Wednesday, May 18, 2016

MAMA MZAZI ATUMIWA PICHA YA VIDEO YA NGONO YA BINTI YAKE AKIBAKWA NA MWANAUME NYUMBA YA KULALA WAGENI

MAMA MZAZI ATUMIWA PICHA YA VIDEO YA NGONO YA
BINTI YAKE AKIBAKWA NA MWANAUME NYUMBA YA
KULALA WAGENI
Dar es Salaam. Mama mzazi wa binti mmoja mkazi wa Dakawa wilaya ya Mvomero
mkoani Morogoro hivi karibuni alipokea ujumbe wa picha ya video katika simu yake ya
mkononi na haraka aliifungua akiwa na shauku ya kuitazama.
Lahaula! Shauku yake ya kuitazama video hiyo aliyodhani ni sawa na nyingine za matukio
ambazo amekuwa akiziona zikisambazwa mitandaoni, iligeuka huzuni na fedheha kubwa
alipoona ikimwonyesha bintiye akidhalilishwa na wanaume huku akilalamika asirekodiwe
bila mafanikio.
Mama huyo alijizoazoa haraka na simu yake akatimua mbio hadi Polisi kuripoti tukio hilo
lililolenga kumdhalilisha binti yake na kuifedhehesha familia nzima. Hicho ndiyo kiini cha
vijana 11 wa Dakawa kukamatwa ili waisaidie Polisi kuhusu walioshiriki tukio hilo na
walioisambaza video hiyo kwa mama huyo na kwenye mitandao ya kijamii hasa
WhatsApp.
Katika video hiyo, wakati mwanamme mmoja akimdhalilisha huyo binti, mwingine
alikuwa akirekodi na baada ya kukamilisha tendo hilo lisilo na utu tena bila huruma
waliwatumia watu wengine katika eneo la Dakawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa aliliambia gazeti hili jana kuwa miongoni
mwa watu wa kwanza kuona video ile alikuwa mama wa msichana. “Alikimbia polisi
kwenda kutoa taarifa,”alisema Betty.
Baada ya kufika Polisi, Betty alisema polisi walimwambia mama huyo hawawezi
kuandika maelezo hadi mhusika ambaye ni binti yake afike kituoni. Walisema hivyo kwa
sababu ni mtu mzima hivyo anatakiwa kutoa maelezo mwenyewe. Saa chache baada ya
kuandikisha maelezo yake, polisi waliwakamata vijana wawili kwa tuhuma za kuhusika na
unyama huo. Betty alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi na leo watafikishwa
mahakamani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na kwamba hadi jana watuhumiwa
11 walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Matei alisema tisa kati yao wanaoshikiliwa ni kwa kosa la kusambaza picha za
utupu huku vijana wawili ambao ni Zuberi Thabiti (30) na Iddy Adamu (32) ni kwa kosa
la kufanya mapenzi na msichana huyo kwa nguvu huku wakirekodi.
Ilivyokuwa
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao walifanya kitendo
hicho Aprili 28 mwaka huu majira ya saa 1.00 usiku katika nyumba ya kulala wageni
yenye jina la ‘Titii’ iliyopo Dakawa.
Kamanda Matei alisema kuwa binti huyo aliitwa kwenye nyumba hiyo ya wageni na
Thabiti ambaye ni mkazi wa Mbarali wilaya ya Mbeya ambaye alikuwa na uhusiano naye
kimapenzi. Baada ya kuingia chumbani alimkuta pia Adamu mkazi wa Makambako,
Njombe ambao walimlazimisha kufanya mapenzi huku mmoja akimrekodi picha za video
na baadaye kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Wanaoshikiliwa kwa kosa la kusambaza picha za utupu ni Rajabu Salehe (26), Said
Athman (26), Musi Ngai (36), Said Muhammed (24), John Peter (24), Hassan
Ramadhan (27), Ramadhan Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjone (30).
Wote ni wakazi wa Dakawa, Morogoro na wamevunja Sheria ya Makosa ya Mitandao,
kifungu namba 14, kifungu kidogo (1) (a)
Kamanda Matei alisema wakati wa tukio hilo watuhumiwa hao walimtisha binti huyo kwa
kisu ili asipige kelele wakati akidhalilishwa na walimtaka asitoe siri hiyo vinginevyo
watamuua.
Kamanda alisema wawili hao ni marafiki wa msichana huyo na kwamba Thabiti ambaye
ni mpenzi wa sasa wa msichana huyo alipanga na Adamu ambaye ni mpenzi wake wa
zamani kumkomesha.
Alisema Thabiti alimwambia mpenzi wake wakutane hotelini. Msichana alipofika
aliwakuta chumbani huku Adamu akiwa ameshika kisu na kamera. “Wakamlazimisha
afanye vile na kumtishia kumuua kama angekataa,”alisema Matei.
Hata hivyo, Betty alisimulia kisa hicho na kusema watuhumiwa hao walifanya unyama
huo kwa sababu ya usaliti wa mapenzi. Alisema msichana alidaiwa kujihusisha kimapenzi
na dereva wa mpenzi wake.
Kwa mujibu wa Betty, baada ya mpenzi wake kugundua alipanga njama ili kuwakomoa
wote wawili. Alisema mpenzi wake alimwambia wakutane hotelini na alipofika alimkuta
Zuberi pamoja na dereva wa mchumba wake hotelini.
“Akawambia wafanye kile kitendo huku akirekodi video,”alisema Betty. “Nia yake ilikuwa
kuwakomoa…kwa nini atembee na dereva wake,”alisema Betty na kwamba baada ya
hapo picha hizo zilianza kusambaa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hali hiyo inaonyesha jinsi maadili yanavyozidi
kuporomoka katika jamii.
“Hilo siyo kosa la kisheria peke yake ni udhalilishaji mkubwa,”alisema.
Dk Hellen alisema licha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu kukemea suala hilo ni vyema jamii ikazingatia suala la maadili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Edda
Sanga alisema vyama vya kutetea haki za wanawake vinafanya mkutano wa pamoja
kujadili suala hilo.
“Leo (jana) tumekutana ili tujadili na kuja na tamko la pamoja,”alisema Sanga na
kuongeza kwamba jambo hilo halivumiliki kwa sababu vitendo kama hivyo vinaendelea
kujitokeza mara kwa mara.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment