Kunao wengi ambao hutaka kuwa wanamitindo watajika na hufanya kila juhudi kukita mizizi. Lakini kwa wengine, unaweza kusema wamezaliwa wakiwa wanamitindo.
Mmoja wao ni Iman, mwanamitindo msifika aliyezaliwa nchini Somalia, ambaye kwa miaka mingi ametawala katika majukwaa ya mitindo.
Mwanzoni hakujulikana lakini mwishowe aling’aa na kuvuma sana katika majukwaa na majarida ya Ulaya miaka ya 1970 na 1980, miongoni mwa majarida hayo yakiwa Vogue, Harper’s Bazaar na Yves St Laurent.
Lakini ilikuwaje hadi akajipata kwenye tasnia ya mitindo?
Mpigapicha Mmarekani, Peter Beard, ndiye hutambuliwa kwa “kumgundua” Iman. Mwanamume aliyempa fursa ya kutokea jukwaani mara ya kwanza kabisa, Alan Donovan, sana huwa hakumbukwi.
Iman, ambaye babake alikuwa mwanabalozi na mamake daktari mtaalamu wa masuala ya uzazi, alikuwa na umri wa miaka 19, wakati huo akiwa mwanafunzi Chuo kikuu cha Nairobi.
Alan Donovan, afisa wa zamani wa wizara ya mashauri ya kigeni ambaye baadaye aligeuka na kuwa mkusanyaji wa turathi na kazi za Sanaa kutoka Afrika, aliandaa maonesho ya kila mwezi ya sanaa ya Afrika na mitindo kwa jina African Heritage Night.
Aliangazia sanaa halisi ya Afrika, mavazi na vito ambavyo alivitengeneza mwenyewe.
Walikutana Iman alipotembelea hoteli ambayo makala ya tatu ya maonesho ya African Heritage Night yalikuwa yakifanyika. Alimwendea Donovan na kumuomba akubaliwe kushiriki katika maonesho ya mitindo usiku huo. Ilikuwa 1975 wakati huo.
Donovan anasema, “Alikuwa anapendeza sana na nilikubali, bila shaka. Na hapo ndipo alipoanza kufanya maonesho ya mitindo. Mara yake ya kwanza kupanda jukwaani ilkuwa wakati huo. Kwa hivyo, watu wengi walitaka kumpiga picha, akiwemo mpiga picha mashuhuri Peter Beard.”
Donovan baadaye alimpangia Iman kushiriki katika maonesho ya sanaa ya Afrika Hollywood, Los Angeles. Habari za kuwasili kwa Marekani ziliangaziwa sana na vyombo vya habari.
Jarida la The New York Post lilimweleza kama “msichana mrembo zaidi duniani”.
Wapiga picha walimzingira alipowasili mjini New York.
Hakufika maonesho hayo ya Hollywood:
“…muda mfupi baada ya kuwasili New York, alitwaliwa na wakala wa mitindo wa Wilhelmina ambaye alikuwa ameona picha zilizopigwa na Peter Beard. “
Wawili hao hawakukutana tena. Donovan anasema muda wao pamoja ulifanyiwa mzaha na gazeti moja la Kenya na kutajwa kuwa “urafiki wa siku moja”.
Alan Donovan alifika Afrika mara ya kwanza 1968 akiwa afisa wa wizara ya mashauri ya kigeni wa Marekani, akijaribu kuingiza chakula eneo la Biafra, lililokuwa limezingirwa na jeshi la Nigeria. Miaka miwili baadaye, alijiuzulu na kuanza kutembea Afrika. Alianza kukusanya na kuuza kazi za sanaa na vito kutoka kwa watu wa jamii ya Turkana, kaskazini mwa Kenya. Na hapo ndipo pendo lake kwa sanaa na utamaduni wa Afrika lilipoanza.
Alishirikiana na makamu wa rais wa zamani wa Kenya Joseph Murumbi, ambaye pia alikuwa akikusanya turathi na kazi za Sanaa za Kiafrika, na akaanzisha African Heritage, kampuni ya kuuza nje kazi za Sanaa ya Kiafrika.
Murumbi alifariki na biashara yake ikasambaratika 2003, lakini Donovan aliweka hai ndoto ya Murumbi ya kuhifadhi Sanaa na utamaduni wa Kiafrika.
Alijenga jumba karibu na mbuga ya taifa ya Nairobi, African Heritage House, ambayo inafanana na misikiti ya kaskazini mwa Mali iliyojengwa kwa matope. Jumba hilo lina turathi nyingi, vitambaa na kazi za Sanaa.
Jumba hili huwavutia watalii wa hapa nchini na hata kimataifa ambao hufika kutazama „Afrika ya zamani”.
Donovan hutumia jumba hilo kupiga mnada kazi za Sanaa kutoka wasanii wa zamani na wale waliosahaulika, na kuwasaidia kufaidi kutokana na kazi zao.
Jumba lake sasa limetangazwa kuwa turathi ya kitaifa lakini kuna hatari.
Reli ya kisasa inayojengwa kutoka Mombasa hadi Kisumu itapitia kwenye shamba lake. Hakuna ajuaye iwapo jumba lake litanusurika.
No comments:
Post a Comment