Sunday, May 1, 2016

Mwasomola na somo la sauti kuu.

SAUTI KUU AU KILIO KIKUU CHA MWISHO

imeandaliwa na Mch. Kenani Mwasomola, Uwakili - SHC

Fungu kuu: Ufunuo 18:1 – 5. “Baada ya hayo naliona Malaika mwingine,
akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi
ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, umeanguka
maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya
kila ndege mchafu mwenye kuchukiza, kwa kuwa mataifa yote
yamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa
nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali
kwa nguvu za kiburi chake”
Utangulizi: Neno malaika, ambalo kwa kiyunani ni “angelosi”
humaanisha mjumbe au taarishi. Neon hili limetumiwa sana katika
kitabu cha Ufunuo. Mahala pengine limetumiwa kumaanisha malaika
wa Mungu watokao juu. Hawa nao ni wajumbe wa Mungu waletao
habari njema kutoka juu mbinguni kwa wanadamu. Lakini pia
wanadamu wanaomwamini Yesu na kupeleka injili ya wokovu kwa
wanadamu wenzao nao hujulikana kama Malaika – wajumbe wa
Bwana.
MALAIKA WA KILIO KIKUU: katika Ufunuo 14:8 ujumbe wa malaika wa
pili unasikika “---- umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio
mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya
ghadhabu ya uasherati wake.
Je Babeli anayetajwa kwamba umeanguka ni nini? Babeli kwangu
kabisa humaanisha machafuko. Babeli ni kanisa la kiulimwengu na
lililoenea ulimwenguni kote. Babeli imeyafanya mataifa yote kunywa
mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake ambayo ni mafundisho ya
uongo yaliyo kinyume na neno la Mungu. Hivyo Babeli huwakilisha
kanisa la kidunia tu.
Uriah Smith, The prophecies of Daniel end the Revelation
(Washington, DC: Review and Herald Publishing Association, 1994) pg.
646 – 7.
Babeli ule mji mkubwa unaundwa na makundi matatu. Hivyo dini
kubwa ya dunia hii zinaweza kupangwa katika vichwa vitatu:
1. ya kwanza na ya zamani sana na iliyoenea sana ni upagani (ukafiri
yaani ushenzi) unawakilishwa na joka.
2. Ya pili ni uasi mkubwa wa upapa, unawakilishwa na mnyama.
3. Ya tatu ni mabinti(makanisa yanayofuata uasi wa upapa) au wazao
wa kutoka kanisa la Rumi ya kiroho, yakiwakilishwa na mnyama
mwenye pembe mbili, ingawaje hiyo haichukui yote.
Vita, mateso, unafuatisha namna ya dunia hii, mtindo wa kidini
ibada ya (mali), kutafuta anasa, na kudumisha kila kosa la kanisa
katoliki, kwa huzuni hudhihirisha makanisa ya Kiprotestant kuwa
sehemu muhimu ya Babeli mkuu 2. Ujumbe wa unaanguka kwa Babeli
ulitolewa kwa mara ya kwanza mnamo 1844 na wanamarejeo watu
walioamini kuwa Yesu angerudi mnamo 22 Oktoba 1844. Huu ujumbe
ulikuwa ni onyo kwa watu ambao walikanusha na kupinga ujumbe wa
marejeo ya Yesu Kristo. Ujumbe huo utarudiwa tena kwa usahihi
kabisa na malaika mwingine ambaye awafuata wale malaika watatu
wa Ufunuo 14:6 – 12. ujumbe wa malaika wa Ufunuo 18:1 – 5
utatolewa kwa nguvu ya mvua ya masika Roho Mtakatifu
atakayemwagwa kwa wingi juu ya watu wa Mungu walio waaminifu
katika kufuata neno la Mungu na wenye imani ya Yesu.
