TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU MKATABA WA LUGUMI
Kumekuwa
na taarifa zinazoendelea kupotosha umma na baadhi ya vyombo vya Habari
kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokuwa ikitekeleza
majukumu yake tarehe 5 Aprili, 2016 ililitaka Jeshi la Polisi
kuwasilisha Mkataba ulioingiwa Kati ya Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi
Enterprises Ltd kuhusu mradi wa Utambuzi wa Alama za Vidole AFIS
(Automated Fingerprint Identification System).
Ofisi ya Bunge inapenda kutoa
ufafanuzi kuhusu jambo hili kwamba, taarifa hizo si za kweli na zina
lengo la kupotosha umma kutokana na kile kilicho amuliwa na kamati hiyo.
Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba tarehe 5 Aprili, 2016, kamati hiyo
ilikutana na kujadili Taarifa ya Ukaguzi wa hesabu zilizokaguliwa za
fungu 28, Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2014
ambapo kamati pamoja na mambo mengine ilibaini dosari katika utekelezaji
wa mkataba huo.
Kutokana na dosari hizo, kamati
iliomba Afisa Masuhuli ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa
mradi huo kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge ili kamati iweze kuchambua na
kujadili maelezo hayo kabla ya kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za
kuchukua. Kufuatia agizo hilo, kamati ilimwandikia pia Katibu wa Bunge
taarifa kuhusu agizo hilo tarehe 12 Aprili, 2016 ili kupatiwa maelezo
hayo kutoka kwa Afisa Masuhuli.
Aidha, Ofisi ya Bunge
ilimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 12
Aprili, 2016 kuwasiilsha Taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotokana na kikao hicho
cha tarehe 5 Aprili 2016 kabla ya tarehe 18 Aprili, 2018 kama
ilivyoshauriwa na kamati . Hivyo ni vyema Umma ukafahamu kuwa
kilichoombwa na Kamati ni Maelezo ya utekelezaji wa Mkataba huo na sio
Mkataba kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya Habari ambapo Ofisi
ya Bunge iliomba maelezo hayo yawasilishwe kabla ya tarehe 18 Aprili,
2016. Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM 15 Aprili, 2016.
No comments:
Post a Comment