Sunday, February 21, 2016

KONA YA MAKENGEZA : Uchafuzi wa kupora mpira.......

SUNDAY, FEBRUARY 21, 2016

KONA YA MAKENGEZA : Uchafuzi wa kupora mpira



Haya ndugu wasikilizaji karibuni sana kwenye mechi ya watani wa jadi. Tena leo mechi imeshapata vuguvugu ya ziada kutokana na mtani mmoja kutangaza kwamba kwa vyovyote vile hawezi kukubali kushindwa. Sisi tulijua kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani, lakini tuna wasiwasi kwamba timu moja imeingiliwa na sera za kisiasa. Lakini mambo yote tisa, kumi kwenye boli. Timu zote mbili ziko tayari na … mpira umeanza.
Fulani amechukua mpira, anampita wa kwanza, wa pili, wa tatu lakini weeeeeeeee kuna nini tena. Yule wa tatu katoa rungu na kumpiga mwenzie kichwani, tena palepale kwenye eneo la kumi na nane. Refa amefika pale na ni PENALTIIII. Ndiyo, na yule wa rungu keshaonyeshwa kadi nyekundu.
Lakini ngoja. Ngoja. Ndugu wasikilizaji nashindwa kuamini. Refa naye kapigwa rungu hadi damu inatiririka na kadi nyekundu imegeuzwa kwa yule aliyepigwa. Ndiyo aliyepigwa anatolewa nje kwa kubebwa huku akifuatwa na kadi nyekundu ya refa mwenye uso mwekundu.
Bila shaka mnasikia kelele. Mashabiki wamekasirika! Wamekasirika. Wanataka kuvamia uwanja lakini kuna kelele kubwa zaidi. Hapana. Siamini. Vifaru vinaingia uwanjani na vimeanza kupiga maji ya kuwasha na mabomu ya machozi. Watu wanakimbia ovyo lakini … aaaagh machozi haya … jamani … baad….a…. ye.
Haya, haya, haya ndugu wasikilizaji. Tunaomba radhi sana kwa yale yaliyotupita. Bila hata kuathiriwa na mabomu ya machozi, tusingeweza kuendelea kutangaza maana kumbe yule mtani asiyeshindwa hana utani. Chumba chetu cha kutangazia kilijaa wanausalama wao wakitaka kujua nani kapendelea, nani kataja rungu. Sisi tukabaki tunakohoa tu hivyo mwisho walituacha kwa kutuonya kwamba macho yetu yasiwe na upendeleo. Hata tukiona kitu kibaya, tujiulize kama kweli tumeona au tunahitaji rungu ili tuone vizuri.
Sasa wachezaji wako uwanjani tena. Hata yule wa kadi nyekundu karudishwa ingawa nahisi anayumbayumba kidogo maana kile kipigo cha ru … cha … cha … alivyogonganisha kichwa kwenye kitu kisichojulikana imemwathiri. Nasikia walifanya kikao huko kwa refa wakati anafunga bendeji. Eti kila timu icheze sawasawa na mshindi atapatikana kwa ufundi si ubabe. Wachezaji wengine walitaka kukataa kucheza maana ilionekana wazi kwamba ni kupoteza muda kucheza na timu ambayo haiheshimu sheria na kung’ang’ania ushindi. Lakini wenzao wamewashawishi, eti ni timu nzuri na mashabiki wanataka wacheze hivyo bora wacheze. Mmmh. Sijui
Na sasa mpira umeanza na watani wababe wanaelekea goli kwa mwendo wa kasi sana. Inaonekana hakuna aliye tayari kuwazuia … goooooooooo. Wanafunga goli ya kwanza. Tena shuti ilikuwa hafifu sana lakini golikipa ni kama hakuona akaruka kushoto wakati mpira unaingia kulia.
Na hapo wanabishana wenyewe kwa wenyewe. Wapo ambao hawakubali kabisa udhaifu huo, kwa hiyo wameshika mpira na kurudi kati na mpira umeanza tena. Fulani kaenda tena, kaenda, kaenda, mchezaji mmoja akatoa kitu kinachofanana na ru … lakini amepiga chenga, na mara ya pili, anapiga chenga licha ya mvua ya marungu na …. Goooooooooooooo … hapana ndugu wasikilizaji siyo goli. Siyo goli. Jamaa kapiga shuti safi sana lakini beki wa kulia akadaka mpira kwa mkono na sasa anakimbia na mpira mkononi. Nakuambia mpira wa mguu umegeuka mpira wa mkono. Refa amepuliza kipenga na anamkimbilia lakini ameshaangushwa na mwana usalama ambaye amemkalia asiweze kufanya kitu. Basi aliyeshika mpira anapita tu. Anapita na mwisho anakimbia hadi kuingia kwenye goooooooooooooo!
Mbili bila wapenzi wasikilizaji lakini naona sasa mambo yanaanza kuchafuka. Mashabiki wanakuja juu na wana usalama wa watani wababe nao wamejitokeza tena na mabomu yao. Ni vurumai wapenzi wasikilizaji. Kweli kuna timu moja ambayo haikubali kushindwa. Lakini mashabiki bado wanataka mechi iendelee.
