Saturday, June 4, 2016

SERIKALI YAJADILI RASIMU YA KISWAHILI YA MPANGO WA KUKABILIANA NA MAAFA

SERIKALI YAJADILI RASIMU YA KISWAHILI YA MPANGO WA KUKABILIANA NA MAAFA

Ofisi ya Waziri Mkuu imejadili na kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wilayani Kilosa Mei 30, 2016.
Rasimu hiyo imejikita katika kutoa miongozo ya uratibu katika kukabili dharura za aina zote za majanga yanapotokea katika ngazi zote za Kitaifa.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Maafa Wilayani Kilosa Mkurugenzi wa Tafiti na Mipango Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Naima Mrisho alieleza kuwa muongozo huo ni sehemu ya kuisaidia jamii katika kupata mbinu bora za kujiandaa, kukabili, na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea ili kuzisaidia jamii zetu. 
“Ni muhimu kuwa na mpango huo kwa kuzisaidia Halmashauri zetu katika kupambana na maafa yanayotukabili,”alisema Bi. Naima 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. John Henjewele alibainisha umuhimu wa Mpango huo ikiwa ni sehemu ya kuanzia na inayotoa muongozo mzuri unaosaidia katika Halmashauri yake katika kukabiliana na Maafa.
 “Tangu mpango kuanza kutumika Desemba 2013 Wilaya ya Kilosa imeweza kuwa na mbinu za kuyakabili maafa yanapotokea hususani yale ya mafuriko” Alisema Mkuu wa Wilaya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bw. Idd Mshili aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuona umuhimu wa kuitembelea Halmashauri yao kwa kuupitia Mpango na kuuboresha ili kusaidia kurahisisha uelewa kwa kua lugha ya Kiswahili inaeleweka kwa urahisi hususani ngazi ya chini na kwa wanavijiji wanaokumbana na maafa pindi yanapotokea.
 “Nichukue fursa hii kuwapongeza Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kuona umuhimu wa kuubadili mpango kutoka lugha ya Kingereza kuwa katika lugha ya Kiswahili ili kufikia makundi yote ya jamii kwa urahisi.”

AWALI: Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa ulianza kutumika mwaka 2013 ikiwa na lengo la kuziwezesha Halmashauri kujiandaa na kuyakabili maafa yanapotokea, Ofisi ya Waziri Mkuu imefanikiwa kufanya Tathimini kwa Halmashauri za baadhi ya Mikoa kwa kuangalia ubora wa mpango tangu uanze kutumika katika Mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Singida na Shinyanga kuanzia Mei 23 hadi 30, 2016.
Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Naima Mrisho akitoa neno la ufunguzi katika mkutano wa kujadili na kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Mei 30, 2016.
Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Bw. Christopher Chusi akichangia hoja wakati wa mkutano wa kujadili na kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa uliofanyika Mei 30, 2016 Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa kujadili na kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wakifuatilia mada ya Menejimenti ya Maafa kutoka kwa Mratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. John Kiriwai (hayupo pichani) katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Morogoro tarehe 30 Mei, 2016.
Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Naima Mrisho akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya maafa katika zoezi la ukakamavu katika kujiandaa na kukabili maafa wakati wa mkutano wa kujadili na kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa Wilayani Kilosa tarehe 30 Mei, 2016.
Mratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Fadhili Mtengela akiwasilisha mada ya kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa katika mkutano wa kujadili mpango huo uliofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro tarehe 30 Mei, 2016.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. John Henjewele (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano wa kujadili na kuboresha rasimu ya Kiswahili ya Mpango wa Halmashauri wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo Wilayani kilosa Morogoro tarehe 30 Mei, 2016.

No comments:

Post a Comment