Saturday, June 11, 2016

DARAJA LA MTO SIBITI KUKAMILIKA HIVI KARIBUNI; PROF. MBARAWA......

DARAJA LA MTO SIBITI KUKAMILIKA HIVI KARIBUNI; PROF. MBARAWA......

sib1Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo (wa kwanza kushoto), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto) kuhusu mradi wa ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti linalounganisha Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na Meatu mkoani Simiyu.
sib2Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo (wa kwanza kushoto) kuhusu usimamizi wa ujenzi wa Daraja la mto Sibiti.
sib3Muonekano wa moja ya nguzo inayoshikilia Daraja la Mto Sibiti linalounganisha Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na Meatu mkoani Simiyu.
sib4Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Bw. Christopher Ngubiagai (katikati), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) alipokagua ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti.
sib5Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) akikagua jengo la nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama linalojengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) mkoani Singida.
indexMuonekano wa juu wa Daraja la Msingi lenye urefu wa mita 75 linalounganisha Wilaya ya Mkalama na Iramba, lililopo mkoani Singida.
sib6Muonekano wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama inavyoonekana katika hatua za awali za ujenzi wake. Zaidi ya milioni 758 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo.
sib7Msimamizi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama (wa kwanza kulia), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), kuhusu hatua za ujenzi wa ofisi hizo mkoani Singida.
…………………………………………………………………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi Hainan International Limited anayejenga Daraja la mto Sibiti ambalo linaunganisha mkoa wa Singida na Simiyu kuendelea na ujenzi  wake.
Amesema hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi  wa daraja hilo na kuwahakikishia wananchi kuwa daraja hilo litakamilika katika kipindi cha hivi karibuni baada ya Serikali kuanza kumlipa mkandarasi huyo.
“Tumeanza kumlipa mkandarasi fedha hivyo tunawahakikishia kwamba katika kipindi kifupi kijacho litakamilika ili kufungua shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Wilaya ya Mkalama na Meatu” , amesema Prof. Mbarawa.
Aidha  Waziri huyo wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kutoza ushuru katika mto huo na kusisitiza kwamba tabia hiyo iachwe mara moja na atakayefanya hivyo anakiuka sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Wananchi wanatakiwa kupita hapa bila ya kulipa gharama yoyote katika mto huu, nimemuagiza Mkuu wa Wilaya na Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida waboreshe eneo la kuvukia ili wakati ujenzi unaendelea huduma za kuvuka ziendelee kama kawaida”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo amemhakikishia waziri kuwa ujenzi wa Daraja la mto sibiti pia utahusisha barabara ya maingilio yenye urefu wa kilomita 25 inayounganisha wilaya ya Mkalama na Meatu.
“Ujenzi wa barabara za maingilio unahusisha makalvati makubwa 10 na madogo 55 ili kuruhusu maji kupita kwa kasi na hivyo kudhibiti mafuriko”, amefafanua Eng. Kapongo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Bw. Christopher Ngubiagai amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa jitihada zake za kutaka kuunganisha wilaya yake na Meatu kwani kukamilika kwa daraja hilo kutaimarisha fursa za usafirishaji wa mazao na huduma za usafiri katika Wilaya hizo.
Zaidi ya shilingi bilioni 18.2 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Daraja la mto Sibiti lenye urefu wa mita 82 na upana wa mita 10.5 ambapo tayari Serikali imeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 4 mpaka sasa.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa nyumba za viongozi wa Wilaya ya Mkalama na jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwataka makandarasi wanaoendelea na  ujenzi wa miradi hiyo kuongeza kasi na  kutumia fedha wanazopata kujenga jengo moja moja kwa awamu ili kupunguza changamoto ya  makazi na ofisi Wilayani humo badala ya utaratibu wa sasa wa kujenga majengo yote kwa pamoja.
.”Msisubiri  mpate fedha zote  kwa nyumba zote, kamilisheni ujenzi wa nyumba moja moja kadri mnavyopata fedha ili kupunguza changamoto za makazi na ofisi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa yuko katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nne mkoani Singida ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, nyumba na  Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment