Wednesday, May 18, 2016

CUF NA CCM WAANZA KUBAGUANA KWENYE HUDUMA ZA KIJAMII VISIWANI ZANZIBAR, CCM WABAGULIWA KATIKA MADUKA NA MABASI

CUF NA CCM WAANZA KUBAGUANA KWENYE HUDUMA ZA
KIJAMII VISIWANI ZANZIBAR, CCM WABAGULIWA KATIKA
MADUKA NA MABASI
Pemba. Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid amefunga maduka matatu ya
rejareja na kusimamisha magari ya abiria kati ya Wete na Mtambwe kwa madai ya kutoa
huduma kwa misingi ya ubaguzi wa kisiasa.
Wafanyabiashara waliofungiwa ni Said Juma Seif, Titi Juma Othman wa Mtambwe na
Hamad Haji wa Mchangamdogo.
Alisema wafanyabiashara hao wamelalamikiwa na wafuasi wa CCM, wakiwatuhumu
kukataa kuwahudumia kutokana na itikadi zao za vyama.
Rashid alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kuwa wafanyabiashara hao
wanawabagua wanaCCM.
“Tumelazimika kuyafungia maduka hayo matatu baada ya Serikali ya Wilaya kujiridhisha
kwamba yanawabagua wanachama wa CCM,” alisema.
Akizungumzia hatua hiyo, Haji aliitaka Serikali kufanya uchunguzi kwanza kabla ya
kuchukua hatua akisema hahusiki na masuala ya kisiasa. Alisema hizo ni chokochoko za
wabaya wake.
Usafiri wasitishwa
Mkuu huyo wa wilaya, aliagiza kuzuiwa kwa magari yote ya kubeba abiria kwenye
Barabara ya Wete – Mtambwe kwa madai hayohayo ya kuwabagua wanaCCM.
Alisema mbali ya hatua hiyo, atawasiliana na wizara husika ili kuchukua hatua kwa
wahusika kwa kukiuka leseni.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama zuio hilo alilosema ni la muda usiojulikana
litayahusu magari ya Ruti B ambayo leo ndiyo yaliyotarajiwa kutoa huduma kwani
yaliyozuiwa jana kwenda Mtambwe, nyumbani kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif ni
ya Ruti A.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wete, Mmanga Juma Ali alisema katika
utekelezaji wa agizo hilo hakutakuwa na huruma: “…Hatutaishia hapo wanaofanya
ubaguzi huo watafikishwa mahakamani.”
Hata hivyo, baadhi wa wahuduma wa vyombo vya usafiri walisema si wao
wanaowashusha, bali ni wananchi na kwamba dereva na konda hawawezi kufanya hivyo
kwa kuwa lengo lao ni kutafuta faida.
Maalim Seif atema cheche
Wakati uongozi wa Wete ukichukua hatua hiyo, Maalim Seif ameendelea na ziara yake
visiwani hapa aliwataka Wazanzibari kuonyesha kuwa wanaikataa Serikali ya Dk Ali
Mohamed Shein.
Akizungumza na watendaji na viongozi wa CUF wa Wilaya ya Micheweni, Kaskazini
Pemba, Maalim Seif aliwataka kutomtegemea yeye pekee kufanya hivyo.
“Tukikazana, Serikali hii itaondoka, ikiwa mnangoja Maalim Seif au Marekani kuiondoa,
kwa sheria ya kimataifa haitawezekana kwani Marekani haiwezi kuingilia mambo ya ndani
ya Zanzibar,” alisema
Makamu huyo za zamani wa Rais wa Zanzibar, alijitoa kwenye uchaguzi wa marudio
uliofanyika Machi 20 ambao Dk Shein aliibuka kidedea.
Uchaguzi huo ulikuwa wa marudio baada ya ule wa Oktoba 25 kufutwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha siku ambayo alikuwa atangaze
matokeo yote.
Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na
vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF
kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali. “CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku
yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu
hawana safari ya kudumu,” alisema.
Aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo
kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa Serikali katika
utekelezaji wa majukumu yao.
“Mfano tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya
usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki
Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama
hicho.
CUF yajipanga kwenda ICC
Alisema kuna mwanasheria mzalendo ambaye ameanza kukusanya vielelezo mbalimbali
kabla ya kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC dhidi ya viongozi wenye
dhamana ya kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama wa raia.
Alisema tayari Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, wamepewa notisi ya kuarifiwa kufunguliwa
mashtaka ICC kutokana na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu uliofanyika
Zanzibar.
CCM yamjibu
Akizungumzia kauli za Maalim Seif, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alisema chama chake hakina muda wa kujibizana na CUF baada ya kumalizika kwa
uchaguzi na kwamba watakutana tena majukwaani na chama hicho kwenye uchaguzi wa
2020.
Baraza la wawakilishi kesho
Wakati hayo yakiendelea Baraza la Wawakilishi linatarajiwa kuanza kesho Chukwani, nje
kidogo ya mji wa Unguja.
Macho na masikio ya wananchi yataelekezwa katika Muswada wa Sheria ya Mafuta na
Gesi ambao unaweza kutegua kitendawili cha rasilimali hiyo kubaki ndani au nje ya
Muungano.
Katibu mpya wa Baraza hilo, Raya Issa Msellem alisema muswada huo utasomwa kwa
mara ya kwanza na wajumbe watapata nafasi ya kuuchangia.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment