Monday, July 11, 2016

VYAMA VYA MUZIKI NCHINI VYASHAURIWA KUFUATA TARATIBU KABLA YA KUKUTANA NA VIONGOZI WA SERIKALI.

VYAMA VYA MUZIKI NCHINI VYASHAURIWA KUFUATA TARATIBU KABLA YA KUKUTANA NA VIONGOZI WA SERIKALI.

IMG-20140718-WA0038Na Benedict Liwenga, WHUSM.
————–
Vyama vya Muziki nchini vimetakiwa kufuata, Sheria, Taratibu na Kanuni pindi Wanachama wake wanapopanga kukutana na baadhi ya Viongozi wa Serikali.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa masuala ya Lugha, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Husna Kitogo ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Sanaa Wizarani hapo wakati alipokutana na Mashirikisho ya Vyama vya Muziki nchini.
Bi. Kitogo amesema kwamba kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Wasanii Wanachama na wasio wanachama kukutana na baadhi ya Viongozi wa juu wa Serikali pasipo Wizara kupewa taarifa jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na kuwataka kufuata Sheria na utaratibu mzuri wa kufanya mawasiliano na Wizara kabla ya kufanya hivyo.
‘’Msifanye kazi kwa mazoea, kwani mnapojiamulia kukutana na Viongozi wa Serikali pasipo kuijulisha Wizara mnakosea kwani Serikali inafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, na baadhi ya watu wanaofanya hivi pindi wanapokwama utaona wanarudi kwetu, jitahidini kujenga utaratibu hata wakutuletea nakala ya barua ili sisi tuweze kuwasaidia katika kukutana nao hao viongozi’’, alisema Kitogo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Madj wa Muziki Tanzania (TDMA) Bw. Asanterabbi Mtaki ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na Usajili wa Vikundi, vibali vya kufanyia kazi, masuala ya Haki Miliki (Copy rights), kodi za bidhaa za muziki pamoja na usimamizi wa mapato ya kazi za sanaa.
Amesema kwamba, baadhi ya Wanamuziki nchini wamekuwa hawatambui umuhimu wa kujiunga na Mashirikisho pamoja na vyama mbalimbali hali ambayo inadidimiza tasnia ya sanaa kwani kunapelekea kukosekana kwa ushirikiano katika kujenga taifa, kutokana na hali hiyo ameishauri Serikali kuwasimamia wanamuziki ambao bado hawajajiandikisha katika Vyama kufanya hivyo ili kuleta nguvu ya pamoja katika kupigania haki za Wasanii nchini.
‘’Naishauri Serikali kuliangalia suala hili la baadhi ya wasanii kutojiandikisha katika vyama na ndiyo hawa wasanii ambao wamekuwa wakikutana kimya kimya na Viongozi wa juu wa Serikali na baadhi ya yao hawako katika Mashirikisho ama Vyama vya Wasanii, hii ni changamoto kwetu sisi, tunaiomba Serikali itusaidie kuwapa elimu hawa watu ili wajue faida na umuhimu wa kujiunga na vyama’’, alisema Mtaki.
Naye Mwanamuziki Mkongwe na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) maarufu kama Bw. Juma Ubao ameiomba Serikali kuendelea kuzisimamia haki za Wasanii nchini hususani katika suala zima la Haki Miliki zao kwani ndiyo kilio chao cha muda mrefu.
‘’Ushirikiano baina ya Serikali na Vyama vya Wanamuziki nchini uzidi kudumu na hivyo tunaiomba Serikali itusaidie katika kupunguza kodi kwa bidhaa za muziki kwani kwa kufanya hivyo kutatuondolea adha ya kununua vifaa visivyo na ubora, kwani tunajikuta tunanunua vifaa hivyo kutokana na kushindwa kununua vyenye ubora zaidi vitokavyo nje kutokana na kodi yake kuwa kubwa.
Katika kikao hicho, baadhi ya mapendekezo waliyokubaliana ni pamoja na suala la usajili unaofanywa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kutambua uwepo wa Shirikisho la Vyama vya Muziki Tanzania, uboreshaji wa Sheria pamoja na Sera ya Sanaa, Wasanii kulipwa kutokana na kazi zao zitumikazo katika baadhi ya Vyombo vya habari nchini pamoja na Wanafani wote nchini kupitia katika Vyama husika.
Kikao hicho kilichoitishwa na Wizara kiliwakutanisha Wajumbe mbalimbali toka Chama cha Madj wa Muziki Tanzania (TDMA), Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), Chama cha Taarab Tanzania (TTA), Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya (TUMA), Chama cha Muziki wa Injili Tanzania pamoja na Vyama venginevyo lengo likiwa ni kutambua baadhi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili vyama hivyo.

No comments:

Post a Comment