Tuesday, May 17, 2016

Serikali yakanusha kuhusu Mashine za kukoboa mpunga na mahindi Halmashauri ya Kahama kufanya kazi saa 24.

Serikali yakanusha kuhusu Mashine za kukoboa mpunga na mahindi Halmashauri ya Kahama kufanya kazi saa 24.

DSCN3456Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
 
SERIKALI imekanusha madai kuhusu mashine za kukoboa mpunga na mahindi katika Halmashauri ya Mji wa Kahama kufanya kazi wakati wa usiku au saa 24.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Salome Makamba ambaye alitaka kujua utayari wa Serikali kuviruhusu Viwanda Wilayani Kahama kufanya kazi masaa 24 ili kufidia uzalishaji uliokuwa haufanyiki kipindi umeme unapokatika wakati wa mchana.
Akijibu swali Mhe. Jafo amesema kuwa, Serikali haijatoa zuio lolote kwa Halmashauri hiyo kwa mashine za kukoboa nafaka kufanya kazi nyakati za usiku ambapo amefafanua kuwa changamoto iliyopo ni kwamba viwanda hivyo vinatumia umeme wa jenereta ambao umekuwa hautoshelezi kuendesha mashine wakati wote hali iliyopelekea kuwepo kwa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.
“Halamshauri imewasiliana na Meneja wa Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (TANESCO) Kahama na yatari tatizo hilo limeanza kushughulikiwa ili kupata umeme wa uhakika kutoka Gridi ya Taifa ambapo tayari kituo cha usamabazaji kimeanza kujengwa Kahama”, alisema Mhe. Jafo.
Ameongeza kuwa, Halmashauri wilayani hapo inahamasisha Wawekezaji wa viwanda vidogo vikiwemo vya kukoboa mpunga, mahindi pamoja na mazao mengine ili kupanua wigo wa mapato kupitia ushuru wa huduma (Service Levy) na ajira kwa vijana.
“Hakuna sababu yoyote kwa Serikali kuzuia wawekezaji katika viwanda vidogo na vikubwa, azma ya serikali ni kupanua uwekezaji wa viwanda kadri iwezekanavyo kwa kuzingatia fursa zilizopo, tunachofanya ni kuboresha mazingira yatakayosaidia uwekezaji huo kufanyika kwa faida ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba umeme wa uhakika unakuwepo.

No comments:

Post a Comment