Watu wa Mungu, wakiwa wamejazwa Roho Mtakatifu (Mvua ya
masika) watasonga mbele kwa nguvu wakitoa mwito kwa watu
walioko katika Babeli ili watoke kurudi wasije wakashiriki
maangamizo yake yaliyo ya hakika. [Uriah Smith, The Prophecies of
Daniel and the Revelation, P. 647.]
Yohana anaandika kisha nikasikia sauti nyingine kutoka
mbinguni ikisema, tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi
zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika
hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake (Ufunuo 18:4 –
5) “---- ujumbe wa malaika wa tatu utatangazwa kwa uweza mkuu na
wale wanaotoa onyo la mwisho dhidi ya mnyama na sanamu
yake” (8T 118). Matangazo hayo, yakiungana na ujumbe wa malaika
wa tatu yanakuwa sehemu ya onyo la mwisho litakalotolewa kwa
wakazi wa dunia hii (GC 604). “WATU WA Mungu ambao bado
watakuwa Babeli wataitwa ili wajitenge na ushirika wake. Ujumbe
huu ndio wa mwisho ambao utapata kutolewa kwa ulimwengu” (GC
390)
Watu maelfu kwa maelfu watatoka kutoka katika Babeli na kujiunga
na watu wa Mungu na Mungu atatia muhuri wake juu yao.
MAIGIZO YA SHETANI KABLA YA KUTIMIZWA KWA UFUNUO 18:1
Mjumbe wa Mungu, Ellen G. White anasema ya kwamba, Adui
wa roho za watu anataka kuzuia kazi hii, na kabla ya wakati wa
vuguvugu kama hilo kuja, atajitahidi kulizuia kwa kuleta uamsho wa
bandia. Katika yale makanisa ambayo naweza kuyaleta chini ya uwezo
wake wa madanyanyo atafanya ionekane kuwa mbaraka pekee wa
Mungu unamwagwa juu yao, kutaonekana kila kinachodhaniwa kuwa
ni mwamko mkubwa wa mambo ya kidini. Makutano ya watu
watashangilia wakisema kwamba Mungu anatenda maajabu kwa ajili
yao, wakati kazi hiyo ni ya roho yule mwingine. Akiwa amejificha
chini ya vazi la dini, shetani atajaribu kuueneza ushawishi wake katika
ulimwengu wote wa Kikristo (GC 464)
Kila siku watu wanasikia na pengine hata kushuhudia maajabu
yanayofanywa kwa jina la Yesu lakini kwa undani wake hasa maajabu
hayo yanafanywa kwa uwezo wa adui Ibilisi. Katika siku hizi za
mwisho shetani, kupitia watumishi wake, atafanya ishara kubwa za
uponyaji na hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya
nchi mbele ya wanadamu. Naye atawakosesha wale wakaao juu ya
nchi kwa ishara zile alizopewa kuzifanaya (Ufunuo 13:13,14). Watu
wengi watakoseshwa kwa ishara hizo na maajabu hayo. Lakini watu
wa Mungu kamwe hawatashibishwa. Daima wao watakumbuka, hata
ishara kubwa na maajabu yasiyo ya kawaida yatakapotendeka mbele
ya macho yao, neno lao ni moja tu, imeandikwa na waende kwa
sheria na ushuhuda, ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, kama
mtu anayefanya ishara za uponyaji, unenaji wa lugha, kufufua watu au
hata kushusha moto kutoka juu mbinguni, hashiki amri za Mungu
na wala hana ushuhuda wa Yesu ambao ni Roho ya unabii(Ufunuo
19:10) huyo mtu hakutumwa na Mungu na roho itendayo kazi ndani
yake siyo ya Mungu. Watu wa Mungu washikao amri za Mungu
(Ufunuo 14:12)nao watafanya ishara na miujiza. Lakini daima
watakumbuka kuwa imani yao haikujengwa juu ya miujiza na
maajabu bali imani yao imejengwa juu ya msingi wa mitume na
manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.
(Waefeso 2:20)
TUWEZAJE KUPAMBANUA KATI YA UAMSHO BANDIA WA SHETANI NA SAUTI
KUU?
