Saturday, June 4, 2016
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:Na Mwandishi Maalum, New York
Viongozi Wakuu wa Polisi kutoka nchi mia moja ambazo zinachangia polisi wao kuhudumu katika ulinzi wa amani na usalama kupitia Umoja wa Mataifa, wamekamilisha mkutano wao wa siku moja uliofanyika jana Ijumaa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Huu ni mkutano kwa kwanza wa aina yake kuwahi kufanyika, ambapo wakuu wa Polisi ( IGPs) wamekutana kwa wingi na kwa wakati mmoja tangu shughuli za Kipolisi zilipoingizwa katika Operesheni za Ulinzi wa Amani kupitia mwamvuli wa Umoja wa Mataifa.
Katika mkutano huu na ambao washiriki walijadiliana, kubadilishana uzoefu, na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kubadilishana za ulinzi na usalama katika nganzi ya Kimataifa, uliandaliwa na Kitengo cha Polisi cha Umoja wa Mataifa ( UNPOL), kitengo ambacho ni sehemu ya Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, na ulifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi ambayo kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikitoa Polisi wake kushiriki katika misheni za ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa, umeongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi na Mkuu wa Operesheni Maalum Bw. Daniel Nyambabe.
Akizungumza kwa njia ya video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema. “ Kutoka Kabul hadi Kishansa na kutoka Port-au Prince hadi Pristina, Polisi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu yao katika mazingira magumu, hatarishi na yenye changamoto nyingi. Lakini pamoja na changamoto hizo bado polisi hawa welevu na mashuja wameendelea kulinda jamii,wanaleta mabadiliko katika maeneo hayo na mengine mengi kwa kurejesha utawala wa sheria na kufungua njia za upatikanaji wa usalama na maendeleo endelevu
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UN, Jan Eliasson, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo , amewaambia viongozi hao wa Polisi kwamba, kutokana na changamoto nyingi na kubwa zinazohusu Amani na usalama wa Kimataifa, utekelezaji wa majukumu ya Polisi na kipolisi kuanzia wale wanaohudumu na kushiriki katika operesheni za Umoja wa Mataifa, na polisi wote duniani kote unatakiwa kubadilika na kuwa wa kisasa zaidi.
Maeneo ambayo Polisi wanatakiwa kubadilika katika utekelezaji wa majukumu yao ni pamoja na kuwa na zana na vifaa vya kisasa, uwezo mkubwa na weledi wa hali ya juu katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiitelejensia, uwezo mkubwa wa kukabiliana na kwa wakati na mitandao ya kihalifu ya kimataifa ukiwemo ugaidi.
“Kabla ya kumaliza hotuba yangu, ningepeda kusisitiza mambo kadhaa ya msingi ambayo ninaamini mtakubaliana nami. Maafisa wetu ( Polisi) wanatakiwa wawe tayari wakati wowote, wanatakiwa kuwa na vifaa na zana za kisasa za kazi , wanatakiwa wawe wanaopewa mafunzo ya hali ya juu, wanatakiwa wawe na uwezo wa kuwafundisha wengine, wanaopashwa kuwa na uwezo kuwa na teknolojia za kisasa, wanatakiwa wawe na fursa ya kupata taarifa za kiitelejensia na kuzifanyia kazi ipasavyo, uwezo wa kupata takwimu za uhalifu na vifaa vya kuzifanyia uchambuzi takwimu hizo” akasema Eliasson.
Katika kusisitiza hayo, pia ameongeza na kutilia mkazo nafasi na fursa ya Polisi wanawake ya kushiriki kwa wingi katika misheni za kulinda Amani. Na kuongeza pia kwamba, maafisa wa polisi wanatakiwa pia wawe ni viongozi wenye uzoefu mkubwa, na wanatakiwa kuwa tayari kusaidia katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kingono.
Viongozi wengine waliowazungumza wajumbe hao ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ( DPKO) Bw. Herve Ladsous pamoja na Bw. Atul Khare Mkuu wa DFS
Baadhi ya Mada zilizojadiliwa katika mkutano wa wakuu hao wa Polisi ni pamoja na changamoto za uhalifu wa kimataifa na Operesheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, hali ya sasa na ya baadaye kuhusu Polisi waohudumu katika Umoja wa Mataifa pengo, fursa nafasi na utaalamu wa Polisi katika Umoja wa Mataifa. Baadhi ya mada hizo zilitolewa na wataalam kutoka INTEPOL,
No comments:
Post a Comment