Aliyesingizia utajiri kukwepa jela Marekani afungwa
Kijana aliyekwepa jela jimbo la Texas kwa kusingizia utajiri baada ya kuua watu akiendesha gari akiwa mlevi amefungwa jela.
Mwaka 2013, Ethan Couch aliua watu wanne baada ya kuwagonga akiwa na gari lake wakati huo akiwa na umri wa miaka 16.Lakini alifanikiwa kukwepa jela.
Mtaalamu wa matatizo ya kiakili wakati huo aliambia mahakama kwamba mvulana huyo alilelewa kwenye maisha ya utajiri kupindukia na kwamba hakufundishwa maadili mema na wazazi wake.
Alitaja hali hiyo kuwa “affluenza”, ingawa neno hilo halijatambuliwa na Chama cha Wataalam wa Mambo ya Kiakili Marekani.
Alitakiwa tu kudumisha tabia njema kwa miaka 10.
Lakini hakuweza na baada ya video kutolewa ikimuonesha akilewa na marafiki zake alitoroka nchi hiyo na kukimbilia Mexico mwezi Desemba.
Lakini baada ya muda alikamatwa na kurejeshwa Marekani.
Jumatano, Mahakama ilimwamuru atumikie vifungo vinne vya siku 180 jela ambavyo vitafuatana, kila kifungo kwa kila mtu aliyeua.
Kwa kuwa tayari ametimiza umri wa watu wazima, ana umri wa miaka 19 sasa, atafungwa katika jela ya watu wazima.
No comments:
Post a Comment