Saturday, July 15, 2017

Vigogo Uwanja wa Ndege wa Mwl Nyerere kupigwa chini


Rorya maendeleo Blog · 14 hours ago

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema watafanya mabadiliko ya uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ili kuimarisha huduma katika uwanja huo.

Amesema ziara yake hiyo ya leo imetokana na malalamiko kutoka kwa abiria wanaolalamika kuhusu huduma za kiwango cha chini zinazotolewa hapo ikiwamo kutokuwa na mfumo mzuri wa hewa katika eneo la kutolea huduma za visa.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, Serikali haitavumilia watendaji wanaofanya kazi kwa mazoea na itahakikisha inatatua malalamiko mbalimbali yanayowasilishwa na watuamiaji wa uwanja huo.

“Tunahitaji kuimarisha uongozi katika uwanja huu, hili ni lango kubwa la kuingia na kutoka abiria wa kimataifa. Inabidi tuzifanyie kazi changamoto zote ili kila mmoja wetu afurahie huduma zetu,” anasema Profesa Mbarawa.

Amesema msongamano mkubwa hutokea kwenye eneo la huduma la kutolea visa, benki na mashine za ukaguzi. “Inabidi tukutane na idara zote zinazohusiana na kuangalia njia bora ya kukabiliana na changamoto hii,” amesema Profesa Mbarawa.

Hivi karibuni baadhi ya magazeti ya Uingereza yaliripoti habari inayohusiana na ujio wa mashabiki wa klabu ya Everton ambao walikaa zaidi ya saa tatu wakisubiri huduma ya visa.

Mbali na hilo, Profesa Mbarawa alisema kuhusu mikataba wataipitia upya mikataba minne kwa watoa huduma wa JNIA kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.

Miongoni mwa watoa huduma hao ni wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali na wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni yanayotoa huduma katika uwanja huo mkubwa nchini.

Bila kubainisha mikataba hiyo, Profesa Mbarawa amesema kuwa baadhi ya mikataba hiyo haina manufaa kwa uchumi wa nchi na hivyo ni lazima ipitiwe upya.

“Wiki ijayo nitaunda timu ya wataalamu ambao watanisaidia kupitia mikataba kabla sijatoa maamuzi, lakini nawahakikishia kila kitu kitawekwa wazi kama tulivyofanya kwenye mikataba mingine ukiwamo wa Kampuni ya Kimataifa inayoshughulikia makontena na mizigo Bandari ya Dar es Salaam (Ticts),’’ amesema.

Amesema kuwa Serikali itafanya mazungumzo na watoa huduma na kufanya maridhiano ya njia mpya zitakazoweka mbele maslahi ya Taifa.

Kaimu Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Salim Msangi amesema changomoto zinazojitokeza ni kwa sababu ya udogo wa jengo la uwanja huo na ambalo awali lililenga kuhudumia watu 1.5 milioni kwa mwaka, lakini mahitaji yameongezeka kufikia 2.5 milioni kwa mwaka.

“Tunajitahidi kukabiliana na changamoto hii kwa kufanya maboresho kadhaa, hali ya sasa si kama mwanzoni, mengi mazuri yamefanyika,”alisema Msangi.

1 comment:

  1. Wynn Slots for Android and iOS - Wooricasinos
    A kadangpintar free app for 출장안마 slot machines from WRI Holdings Limited that lets you play the popular games, casinosites.one such as wooricasinos.info free video 토토 slots, table games and live casino

    ReplyDelete