Friday, June 17, 2016

PEMBA WAMUOMBA KAMISHNA WA POLISI KIKOSIKAZI KWA AJILI YA UPELELEZI NA UKAMATAJI WA WANAOFANYA HUJUMA KWENYE MAZAO


Polisi+Zenji+PHOTONa Masanja Mabula –Pemba
SERIKALI  katika   Wilaya  ya Wete , imemuomba Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar kuleta kikosi kazi cha Polisi Kisiwani Pemba kwa ajili ya kusaidia  upelelezi na ukamatwaji wa watu wanaofanya hujuma za kuharibu vipando na mali za wananchi .
Mkuu wa Wilaya ya Wete  , Rashid Hadid Rashid aliyasema hayo baada kutembelea shamba la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba  Dadi Faki Dadi lililoko Finya Mianzini , kukatwa minazi 46 , mikarafuu 5 na mashina ya mihogo 51.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa ombi hilo  kufuatia vitendo hivyo kuongezeka kila uchao na kusababisha hasara kwa wenye mali na Taifa kwa ujumla, jambo ambalo linaweza kudhoofisha uchumi wa nchi na wananchi wake .
“Kutokana na kuongezeka kwa matukio ya hujuma , iko haja kwa Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar kuleta kikosi kazi kwa ajili ya kufanya upelelezi ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ”alisema Mkuu wa Wilaya .
Aidha  Mkuu huyo wa Wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati na ulinzi na usalama  amelaani vikali vitendo hivyo vya hujuma vinavyofanywa na watu wasiojulikana na kuvitaja kwamba ni njama za makusudi zinazofanywa na baadhi ya watu kwa misingi ya itikadi za kisiasa .
Akitoa taarifa  kwa kamati ya Ulinzi ya Ulinzi na Usalama , Mlinzi wa Shamba hilo Ali Naulima Ulamu alisema , hujuma hizo alizibaini baada ya kufika katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli za kilimo majira ya saa kumi na mbili (12) asubuhi .
Ulima alifahamisha kwamba bado hajawabaini watu waliohusika na kitendo hicho ambapo , alichukua hatua ya kumupa taarifa Sheha pamoja na mmiliki wa Shamba kuhusiana na hujuma hizo  .
“Nilibaini kuwepo na uharibifu huu majira ya saa 12 asubuhi baada ya kufika kwa ajili ya shughuli za kilimo , lakini nilichokifanya ni kutoa taarifa Serikalini pamoja na kumpa taarifa mmiliki wa shamba ”alieleza.
Kwa upande wake mmiliki wa shamba hilo Dadi Faki Dadi aliwataka wananchi kuwa na  hofu ya Mungu kwa kuhakikisha wanajiepusha matendo ambayo yanakinzana na Haki na Binadamu na utawala wa misingi ya Sheria .
Alieleza kwamba ni jambo la kushangaza kwa muumini wa dini kutekeleza vitendo vya kuhujumu mali za mwenzake hasa katika kipindi hichi cha mfungo wa mwezi  mtukufu wa Ramadhan  .
Aidha amewashauri viongozi wa dini kutumia fursa waliyonayo kwa kutenga muda wa kuyaungumzia matendo hayo wakiwa katika sehemu zao Ibada , ili waumini waweze kutambua athari zake .
Hili ni tukio la nane kutokea katika Wilaya ya Wete la kuhujumiwa kwa mali , mazao na vipando vya wananchi ikiwemo uchomaji moto nyumba , mashamba ya mikarafuu , majengo ya Serikali , kufyekwa kwa mashamba ya mipunga na kung’olewa kwa vipando   baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu wa marejeo uliofanyika machi 20 mwaka huu .
Tangu kuanza kutokea kwa matukio hayo katika Wilaya hiyo , hakuna mtu au kikundi cha watu waliokamatwa wakihusishwa na hujuma hizo .

No comments:

Post a Comment