Tuesday, July 12, 2016

RAIS MAGUFULI APUUZWA MCHANA KWEUPE,NA DC NA MKUREGENZI WAKE,SOMA HAPO KUJUA




 John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MARRY Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mwanza na Housian Kusiga, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la hilo wamekiuka agizo la Rais John Magufuli la kufanyika kwa sherehe za kupongezana pindi mtumishi wa umma anapoteuliwa kushika nyadhifa, anaandika Moses Mseti.

Machi mwaka huu, Rais Magufuli akiwaapisha wakuu wa mikoa jijini Dar e Salaam, aliwataka kutosherehekea kuteuliwa kwao na kwamba, wafanye hivyo siku wakitimuliwa.

Rais Magufuli pia aliwaagiza wakuu hao wa mikoa kuwekeza nguvu zao katika kuondoa tatizo sugu la madawati kwenye shule za umma, agizo ambalo muda wake ulikamilika Juni 30 mwaka huu huku Mkoa wa Mwanza ukikwama kufikia malengo hayo.

Sherehe za kumkaribisha mkuu huyo wa Wilaya ya Nyamagana na kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Baraka Konisaga maarufu mtumishi wa Mungu, ziliandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza chini ya kaimu mkurugenzi huyo.

Sherehe hizo zilizofanyika katika Hoteli ya New Mwanza ambapo zaidi ya watu 100 wakiwemo watumishi wa Jiji la Mwanza wakihudhuria ambapo kiasi cha zaidi ya Sh. 30 milioni zikitajwa kutumika.

Sherehe hizo zilizoanza saa 12 jioni hadi saa 4 usiku, waandishi wa  vyombo mbalimbali vya habari  walitimliwa na kutakiwa kutoripoti habari hii.

Awali, waandishi walialikwa na baadhi ya viongozi hao wakiwemo wakuu wa wilaya kwa ajili ya kuripoti lakini baadaye ikaibuliwa hoja ya kwamba, inaweza kusababisha tatizo hasa kutokana na kutokamilika kwa fedha za ununuzi wa madawati.
Hosian Kusiga, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo alipotafutwa kuzungumzia suala hilo amesema kuwa, fedha zilizotumika kuandaa sherehe hiyo hazikutoka katika mfuko wa serikali na kwamba, walichangishana baadhi ya watumishi wa jiji na taasisi mbalimbali.
“Wewe kama ulivyoona mwenye katika sherehe hiyo yalikuwepo makundi mbalimbali, ikiwemo Mwauwasa (Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira) mkoani Mwanza na sio fedha kutoka Jiji,” amesema Kusiga ambaye pia ni Ofisa Mipango wa Jiji.
Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana akizungumzia suala hilo amesema kuwa, fedha zilizotumika katika sherehe hiyo sio fedha za serikali.
“Pesa zilizotumika sio za serikali, unaniuliza fedha zilizochangwa eti kwanini hazijapelekwa kwenye madawati, mimi ningewakataza wasifanye sherehe, hivi wewe vipii… mbona sikuelewi,” amesema.

No comments:

Post a Comment