Sunday, February 21, 2016

KAMANDA KOVA KIZIMBANI..............

MVUTANO WA SHERIA WATAWALA KESI YA KAMANDA KOVA NA NZOWA......MAKAMANDA HAWA WANAGOMBEA NYUMBA YA SERIKALI ALIYOUZIWA KOVA


Mahakama ya rufani jana imeanza kusikiliza kesi ya viongozi wawili waandamizi wa polisi, Kamishna mstaafu, Suleiman Kova na Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Godfrey Nzowa wanaogombea nyumba ya Serikali.

Katika rufani hiyo, Nzowa anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, kumpa haki ya kumiliki nyumba ya Serikali, Kova ambaye ni mlalamikiwa wa kwanza katika kesi hiyo. Mlalamikiwa wa pili ni Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA).

Nzowa anapinga nyumba ambayo anaishi hadi sasa, iliyokuwa na namba 203 na baadaye kubadilisha kuwa namba 140 kuuziwa Kova kwa kuwa wakati tangazo la kuuzwa nyumba za Serikali linatolewa yeye ndiye alikuwa akiishi katika nyumba hiyo.

Hata hivyo, TBA ilimuuzia Kova ambaye alikuwa amehamishiwa mkoani Kigoma.

Tangazo la kuuzwa nyumba hiyo, lilitolewa Mei Mosi, 2002, wakati Nzowa akiwa katika nyumba hiyo baada ya kuhamia Arusha Januari 8, 2002.

Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za kulevya nchini na Kova ambaye amestaafu karibuni akiwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, waliwasili mahakamani jana saa tatu asubuhi.

Wa kwanza kufika alikuwa Kova akiwa anasindikizwa na watu kadhaa na baadaye Nzowa alifika akiwa ameongozana na familia yake.

Wakiwa mahakamani kila mmoja alikaa eneo lake, akifuatilia mabishano ya kisheria ya mawakili na baada ya shauri hilo kuahirishwa saa 6.25 mchana walitoka nje ya chumba cha Mahakama, kila mmoja akishauriana na wakili wake.

Pingamizi la rufani 
Kabla ya kuanza kusikilizwa rufani hiyo jana mbele ya majaji Mbarouk Salum, Benard Luanda na Mussa Kipenga, mawakili wa wajibu rufani katika kesi hiyo, wanaowatetea Kova na TBA, waliwasilisha pingamizi la kusikilizwa rufani hiyo kwa maelezo kuwa liliwasilishwa nje ya muda na lina upungufu wa kisheria.

Mawakili Dilip Kesaria na Pascal Qamala wanaomtetea Kamishna Kova na mawakili wa Serikali, Harun Matagane na Sylvester Mwakitalu wanaowakilisha TBA walieleza kuwa ni muhimu Mahakama ikaheshimu taratibu zake na kuhakikisha nyaraka zinazowasilishwa mbele yake zipo sahihi.

Wakili Kesaria alisema notisi ya kukata rufani ilitolewa Oktoba 3, 2013, lakini rufani iliwasilishwa rasmi mahakamani Januari 2, 2015 nje ya muda wa kisheria.

Mawakili hao wa walalamikiwa walieleza mkanganyiko wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani na waliiomba mahakama kuitupa rufani hiyo kwa kuwa ina upungufu ya kisheria.

Hata hivyo, mawakili Mpaya Kamara na Neema Mtayangulwa walipinga hoja hiyo wakisema hakuna dosari za kisheria katika uwasilishaji wa rufani hiyo.

Kamara alisema rufani na notisi vimefikishwa mahakamani ndani ya muda na ndiyo sababu Msajili wa Mahakama alivipokea.

Alisema kama kulikuwa na upungufu katika nyaraka, wanaopaswa kulaumiwa siyo wao, bali maofisa wa Mahakama waliopokea nyaraka za rufani na akatoa vielelezo vya kesi kadhaa ambazo ziliendelea mahakamani licha ya kuwapo dosari ndogo.

Kamala aliwaomba majaji kutupa hoja za wajibu rufani na kama ikifikia uamuzi wa kulipa gharama za pingamizi hilo, basi wajibu maombi wa pili ambao ni TBA ndiyo wanaopaswa kufanya hivyo.

Baada ya pande zote kuwasilisha hoja hizo, Jaji Mbarouk aliahirisha shauri hilo hadi hapo watakapomaliza kuzipitia.

No comments:

Post a Comment