Tuesday, June 30, 2015

UKIWA HIVI, MAPENZI KWAKO YATA‘RANI’ DUNIA-2

UKIWA HIVI, MAPENZI KWAKO YATA‘RANI’ DUNIA-2

NIJumanne tena, bado naamini wapenzi wasomaji wangu wa safu hii mpo salama kabisa kimawazo na kivingine pia! Mada ya leo inatoka wiki iliyopita; ukiwa hivi, mapenzi kwako yata ‘rani’ dunia!
Wiki iliyopita nilizungumza mambo mengi kuhusu mada hii. Nilichambua kuhusu vifo vinavyotokana na mapenzi, ugomvi baina ya wanandugu kisa kikiwa mapenzi na kadhalika.
MSEMO WA MAPENZI KU ‘RANI’ DUNIA
Leo sasa, nataka kupita kwenye neno lenyewe la ukiwa hivi, mapenzi kwako yata ‘rani’ dunia. Huu msemo wa mapenzi yana ‘ran’ dunia upo kwenye wimbo wa Mbongo Fleva, Ali Kiba.
Yeye katika wimbo wake huo alikusudia kusema kuwa, kila kitu duniani kinamalizika na mapenzi. Vilio vya mapenzi vipo vingi sana. Watu wanalizwa na mapenzi. Wanasumbuka  na mapenzi. Kwa ujumla, sehemu kubwa ya maisha ya binadamu yanaendeshwa na mapenzi kila kukicha.
WAATHIRIKA WAKUBWA
Niliwahi kuzungumza na mwanasaikolojia mmoja wa hapa nchini, akasema kuwa, watu wanaosumbuliwa na mapenzi duniani kote ni wale wanaotoka kwenye kundi lenye ubongo wa kuhifadhi kumbukumbu mbaya.
Alisema: “Utakuta mtu amemfumania mke wake, anachukua uamuzi wa kuua. Tukio hilo kweli ni zito lakini si kwa kiasi cha kuutoa uhai wa mtu bali mfumaniaji anapokuwa na ubongo wa kuhifadhi kumbukumbu mbaya ndiyo hutokea hali hiyo.
“Huwa haikwepeki. Ni makundi ya watu, wenye ubongo wa kuhifadhi kumbukumbu mbaya wanapokerwa katika uhusiano hufanya lolote wakiamini wanajiweka sawa kiakili. Lakini sivyo,” alisema mwanasaikolojia huyo.
HATARI ZAIDI
Mtu huyo aliendelea kusema kuwa, watu wenye muundo huo akilini ndiyo wanaosumbuka kila kukicha. Na mabaya wanayoyafanya kwa wenza wao kuhusu mapenzi ni suluhisho la muda tu kwani baadaye ni majuto ndani ya nafsi.
“Watu wengi wapo kwenye magereza kutokana na uamuzi waliouchukua kuhusu wapenzi wao. Wengine wamevunja ndoa, kutokana na maamuzi hayohayo. Wengine wanaoa, wanaacha, wanaoa wanaacha. Wengine wanaolewa, wanaachika. Kisa ni huo muundo ndani ya akili zao.
“Hawa watu bwana, ingawa na wenyewe hawapendi kuwa hivyo lakini ukizaliwa na muundo huo wa kuhifadhi kumbukumbu mbaya, mapenzi yatasumbua sana kwako.”
HATA NJE YA MAPENZI
Mtaalam huyo aliendelea kusema kuwa, kundi hilo la watu hata nje ya mapenzi huwa hawawezi kuweka kando ya akili jambo baya wakafanya lingine jema.
“Naamini umewahi kusikia kama si wewe kukutokea. Mfano, mtu amekutumia meseji mbaya ya kukutukana. Unashindwa kula, unashindwa kufanya kazi, unashinda na masikitiko na kila mtu unamwambia ulichotendwa. Ukiona upo hivyo, mapenzi kwako yapo hivyohivyo.
KUNDI LENYE FURAHA
Mtaalam aliendelea kusema kuwa, wapo binadamu waliozaliwa na ubongo wa kutupa nje mabaya na kubaki na mazuri tu. Watu hawa, hata wakifumania, hawakurupuki kuua wala kutoa talaka.
“Wapo wanaume walishawafumania wake zao na hawakuchukua hatua yoyote ile. Baadaye wake wenyewe wakaondoka nyumbani kwa kuwa hawajaulizwa chochote na maisha yanaendelea.
“Kundi hili, huwa halisumbuliwi na mapenzi kwa vile lina ubongo wa kutupa kando matatizo. Watu hawa, hata kama ana mpenzi kampenda, wakiachana, anaweza kuumia kwa siku zisizozidi saba. Inakuwa kama jeraha, baada ya muda linapona.
“Watu hawa, hata kama wametumiwa meseji mbaya, wanaweza kusoma, wakimaliza wanafuta na hata kama wapo na marafiki zao hawawaambii na uchangamfu wao huendelea kuwa vilevile,” alisema mtaalam huyo.

JE, UNATAKA TIBA?
Tuonena wiki ijayo ambapo dawa ya kukwepa mapenzi kwako yasi ‘rani’ dunia itapatikana.

No comments:

Post a Comment