Friday, June 5, 2015

MPINA KUCHUKUA FOMU YA URAIS JUMATAT.

MPINA KUCHUKUA FOMU YA URAIS  JUMATAT.






MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) anatarajiwa kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho Jumatatu ijayo.

Mpina ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM wiki hii katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika makao makuu ya jimbo la Kisesa, Mwandoya ameliambia gazeti hili jana, kwamba kama atafanikiwa kuingia Ikulu atabadili utendaji kazi serikalini na kuleta ahueni ya maisha kwa Watanzania wote.

Alisema katika mazingira haya haiwezekani nchi kuwa na vipaumbele, huku kukiwa hakuna fedha za kugharamia vipaumbele hivyo kutokana na msingi huo Serikali ya awamu ya tano atakayoiongoza kipaumbele chake cha kwanza na cha pili ni kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na usimamizi thabiti wa fedha za na rasilimali za umma.

Alitaja vipaumbele vingine kuwa vitakuwa elimu, afya, maji, miundombinu ya kiuchumi (Barabara, umeme, mawasiliano, viwanda, kilimo vitakuwa vinabadilika kila mwaka kulingana na mahitaji.

Alisema changamoto ambazo bado zinalikabili taifa letu ni nyingi na zinahitaji kiongozi ambaye atakuwa tayari kujitoa mhanga na bila uwoga wowote hata kama ni katika mazingira magumu namna gani na hata kupoteza maisha awe tayari.

"Hapa naweka wazi kuwa ninao uwezo mkubwa wa kumudu majukumu ya Amiri Jeshi Mkuu wa nchi kwamba siogopi kitu chochote na niko tayari kwa lolote lile katika mapambano ya kulitumikia taifa langu, kwani ni heri punda aumie lakini mzigo wa tajiri ufike," alisema Mpina.

Mpina alisema kutokana na uzoefu alioupata katika kipindi chake cha miaka 10 ya ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na miaka 5 ya ubunge wa Bunge la Afrika (PAP) pia Kamishna Vyuo Vikuu (TCU) kwa kipindi cha miaka 6 amegundua kuwa changamoto kubwa kuliko zote nchini na Afrika kwa ujumla ni udhaifu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na usimamizi duni wa fedha na rasilimali za umma.

Hivyo alisema Serikali yeyote haiwezi kuwa na kipaumbele kama haina fedha au kama ina matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma akitolea mfano hivi sasa hapa nchini matumizi ya kawaida ni makubwa kuliko mapato ya ndani, taarifa za wakaguzi CAG na PPRA zinathibitisha upotevu mkubwa wa fedha za umma kila mwaka, taarifa za TMAA na TEITI zinaonyesha utoroshaji mkubwa wa madini hapa nchini na ukwepaji wa kodi.

Mpina alisema sababu zilizomsukuma kugombea urais ni pamoja na kutoridhishwa na ukusanyaji wa mapato yasiyotosheleza mahitaji, imekuwa ikiripotiwa ukwepaji mkubwa wa kodi bandarini, mikataba mibovu ya madini na gesi, makampuni makubwa yanayokwepa kodi MNEs kwa mbinu mbalimbali ikiwemo Transfer Pricing, misamaha ya kodi isiyokuwa na tija, mfumo duni wa ukusanyaji wa maduhuli.

"Naamini kuwa endapo maeneo haya yatasimamiwa kikamilifu mapato ya serikali yataongezeka na kuwa kati ya mara 2 hadi mara 3 ya mapato yanayokusanywa hivi sasa. Nikipewa ridhaa nimejiandaa vizuri sana katika eneo hili kwa kuwekeza rasilimali fedha na watu, kuongeza ufanisi na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato ya serikali," alisema Mpina.

Pia fedha za Serikali zilizokopwa na kampuni binafsi na zimekaidi kulipa ambapo hadi leo kuna watu, kampuni zimekopa fedha za serikali zaidi ya shilingi trilioni 2 lakini wamekaidi kulipa madeni hayo pamoja na kwamba wanao uwezo wa kulipa fedha hizo na kusisitiza kuwa haiwezekani kuendelea kutoza kodi watu maskini halafu wengine wanajimilikisha fedha za umma kinyemela. Watu kama hawa katika serikali yake watakuwa wa kwanza kufilisiwa ili kurejesha fedha hizo za umma.


Mpina alisema utoroshaji wa fedha nje ya nchi Tanzania imekuwa ikiripotiwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo utoroshaji wa fedha nje ya nchi ni mkubwa ambapo ni zaidi ya asilimia 2 ya pato la Taifa hutoroshwa na kufichwa nje ya nchi na watu wachache. Mapato ambayo yangeweza kujenga miundombinu ya kiuchumi, kutoa huduma za kijamii na kuondoa umaskini badala yake zinakuwa ni fedha za wachache.

"Kwa waliozoea kufuja, kuiba, kufanya ubadhirifu ni bora waachie ngazi kabla sijaapishwa; na kwa wale walioficha fedha nje ya nchi ni bora wazirejeshe nchini mapema kabla sijaapishwa kwani wote hawa watakiona cha mtemakuni kwani hatari inayokuja kwao ni heri wasingezaliwa," alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa uliohudhuria mkutano huo.

Kuhusu uteuzi wa mawaziri, Mpina alisema mawaziri wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kushindwa kumudu majukumu yao wamekuwa wakifanya sherehe pindi wanapoteuliwa kushika nyadhifa hizo, swali la kujiuliza iweje mtu aliyekabidhiwa majukumu mazito sawa na kutolewa kafala afanye sherehe?

"Mfano, Waziri wa Afya anawezaje kufurahia uteuzi na kufanya sherehe huku akijua kuna Watanzania wanakufa kwa kukosa matibabu? Mawaziri nitakao wateua watakuwa wametolewa kafala kulitumikia Taifa lao na hivyo hakuna namna yeyote ambayo wanaweza kufanya sherehe mbali ya kwenda misikitini na makanisani kuombewa. Hakutakuwa na muda maalum kwa mawaziri kufukuzwa na kuondolewa kazini. Na kwamba uteuzi utakuwa wa usaili wa kuandika na mahojiano ili kuthibitisha uwezo wa nafasi anayoiomba," alisema Mpina.

No comments:

Post a Comment