Buriani Makongoro Oging’
TAGS
Mwandishi Makongoro Oging’ enzi za uhai wake. “Makongoro Oging’ amefariki dunia,” yalikuwa ni maneno yaliyopenya
masikioni mwangu kutoka kwa Oscar Ndauka, Mhariri Kiongozi wa Global
Puplishers alipofika nyumbani kwangu Jumamosi usiku wa Mei 21,
mwaka huu akiwa na Sifael Paul, Mhariri wa Gazeti la Ijumaa Wikienda. Nilipigwa na butwaa kusikia habari hiyo ambayo kama ningekuwa na
matatizo ya kiafya ningeweza kupata presha, huku mke wangu akishikwa
na mshangao na akihoji kama vile hakusikia: “Makongoro kafariki duni?”
Tar 14.8.2015 Makongoro akimuhoji mke wa aliyekuwa askari wa gereza
la Dondwe Pwani ambaye aliuawa katika uvamizi wa kituo cha Stakishari,
Picha na Richard Bukos. Nilimuona akifuta machozi kwa khanga, kisha nami nikachukua kitambaa na
kufuta machozi. Tulizungumza mengi hadi saa nane usiku kupanga tufanyeje
kesho kukicha baada ya kuzungumza na mke wa Makongoro usiku huo huo
na kututhibitishia habari hiyo. Jina la Makongoro Oging’ siyo geni kwa watu wanaofuatilia habari hasa
wasomaji wa magazeti ya Global Publishers hususan Gazeti la Uwazi. Ni juzi tu aliniletea fomu zake za kutaka press card na alipoijaza ikaonesha
kuwa yumo ndani ya tasnia ya habari kwa miaka 21 sasa, hivyo kutosha
kusema kwamba ni mkongwe katika fani hii. Makongoro alikuwa mahiri wa kuandika habari za uchunguzi kwani mwaka
2004 alipewa tuzo ya mwandishi bora wa habari hizo, iliyotolewa na Chuo
cha Uandishi wa Habari cha Royal Tanzania kilichopo Ubungo, Dar es
Salaam. Miongoni mwa watu waliotunukiwa tuzo siku hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya
Mvomero, Betty Mkwasa pamoja na waandishi wa habari wengine ambao
majina yao siwezi kuyakumbukwa kwa sasa.
Alistahili kwa sababu Makongoro alipokuwa kazini hakuwa na mchezo.
Alikuwa akifuatilia habari za uchunguzi kwa kina. Nakumbuka siku moja
aliandika habari moja ya udhalilishaji uliofanywa na vijana fulani baada ya
kumteka msichana mmoja na kumpiga sana kisha kumvua nguo. Sakata hilo lilifika jeshi la polisi wakati huo Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalum, Kamishna Mstaafu Alfred Tibaigana akiwa madarakani alinipigia
simu na kunitaka niende na Makongoro ofisini kwake ‘ sentro’. Tulipofika tu akatuona tupo kwenye korido akasema kwa sauti, “Kamanda
Zombe ( Abdallah), watu wa Uwazi wamefika, Makongoro uliyekuwa
ukimtafuta huyu hapa, kaja na bosi wake.” Zombe aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa polisi wa kanda maalum ya Dar es
Salaam wakati ule, alikuwa kwenye chumba kimoja na aliposikia sauti ya
bosi wake alitoka na kutulaki huku akitukaribisha.
“Karibuni sana.” “Ahsante.” “Tumekuwa tukifuatilia gazeti lenu la Uwazi na habari ya wiki hii ipo mezani
kwangu naomba mtusaidie mawili matatu,” alisema Zombe. Baadaye alitukabidhi kwa askari mmoja wa upelelezi ambaye namkumbuka
kwa jina moja tu la Judi ili tufanye naye mahojiano. Judi alituchukua hadi ofisini kwake na kuanza kunihoji mimi kwa dakika
chache kama mhariri wa habari ile na baadaye akaanza kumhoji Makongoro
ambaye alichukua muda mrefu kutokana na mambo mengi ambayo alikuwa
anayajua kuhusiana na habari ile.
Baada ya mahojiano yale Kamanda Tibaigana alituita ofisini kwake na kusifia
umahiri wa Makongoro katika kuandika habari za uchunguzi na akasema
huwa zinamsaidia sana katika uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ambazo
zinawafikia. Tangu siku hiyo Makongoro Oging akawa rafiki wa Tibaigana na Zombe
pamoja na askari wengine wengi pamoja na mawakili akiwemo Mabere
Marando hali iliyofanya awe mahiri wa kuandika habari zinazohusu
watuhumiwa mbalimbali. Ilikuwa siyo rahisi kwa Makongoro kwenda kwenye kituo fulani cha polisi na
kukosa ushirikiano anapofuatilia jambo kutokana na uhusiano mzuri
alioujenga na askari hao hata wale wa Magereza na Kikosi cha Zima Moto.
Kwa upande wa wagonjwa katika hospitali mbalimbali, Makongoro alikuwa
akiwaandika sana na kuwaombea misaada kwa wasomaji wa Gazeti la Uwazi
na alifanikiwa kuwawezesha baadhi yao kupelekwa nje ya nchi kutibiwa kwa
kuchangiwa na wasomaji. Wengine walipelekwa India, wengine hospitali za humu ndani na kubadili
maisha yao baada ya kutibiwa na kupona kutokana na kalamu yake
aliyoitumia kwa manufaa ya jamii. Wapo watu ambao walikuwa na maisha duni lakini Makongoro kwa kutumia
kalamu yake aliandika habari zao na baadhi yao kufanikiwa kujengewa
nyumba za kisasa. Kwa upande wa wanafunzi, Makongoro hakuwaacha nyuma, nao alikuwa
akiwafuata na kuandika matatizo yao. Wapo waliokuwa wakikwama
kimasomo kutokana na wazazi wao au walezi wao kushindwa kuwalipia ada,
mwandishi huyu aliandika habari zao na baadhi yao wakafadhiliwa na
kusoma hadi chuo kikuu. Makongoro hakuwa mchoyo wa fani yake, nimemshuhudia zaidi ya miaka 15
akiwafundisha waandishi chipukizi habari za uchunguzi na kuwa wa
kutumainiwa katika chumba cha habari. Alikuwa akipenda kuwafundisha uandishi wa uchunguzi waandishi chipukizi
kivitendo kwani baadhi yao alikuwa akiongozana nao kwenye matukio na
kuwafundisha kivitendo jinsi ya kufuatilia habari za uchunguzi alizokuwa
akiziandika enzi za uhai wake.
Kazi yake ilimfanya ajulikane sehemu nyingi, kama vile ndani ya majeshi yetu
yote, katika hospitali kubwa, mitaani na hata kwenye mashirika na taasisi za
umma na zile binafsi. Alikuwa jasiri kwa kufuatilia jambo bila woga na ndiyo maana mpaka anaaga
dunia Jumamosi saa moja jioni hatukuwahi kuwa na kesi kwenye gazeti
iliyosababishwa naye. Makongoro ameacha mjane na watoto watatu. Mungu ailaze roho yake
mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment