Saturday, June 11, 2016

SERIKALI YATANGAZA UTARATIBU MPYA MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA, PIA YAFAFANUA FEDHA ZILIZOOKOLEWA WATUMISHI HEWA.

SERIKALI YATANGAZA UTARATIBU MPYA MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA, PIA YAFAFANUA FEDHA ZILIZOOKOLEWA WATUMISHI HEWA.

indexWaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2016.
………………………………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
SERIKALI imetangaza utaratibu mpya utakaofuatwa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2016 ambapo imewaagiza Watendaji Wakuu katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali kutenga siku moja ya kukutana na watumishi katika sehemu zao za kazi kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, imewaagiza watendaji hao kutenga siku nyingine moja kwa ajili ya kukutana na wananchi, kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero zao zinazohusiana na huduma zinazotolewa na Taasisi zao.
Akitangaza utaratibu huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeamua kubadili mfumo wa maadhimisho hayo kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi na watumishi wa umma katika maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa wakati wa maadhimisho hayo Watendaji hao watatakiwa kukutana wananchi na kusikiliza kero zinazohusiana na huduma zinazotolewa na taasisi zao pia kukutana na watumishi wa umma katika sehemu zao za kazi kusikiliza kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili zikiwemo za upandishwaji wa vyeo, madai mbalimbali na taratibu mbalimbali kuhusu utumishi wa umma.
Amesema kuwa baada ya maadhimisho hayo kila Wizara, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi ya Umma itapaswa kuandaa taarifa jinsi ilivyotekeleza maagizo yaliyotolewa kwa kuiwasilisha Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kabla ya Juni 30, 2016.
Ameeleza kuwa Tanzania inaungana na mataifa mengine ya Bara la Afrika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika  chini ya Kaulimbiu isemayo Uongozi wa Umma kwa Ukuaji Jumuishi:kuelekea katika Afrika tunayoitaka.
Mhe. Angellah amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatajikita katika kuangalia mchango wa Utumishi wa Umma katika ukuaji wa uchumi Barani Afrika, mchango wa Utumishi wa Umma katika kuiwezesha Ajenda ya Afrika ya 20163 ambayo inaweka mkazo katika maendeleo ya Afrika na Haki za Wanawake.
Amesisitiza kuwa malengo na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ni kufikia uchumi wa viwanda uliofungamanishwa na maendeleo ya watu, Tanzania ikiwa imejiwekea malengo ya kupiga hatua katika ukuaji wa uchumi kupitia maendeleo ya viwanda.
Amesema ili kufikia azma hiyo Serikali kupitia Utumishi wa Umma ina wajibu wa kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi huku watumishi wa umma wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi, kutoa huduma kwa wananchi wote kwa wakati pasipo urasimu wala ukiritimba pia kuepuka vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

No comments:

Post a Comment