Tuesday, July 14, 2015

MAGAZETINI JULY14…Idadi ya vijana wenye Ukimwi, NEC yatangaza majimbo mapya na Mgombea adai milioni1 yake.

MAGAZETINI JULY14…Idadi ya vijana wenye Ukimwi, NEC yatangaza majimbo mapya na Mgombea adai milioni1 yake.

By Royamaendeleo.
NICEEMWANANCHI
Wakati vijana 40,000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wakibainika kuambukizwa ugonjwa Ukimwi jijini Dar es salaam, viongozi, wabunge na wafanyabiashara wametajwa kuwa vinara wa kusambaza ugonjwa huo.
Mratibu wa tume ya vijana ya kupamba na ugonjwa huo Tacaids Grace Kessy alisema vijana wasipobadili tabia wataendelea kuwepo hatarini.
Alisema katika taarifa zilizokusanywa za mwaka 2011/12 zilibainika kuwa kati ya vijana waliopima 40,000 walikuwa na ugonjwa huo , wakifatiwa na vijana 10,000 kutoka Mikoa ya Shinyanga, Kagera na Mbeya.
“Tatizo la maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi ni kubwa hasa kwa vijana hivyo ni muhimu kuwa na mikakati ya pamoja na kudhibiti hali hiyo”.
Mbunge wa jimbo la Arumeru Godless Lema alisema suala la kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo ni la kimaadili kwani sasa wanaoharibu watoto ni watu wenye uwezo wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, wabunge na viongozi mbalimbali kutyokana na umaskini wa vijana.
“Taifa lina tatizo kubwa la kimaadili, hivi sasa wazazi wameacha jukumu la kulea watoto na kuwaachia wafanyakazi wa ndani, wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na simu kufanya mambo makubwa mabayo si muda wao kufanya”.
MWANANCHI
Siku moja baada ya CCM kumpitisha Dk John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais, Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema chama hicho kimefanya uamuzi sahihi kwa kuwa waziri huyo wa ujenzi ni mchapakazi na hakutumia fedha kuipata nafasi hiyo.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati mgombea huyo akipokewa Dar es Salaam leo akiambatana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kuwatambulisha kwa wananchi utakaofanyika Mbagala Zakhiem.
Juzi, Magufuli alipitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM kwa kura 2,104 na kuwashinda Balozi Amina Salum Ali aliyepata kura 253 na Dk Asha Rose Migiro kura 59.
Jaji Warioba ambaye awali aliwakemea baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo ndani ya CCM kwa kukiuka kanuni, alisema mchakato huo ulikuwa umeingiliwa na kila aina ya michezo michafu ya rushwa na uvunjaji wa kanuni na taratibu, lakini alielezea kufurahishwa kwake baada ya mambo hayo kuwekwa kando wakati wa kupitisha mgombea.
“Nilikuwa na wasiwasi kama vikao vya chama vitatenda haki katika kupitisha mgombea kutokana na baadhi ya viongozi kujipambanua wazi kwa wagombea wanaowaunga mkono,” alisema Jaji Warioba jana.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Jaji Warioba alieleza kasoro mbili zilizoibuka katika mchakato huo, moja ikiwa ni baadhi ya wagombea kueleza sera zao, wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi na pili, kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye ngazi ya uamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais.
Mbali na Warioba ambaye ni Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jambo hilo pia lilikemewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na wajumbe wa iliyokuwa tume hiyo katika kongamano lililoandaliwa na taasisi hiyo lililofanyika Julai 9, Dar es Salaam.
“Nimefarijika jinsi hali ilivyokuwa nadhani kwa mara ya kwanza fedha haikushinda,” alisema Jaji Warioba huku akisisitiza kuwa ni jambo baya kumpata kiongozi kwa nguvu ya fedha.
Alisema pamoja na kuwa fedha haikushinda, lakini ukweli ulio wazi ni kwamba wapo waliotumia fedha nyingi katika mchakato huo kwa lengo na kupitishwa kugombea urais.
“Sote tunajua kuwa Magufuli hakutumia fedha wala viongozi wakati akisaka wadhamini mikoani. Yeye alikwenda kwa wanachama na kutafuta wadhamini kimyakimya. Ni mtu sahihi. Alifanya kazi hiyo bila kutumia fedha,” alisema.
Alisema makundi yalikuwa yanatishia kuvunja umoja ndani ya chama hicho na kwa sasa ana imani na Dk Magufuli kuwa atawaunganisha wanaCCM kutokana na rekodi zake za utendaji kazi.
Alisema mbunge huyo wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi ni chaguo zuri kwa kuwa si mtu wa makundi na atakuwa na kazi nyepesi kuwaunganisha wanachama wa CCM.
MWANANCHI
Ni fainali leo pale vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vitakapompitisha mgombea wake urais atakayepambanishwa na yule wa CCM, Dk John Magufuli aliyepitishwa Dodoma juzi.
Fainali hiyo ndani ya Ukawa inatarajiwa kuhitimisha mvutano uliokuwapo baina ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye tayari amechukua fomu kuwania urais ndani ya umoja huo na mgombea anayetajwa na Chadema, Dk Willibrod Slaa. Mwingine aliyechukua fomu katika umoja huo ni Dk Kahangwa wa NCCR-Mageuzi.
Yeyote atakayeibuka katika mpambano huo na kutangazwa rasmi leo, atakwenda kushindana katika fainali nyingine dhidi ya mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Wanaopewa nafasi ni Dk Slaa aliyegombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kutoa upinzani mkali kwa Rais Jakaya Kikwete na Profesa Lipumba ambaye amejaribu bahati yake mara nne, 1995, 2000, 2005 na 2010 na sasa akitaka kujaribu kwa mara ya tano.
Wawili hao wameibua mvutano ndani ya vikao vya Ukawa na wajumbe wengi walikuwa wanaipa nafasi Chadema kusimamisha mgombea urais wa Muungano baada ya CUF kupewa nafasi ya kusimamisha mgombea urais Zanzibar.
Jumamosi iliyopita, kamati ya viongozi ya wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo, NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF ilikutana asubuhi na jioni kutoa tathmini ya walichokubaliana mbele ya wabunge wote na viongozi wa vyama hivyo kuwa mgombea wao atatangazwa leo.
Akitangaza uamuzi huo, Profesa Lipumba aliwaeleza waandishi wa habari kwamba kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama hivyo ila hayawezi kuleta matatizo, kwamba wapo pamoja na watatoa majibu ya pamoja.
Wiki mbili sasa, viongozi wa Ukawa wamekuwa na mjadala mzito kuhusu kugawana majimbo ambayo mpaka sasa wamekubaliana kwa asilimia 97 na kushindwa kuafikiana kuhusu urais kutokana na mvutano kati ya Chadema na CUF.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliliambia gazeti hili jana kuwa kikao cha leo kipo palepale na kusisitiza kuwa bado wanaendelea na mazungumzo.
“Watanzania wasubiri kesho (leo) tutawaleleza kilichoafikiwa. Unajua kwenye siasa saa 24 zinaweza kuwa miezi 24. Siasa ni siasa na kila kitu kinawezekana katika siasa,” alisema.
“Kama tumeshawaambia watu kesho (leo) ndiyo tutazungumza, itabaki kuwa hivyo. Leo (jana) hatuwezi kusema chochote. Unajua tuna vitu vingi tunaendelea kuvikamilisha kwa sasa, tuvute subira na kila kitu tutakiweka wazi kesho,” Mbowe.
Leo kabla ya kumtaja mgombea wa urais, viongozi wa Ukawa watakuwa na kikao cha majadiliano ambacho kitatoa mwelekeo wa umoja huo huku taarifa kutoka ndani ya vyama hivyo zikieleza kuwa mwafaka bado haujapatikana.
JAMBOLEO
Kada wa Chama cha Mapinduzi Dk.Musa Muzamili Kalokola aliyekuwa akiomba ridhaa ya kuomba kugombea nafasi ya Urais ametoa kituko baada ya jana kutaka arudishiwe fedha yake milioni 1 aliyochukulia fomu.