Mjumbe wa Mungu, anaweka bayana ya kwamba katika
uamsho bandia, kuna msisimuko wa kihisia kuchanganya ukweli na
uongo, ambavyo vimekusudiwa kuwapotosha watu. Hata hivyo,
hakuna haja kwa yeyote kudanganyika. Katika nuru ya neno la Mungu
si vigumu wanapodharau ushuhuda wa Biblia, wakigeukia na
kuziacha zile kweli zilizo dhahiri na zenye kuupima moyo na ambazo
zinahitaji kujikana nafsi na kuukataa kabisa ulimwengu, hapo ndipo
tunapoweza kuwa na uhakika ya kwamba mbaraka wa Mungu,
haujatolewa. Na kwa kanuni ile aliyoitoa Kristo mwenyewe,
mtawambua kwa matunda yao (Mathayo 7: 16),ni dhahiri kwamba
vuguvugu hilo siyo kazi ya Roho wa Mungu (GC 464, 465)
Je Ni lini ambapo anguko la Babeli (Ufunuo 18:2) litakuwa
limetimilika hata Ufunuo 18:2 liweze kuhubiriwa kama uliotimia
kabisa? “ uliowanywesha mataifa, yote mvivyo wa ghadhabu ya
uasherati wake” (Ufunuo 14:8) Mafundisho ya uongo. Jambo hilo
linafanyikaje? Kwa kuwalazimisha watu kuikubali sabato ya uongo(8T
94) Jumapili ndiyo sabato ya uongo. Ni mpaka hapo hali hiyo
itakapofikiwa na muungano wa kanisa lna ulimwengu
utakapokamilika anguko la Babeli litakapokuwa limekamilika. Badiliko
ni la kuendelea, na utimizo kamili wa ufunuo 14:8 bado uko siku za
usoni (GC 390).
Kupitishwa kwa amri ya Jumapili kutakuwa ndiyo mwanzo wa
taabu na mateso.Lakini “mwanzoni mwa wakati wa taabu, tulijazwa
na Roho Mtakatifu tulipoondoka kwenda kuitangaza Sabato kwa
ukamilifu zaidi” (EW 33, NA 85). “Sabato hiyo ya uongo italazimishwa
kwa sheria ya ukandamizaji. Shetani na malaika zake wako macho
sana, tena wanashughulika kwa nguvu sana -----. Lakini wakati shetani
atakapofanya kazi kwa maajabu yake ya uongo, ndipo utakapotimizwa
wakati uliotabiriwa katika Ufunuo, na malaika yule mwenye mamlaka
kuu atakayeitangaza dunia yote kwa utukufu wake, atatangaza anguko
la Babeli, na kuwaita watu wa Mungu walioko huko watoke (7BC 985,
RH 13/12/1892).
SAUTI KUU ITAFANANA NA PENTEKOSTE.
Kazi hiyo itafanana na ile ya siku ya pentekoste. Kama vile
mvua ya vuli iliyotolewa kwa kumwaga Roho Mtakatifu mwanzoni
mwa kazi ya injili ili kusababisha kuchipua kwa mbegu zile za
thamani, ndivyo “ Mvua ya masika itakavyotolewa mwishoni ili
kukomaza mavuno” (GC 611)…“Kumwagwa kwa Roho katika siku za
mitume ilikuwa ni mvua ya vuli, na matokeo yake yalikuwa ya
utukufu sana. Lakini mvua ya masika itakuwa nyingi zaidi” (Ev 701).