‘Tutawashinda tu. Tutawashinda tu.’
Ndivyo wanavyosema lakini samahani ndugu wasikilizaji naona nalengewa na rungu pi …. PAAAAA.
Samahani ndugu wasikilizaji imebidi tuwarudishe studio kutokana na makosa ya kiufundi.
Mnasikia jamani? Michezo ikiingiliwa na kanuni za siasa, haitakuwa hivyo? Nadhani ndiyo maana nilipata barua kutoka kwa mtu mwingine.
Imetosha! Hatimaye majirani zetu wamenishawishi kukubali. Uchaguzi wa nini wakati ni uchafuzi mtupu? Tena nashindwa kuelewa kwa nini chama fulani au wapenzi wa chama fulani wanajisumbua na kujiumbua kuendelea na mchakato wa uchaguzi huku mwenye nchi na wenzake wameshatangaza hawawezi kuachia ngazi. Sasa wengine wanategemea nini? Kwamba muujiza utatokea na huyu mng’ang’anizi atapigwa chini kama Saulo kwenye Biblia na kuona mwanga wa demokrasia. Haiyumkiniki.
Au mnaompinga anayeshika vyombo vyote vya dola, vya wazi na kificho, mtapata kura za kumshinda huku akiwa na uwezo wa kutengeneza kura za sura, na vituo vipya na kuteketeza hata kura za kwako. Mtapata wapi? Na mnafikiri ataona aibu baada ya kuumbuliwa kwamba amejazilia kura kwenye kituo fulani kiasi kwamba, ingawa kituo kina wapiga kura 300, kura za mwenye nchi zimefikia l00,000. Hawa hawana haya.
Ndiyo. Mnategemea nini wakati wanatangaza kabisa kwamba katika chafuzi za aina hiyo, wanaopiga kura si muhimu, wanaohesabu kura ndiyo waamuzi. Hata hapa tunaye aliyesema hivyo. La muhimu ni jinsi ya kuhesabu kura. Na sisi tunajua kuhesabu. Kama wanasema hivi, waziwazi, bila aibu wala soni wala haya, mnapoteza muda wa nini? Ni sawasawa na kuingia kwenye mechi ya mpira huku timu moja inavunja sheria zote. Kweli utaendelea kucheza katika hali hii? Kwa nini kwenye mchezo mchafu wa uchafuzi tunakubali basi?
Kweli Makengeza, nimenyanyua mkono, nimekata tamaa, sioni sababu ya kushiriki tena. Siongelei matumizi ya nguvu. Watu wanajeruhiwa, wanapata ulemavu wa kudumu na hata kukatishwa maisha bila sababu, lakini hayo tumezoea na tunaamini wengine wakijitoa muhanga, mwisho tutashinda. Tunajivunia jinsi tulivyo wataalamu wa kuhimili mabomu ya machozi na tunaendelea kurukaruka kama kuku mbele ya nyoka. Imani ya kushinda inatoa nguvu ya ziada.
Ndipo hapo nina shida moja ya kimsingi zaidi, maana matamshi haya ya kwamba ‘nilipata nchi hii kwa tabu au mtutu wa bunduki au matumizi ya nguvu unafikiri nitaiacha hivihivi’ yamezidi kuenea. Nadhani yalianzishwa na Meles Zenawi huko Ethiopia na sasa yamekuwa kama ugonjwa wa kuambukiza na sisi sote tunaangalia tu. Hatuchukui hatua yoyote ya maana wakati matamshi haya yameshanajisi si tu mchakato wa uchafuzi wa hapa au kule au kwingineko, bali hata maana ya demokrasia.
Ndiyo maana najiuliza watu wataamka mwaka gani?
Gwiji wa mapinduzi alitamka kwamba dini ni bangi ya wananchi. Na kweli inaendelea kuwa bangi kwa watu wengi sana.
Wanaamini manabii ambao hawana lolote zaidi ya uwezo wa kuigiza hadi wanaacha dawa na kufa, hadi wanatoa senti zao za mwisho ili mchungaji wao akaribie mbinguni kwa ndege ya fahari. Bangi kwelikweli.
Inavuruga kabisa akili za watu.
Lakini sasa naona hata uchaguzi ni bangi ya wananchi. Hebu angalia. Hata kama walijua safari iliyopita mambo yalichakachuliwa hadi basi, safari hii watajitokeza tena, watatengeneza nyomi, watasahau njaa na kiu na matatizo yao yote katika imani kwamba safari hii mambo yatakuwa tofauti.
Ukiangalia kisayansi, huu utofauti umejitokeza wapi? Hasa kama mwenye nchi ameshikilia nchi na vidole vya chuma na kutangaza haachii hata kama hakupata kura kabisa. Yaani hawa wengine wote wameturudisha katika enzi za ukabaila. Wafalme huchaguliwa na Mungu wewe binadamu ni nani kupinga? Ndivyo walivyo na sisi tuko tayari kucheza mchezo huo wa danganya toto.
Hadi lini?     

No comments:

Post a Comment