetbard Njewike alithibitisha kukamatwa kwa walimu hao wawili wapya wa shule ya msingi Sang’ang’a iliyopo umbali wa kilometa moja kutoka mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kamanda huyo alisema walimu hao katika kipindi hiki cha likizo, mwishoni mwa wiki waliamua kwenda kutembelea kijiji jirani cha Nyametaburo Kipimo ambacho kiko upande wa Kenya.
Alisema wakati wakiwa kijijini hapo walikutwa na Polisi wa nchi hiyo na kuwapeleka, kituo cha Polisi na Uhamiaji cha Isebania kuwahoji ambapo ilidaiwa waliingia nchini humo bila ya kufuata taratibu za kuwa na vibali vya kuingia nchini humo.
“Tumewasiliana na wenzetu wa nchini Kenya ambapo wamedai kuwapeleka mahakamani kujibu shitaka la kuingia nchini humo bila vibali na wanatakiwa ndugu zao ama marafiki wakawadhamini huku juhudi za kuwasaidia walimu hao zinafanyika ili waweze kuachiliwa,” alisema Njewike.
Awali habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya Kenya, ikiwemo televisheni na redio za Citizen zilitangaza kuwa walimu hao walidaiwa kuwakusanya na kuwashawishi vijana wakiwemo kutoka Tanzania na Wakenya kujiunga na vikundi vya kigaidi vya al Shabaab.
Hata hivyo, taarifa hizo zinapingana na hali halisi kwani walimu hao ni wageni wa maeneo hayo na waliingia bila vibali kutokana na mazoea ya wanavijiji vya mipakani mwa Tanzania na Kenya ambapo baadhi ya makabila yaliyopo katika nchi hizi mbili hutembeleana bila ya kuwa na vibali vyoyote vile.
Njewike alisema walimu hao walifuata mkumbo huo wa wakazi wa maeneo hayo na kujikuta wapo mikononi mwa vyombo vya dola, hadi jana bado walimu hao wapo chini ya ulinzi nchini Kenya.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wilayani Tarime (CWT), Shirikisho Nyagosalima alisema kuwa walimu wilayani hapa wanachangishana fedha ili waende nchini Kenya kwa ajili ya kuwawekea dhamana walimu hao ambao bado ni wageni katika maeneo yao ya kazi.

No comments:

Post a Comment