Majeshi ya Riek Machar kushika doria Juba
Wapiganaji wanaomuunga mkono kiongozi wa upinzani ambaye pia ni naibu wa kwanza wa rais wa Sudan Kusini , Riek Machar, wataanza kushika doria katika mji mkuu wa Juba kuanzia mwezi ujao.
Hii itakuwa ndio mara ya kwanza kwa wapiganaji hao watiifu kwa Machar kuingia Juba tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe Desemba mwaka wa 2013.
Mapema mwezi huu rais wa Sudan Kusini Salva Kiir alimteua bwana Machar kuwa naibu wake kama sehemu ya mapatano ya kusitisha vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilianza kwa kufutwa kazi kwa bwana Machar.
Maelfu ya watu wameuawa kufuatia machafuko yaliyotibuka.
Mamilioni ya raia wa taifa hilo changa zaidi duniani wamelazimika kukimbilia usalama wao katika mataifa ya nje.
Takwimu za afisi ya umoja wa mataifa inayoshughulikia swala la wakimbizi inaonesha kuwa zaidi ya watu milioni mbili walitoroka makwao kufuatia mapigano kati ya wanajeshi watiifu kwa rais Kiir na wapiganaji wanaomuunga mkono bwana Machar.
Mapatano ya awali kati ya mahasidi hao wawili yalivunjwa na sasa wadau wanaimani kuwa amani itadumu kutokana na ishara zilizoko sasa.
No comments:
Post a Comment