Je, watoto wa Mungu ambao bado watakuwa Babeli
wataupokea mwito wa sauti kuu? Jawabu ni ndiyo. Mjumbe wa
Mungu Ellen White anasema, Roho zilizokuwa zimetawanyika katika
mashirika yote ya kidini ziliitikia mwito na zile zilizokuwa za thamani
ziliharakishwa kutoka katika makanisa yakwenda kuangamizwa, kama
vile Lutu alivyoharakishwa kutoka Sodoma kabla ya maangamizi yake
(EW 279). Hakuna chochote kitakachoweza kuwazuia wabakie
Babeli. Mahusiano ya kifamilia, mahusiano ya kikanisa, sasa hayana
uwezo wowote wa kuwazuia. Ukweli ni wa thamani zaidi kuliko
mengine yote.Bila kujali mawakala walioungana dhidi ya ukweli, idadi
kubwa ya watu, watachukua msimamo wao upande wa Bwana. (GC
612).
WAADVENTISTA WASABATO AMBAO HAWAJAONGOKA.
Jambo la kusikitisha, Waadventista wa Sabato ambao
hawajaongoka hawatatambua sauti kuu na wataipinga kazi
hiyo. White anasema kuwa “kutakuwa na udhihirisho wa ajabu wa
uweza wa Mungu katika makanisa yetu, lakini uweza huo hautawajia
wale ambao hawajajinyenyekeza wenyewe mbele za Bwana, na
kuifungua mioyo yao kwa maungamo na toba katika udhihirisho wa
uweza unaoiangaza dunia yote kwa utukufu wake, wao wataona tu
kuwa ni mila fulani ambacho katika upofu wao watafikiria kuwa ni
cha hatari, kitu fulani kitakachoamsha hofu zao, nao watajidhatiti
kuupinga kwa kuwa Bwana hafanyi kazi yake kulingana na matarajio
na mawazo yao, basi, wataipinga kazi hiyo. Watasema “kwa nini sisi
tusiweze kumjua Roho wa Mungu wakati tumekuwa kazini kwa miaka
mingi sana?” RH 7/11/1918…. “Dhoruba inapozidi kukaribia, kundi
kubwa la wale wanaodai kuwa na imani katika ujumbe wa malaika
wa tatu lakini ambao hawakutakaswa kwa kuitii ile kweli, wataziacha
nafasi zao na kujiunga katika safu za wapinzani” (GC 608)
Huu ndio wakati wa kila mmoja kuchukua msimamo thabiti
kuwa upande wa Bwana. Wale wanongojea wakati fulani wa pekee
ambamo watategemea tabia zao kugeuka ghafla na kuwa kama Kristo,
wakati huo hawataupata. Leo hii ndivyo nafsi na wakati wa kupata
mvua ya vuli (Roho Mtakatifu wa kwanza) tayari kwa kupokea mvua
ya masika yaani Roho Mtakatifu atakayemwagwa bila kipimo wakati
wa mwisho na atayewawezesha malaika wa Ufunuo 18:1 – 5 kupeleka
ujumbe wa onyo la mwisho kwa kishindo kikubwa sana.
“Wakati uweza wa Mungu utakapounganishwa na juhudi za
binadamu, kazi itaenea kama moto katika nyasi kavu zilizokatwa
Mungu atatumia mawakala ambao asili yao mwanadamu hataweza
kuifahamu, malaika watafanya kazi ambayo wanadamu wangeweza
kupata mibaraka ya kutimiza, kama wasingepuuzia kuitikia madai ya
Mungu” (RH 15/12/1885)
Mambo makuu ya kufanya ili kujiandaa kwa wakati huo wa mwisho:-
1. Soma neno la Mungu (Biblia) kila siku
2. Omba bila kukoma. Uwe na maombi ya mnyororo katika maisha
yako yote.
3. Fanya kazi ya kuihubiri Injili waweza kuhubiri kwa njia ya kupeleka
vitabu, sauti ya unabii, Biblia yasema, masomo ya mgunduzi,
mahubiri ya hadhara, kuonana kuombea wagonjwa hospitalini na
majumbani n.k. Mungu atatungoja sisi kama watu wake tuweze
kuifanya kazi yake kwa mali, nguvu, na akili zetu.
Wito: ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu kwa Bwana?
(1Nyakati 29:5)