Tuesday, July 5, 2016

WAKUU WAPYA WA WILAYA ZA MKOA WA MWANZA WAPEWA MAJUKUMU MARA BAADA YA KUAPISHWA.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, akizungumza katika hafla ya kuwaapisha wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Mwanza hii leo, Julai 04,2016 katika viunga vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Na BMG
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewataka wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha wanashirikiana na kamati za ulinzi na usalama pamoja na wananchi kwenye wilaya hizo ili kukomesha mauaji dhidi ya watu wenye
ulemavu wa ngozi na vikongwe yanayochangiwa na imani potofu za kishirikina.
Akizungumza baada ya kuwaapisha wakuu hao wa wilaya zote saba za mkoa wa Mwanza, Mongella amesema kwa muda mrefu mkoa wa Mwanza umekumbwa na matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino na vikongwe kutokana na imani za kishirikina
na kwamba wakati umefika kuhakikisha matukio hayo yanakwisha.
Amesema mkoa huo umejipanga vyema kuhakikisha matukio hayo yanakuwa historia kwa kuwa hakuna binadamu mwenye mamlaka ya kutoa uhai wa binadamu mwenzake kwa sababu yoyote ile.
Mkuu huyo wa mkoa amewapa mwezi mmoja wakuu hao wapya wa wilaya kumaliza tatizo la madawati pamoja na kuwachukulia hatua watumishi hewa 1,057 waliogundulika kwenye wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Mongella amewata wakuu hao wa Wilaya kuhakikisha kwamba matumizi ya dawa za kulevya katika wilaya zao yanakomeshwa ambapo amepiga marufuku matumizi ya shisha katika hoteli na klabu zote za muziki pamoja uchezaji wa “pool table” na unywaji wa pombe saa za kazi huku akitanabaisha kwamba atakaeshindwa kutekeleza maagizo hayo ni dhahiri shahiri kwamba atakuwa ameshindwa kusimamia majukumu yake.
 
Aidha Mongella amemtaka mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kuhakikisha kwamba hadi ifikapo Agosti mosi mwaka huu awe amewaondoa wafanyabiashara ndogondogo waliosambaa kwenye maeneo mbalimbali ya katikati ya jiji Mwanza.
 
Wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Mwanza walioapishwa, wamesema wamejipanga vyema kushirikiana na viongozi wengine pamoja na wananchi katika Wilaya zao ili kuhakikisha kwamba wanatekeleza vyema majukumu yao ikiwemo kuimarisha suala la ulinzi na usalama katika jamii.
Wakuu wapya wa Wilaya saba za Mkoa wa Mwanza walioapishwa hii leo ni Mary Onesmo Tesha wa Nyamagana, Estomin Francis Chang’a wa Ukerewe, Hadija Rashid Nyembo wa Magu,
Juma Samwel Sweda wa Misungwi, Emmanuel Enock Kipole wa Sengerema, Dkt.Leonard Moses Masale wa Ilemela na Mhandisi Mtemi Msafiri Simion wa Kwimba ambapo wote wamekabidhiwa vitendea kazi ikiwemo Katiba ya Tanzania pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/20.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mh.Emmanuel Enock Kipole (kulia), akiapa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella (kushoto).
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe.Estomin Francis Chang’a (kushoto) akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe.Hadija Rashid Nyembo, akiapa hii leo

No comments:

Post a Comment