Sunday, June 12, 2016

VIONGOZI WA MFUKO WA MAENDELEO YA PAMBA WAUMBULIWA

WATANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUPIGA VITA MATUKIO YA MAUAJI

indexWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania, viongozi wa dini zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita matukio maovu ya mauaji yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema anatarajia hali ya amani, usalama na utulivu inaendelea kuwepo nchini, hivyo wananchi hawana budi kushirikiana na kushikamana na Serikali katika kuhakikisha matendo maovu hayatokei katika maeneo yao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati  alipowasili mkoani Geita kwa ajili ya kuhudhuria ibada ya kuwekwa wakfu Padre Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.
“Mfano tukio la Mwanza watu wanavaa kanzu na wanaingia msikitini na kukuta wenzao wanafanya ibada kisha wakawachinja, hii haiwezekani kwa binadamu wa kawaida hivyo tushirikiane katika kupiga vita matendo haya,” alisisitiza.
Hivi karibuni jumla ya watu 15 waliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga katika mikoa ya Mwanza,Tanga, Dar es Salaam  na Mara.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga amesema vitendo vya watu kuuawa kwa kukatwa mapanga vimepungua baada ya kuanzisha kampeni maalumu ya kukemea mauaji hayo.
Alisema katika kampeni hiyo wameamua kuwatumia walimu, viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wauguzi ambao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina na badala yake wajikite katika masuala ya maendeleo.

VIONGOZI WA MFUKO WA MAENDELEO YA PAMBA WAUMBULIWA

DC MARWAMKUU wa wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Ibrahimu Marwa amesema viongozi wa Mfuko wa Wakfu wa maendeleo ya zao la pamba uliwapelekea wakulima pembejeo feki na kuwasababishia hasara.
Amesema hatua hiyo inatokana wafanyabiashara na viongozi wa mfuko huo kuwa na maslahi binafsi katika zao la pamba hivyo kushindwa kuwasaidia wakulima ipasavyo.
Marwa aliyasema hayo jana (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga alipokuwa akisoma taarifa ya Mkoa huo kwa Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa alipowasili Mkoani hapo.
Alisema mara baada ya wakulima kupelekewa pembejeo hizo na kubaini kuwa na kasoro walizipeleka katika Kiituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukirigulu kilichoko mkoani Mwanza ambacho nacho kilithibitisha kuwepo kwa kasoro.
Kwa upande wake Waziri Mkuu amewataka Maofisa Kilimo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na kuwasaidia wakulima wa pamba ili waweze kupata tija.
Ametaka Maofisa Kilimo na viongozi wa maeneo yanayolima pamba kujipanga upya baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka kwa kuanza mikakati ya kufanya utafiti wa mbegu bora za pamba na kuziandaa za kutosheleza wakulima wote.
Alisema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Maofisa Kilimo ambao wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa sababu mashamba ya wakulima yanashindwa kuendelea kwa kuwa hakuna mtu anayewafuatilia.
“Mwakani muanze kufanya utafiti kuanzia hatua za awali na kituo cha Ukirigulu kipewe kazi ya kusimamia zao hili na kiwe na shamba darasa kwa ajili ya kufundishia wakulima. Lengo ni kuhakikisha zao hili linakuwa na tija,” alisema.
Hata hivyo Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri za Wilaya zinazolima pamba zifanye utafiti ili kujua sababu zilizosababisha wakulima kupunguza ari ya kulima zao hilo.  
Pia amewataka waachane na mfumo wa kilimo cha mkataba kwa sababu hauna tija kwa mkulima kwani hautengenezi ushindani na badala yake wajifunze mfumo unaotumika katika uuzaji wa zao la korosho.

No comments:

Post a Comment