Kalokola ambaye alikuwa miongoni mwa makada 42 wa CCM waliochukua fomu za kuomba kuwnaia Urais, amesema hakubaliani na mchakato wa kumapata mgombea wa CCM ulivyokwenda, kwani wagombea hawakupewa fursa ya kujieleza , hivyo anataka arudishiwe fedha zake.
Alisema utaratibu ulikuwa wa hivyo na kwamba inashangaza wagombea kutolewa fursa ya kujieleza mbele ya wajumbe.
“Sikubaliani na mchakato ulivyokwenda hata kidogom hivyo nitaandika demand notisi wanirudishie fedha zangu walizochukua na nilizotumia kuzunguka kutafuta wadhamini,”Kalokola.
Alipoulizwa kama atamuunga mgombea aliyepitishwa na CCM kuwania nafasi ya Urais alisema kuwa kila mtu atabeba msalaba wake.
NIPASHE
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi ambao idadi yao haijulikana wakiwa na silaha za moto wamevamia Kituo cha Polisi Stakishari jijini Dar es Salaam na kuua watu saba, wakiwamo askari wanne kisha kupora silaha kadhaa na kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo inadaiwa kuwa majambazi hayo yaliyopora bunduki aina ya SMG 15 na Idadi hiyo imefanya idadi ya polisi waliouawa kwa kuvamiwa katika vituo vya polisi nchini kufikia 11 na silaha 53 katika kipindi cha miezi 13 kuanzia Juni 2014 hadi sasa.
Mkuu wa Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu, akizungumza jana katika kituo hicho kilichopo Kata ya Ukonga Wilaya ya Ilala,  alisema majambazi hao walikivamia usiku wa kuamkia juzi saa 5:20 .
 Mangu alisema katika tukio hilo, askari wanne wameuawa, raia wawili na mtu mmoja anayesadikiwa kuwa ni mmoja wa majambazi hao.
 Aidha, katika tukio hilo, watu wanne wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi,  akiwamo askari mmoja na raia  ambao walikuwepo kituo hapo kwa ajili ya kuripoti matukio mbalimbali ya uhalifu.
Mangu  ambaye aliwasili kituoni hapo akiwa na Kamanda wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema majambazi hao walifika kituoni hapo kama raia wa kawaida waliotaka huduma, lakini wakati wakianza kupewa maelekezo ya kusikilizwa walianza kumshambulia askari aliyekuwa akiwasikiliza.
“Ni kweli Jeshi la Polisi tumepata tukio kubwa ambalo ni la hatari na tumepoteza askari wanne, raia watatu na jambazi mmoja ambaye hatuwezi kumtaja jina lake kwa ajili ya usalama zaidi, pia askari wetu mmoja amejeruhiwa pamoja na raia wengine watatu waliokuwa kituoni,” Mangu.
IGP Mangu apoulizwa kuhusu idadi ya silaha zilizoibiwa alisema kwa sasa hawawezi kutaja idadi kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Hata hivyo, licha ya IGP Mangu kushindwa kutoa takwimu ya silaha zilizoporwa, taarifa zilizoelezwa na baadhi ya askari wa kituo hicho ambao hawakutaka kutaja majina yao kwa kuwa si wasemaji wa jeshi, walisema jumla ya silaha zilizoporwa ni 15 aina ya SMG.
 Mangu alisema pamoja na kwamba tukio hilo ni la kijambazi lakini linaweza kufananishwa na la kigaidi kutokana na kuuawa kwa askari na kukimbia na silaha.
NIPASHE
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema linaendelea kufanya uchunguzi wa mamilioni ya fedha zilizokamatwa katika Hoteli ya St. Gaspar mjini hapa, zinazodaiwa kuwa zilitolewa na Mfanyabiashara Yusufu Manji, kwa nia ya kuwahonga waliokuwa wajumbe wa vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime, jana alisema kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na kuahidi kutoa taarifa kamili kwa vyombo vya habari.
“Bado tunalishughulikia, subirini taarifa ikikamilika, tutaitoa tu, msiwe na wasiwasi wala msisababishe, tufanye kazi kwa shinikizo, “ alisisitiza Kamanda Misime,
Kwa upande wake, Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa(TAKUKURU),  Emma Kuhanga, alisema kuwa pamoja na kupata taarifa kuhusiana na tukio hilo kutoka kwa vyanzo mbalimbali, hawako tayari kulizungumzia kwa sababu linachunguzwa na Jeshi la Polisi.
Kuhanga alisema wao polisi wanachunguza tukio hilo kwa kuwa maofisa wa taasisi yao (Takukuru) hawakuwapo kwenye eneo la tukio na kwamba kwa kawaida polisi pia hushughulikia makosa ya rushwa.
“Ikitokea ushahidi ukakamilika, kwakuwa sisi tuna prosecutor (mwendesha mashtaka) wetu, polisi wakiona umuhimu wa kuhamishia suala wanaloshughulikia ambalo linahusu rushwa, wanaweza kulihamishia kwetu kwa kufahamu kuwapo kwa chombo maalumu kinachoshughulikia makosa ya rushwa tu, “ alisema Kuhanga.
Fedha hizo zilikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika hoteli hiyo iliyopo eneo la Kisasa, zikiwa mikononi mwa mfanyakazi wa Kampuni ya Quality Group (T), Amit Kevaramani, akiwa na hati ya kusafiria M1470774 ya nchini India.
Kiasi cha fedha kilichokamatwa ambacho hakijathibitika mara moja kinadaiwa kufikia  Sh. 725,2050,000.
Inadaiwa kuwa  fedha hizo zilikamatwa baada ya kuwapo kwa watu walioshtukia mwenendo wa mfanyakazi huyo wa kampuni ya Manji, aliyeonekana akihamisha mabegi makubwa  mawili na kupeleka kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje ya hoteli hiyo likiwa aina ya Toyota Land Cruiser.
Katika hoteli hiyo ambayo kulikuwa na wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu, na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM inadaiwa kuwa mamilioni hayo yalikuwa yanapelekwa kwa kambi ya mmoja wa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu wiki iliyopita kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
NIPASHE
Mkutano wa Waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, uliotakiwa kufanyika jana nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam, umehairishwa, huku kukiwa na taharuki juu ya kile alichotarajiwa kukizungumza kwa umma na taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikizagaa.
 Sababu za kuahirishwa kwa mkutano huo zinaelezwa kuwa ni kutokana na kuchelewa kufika kwa Lowassa akitokea mjini Dodoma.
 Mapema asubuhi jana Waandishi wa Habari walitakiwa kufika nyumbani kwa kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM kwa ajili ya kuzungumza jambo ambalo halikuwekwa wazi.
 Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari tangu majira ya saa 3:30 asubuhi, waliwasili nje ya nyumba hiyo na kuelezwa kuwa Lowassa bado hajafika na hivyo hakuna mkutano kama ilivyokuwa imetengazwa awali.
 Taarifa mbalimbali zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na WhatsApp zilikuwa zikieleza kuwa nyumba ya kiongozi huyo imezingirwa na watu wa usalama wa Taifa kwa lengo la kuimarisha ulinzi, huku wengine wakidai kuwa anajiandaa ‘kutimkia’ upinzani baada ya kukosa nafasi ya Urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 Katika mitandao hiyo kuna kiu kubwa ya watumiaji wake kutaka kusikia kauli ya kiongozi huyo baada ya jina lake kuenguliwa katika mchakato huo.
 Lowassa alijizoelea umaarufu wakati akiwa Waziri Kuu, wizara alizoziongoza ikiwamo Wizara ya Maji, Maendeleo ya Mifugo, kutokana na umahiri wake wa kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo.
Msemaji wa Lowassa, Abubakari Liongo, alisema mkutano huo wa Waandishi wa habari ulipangwa kufanyika jana majira ya saa 5:00 asubuhi, lakini ulishindikana kutokana na kwamba walichelewa kuwasili kutoka mkoani Dodoma.
“Taarifa zinazosambaa kuwa nyumba ya Mheshimiwa imezingirwa na watu wa ulinzi siyo za kweli, na waandishi waliofika pale asubuhi waliona hilo, pia kuhusu kuhamia upinzani ni maneno ambayo watu wameamua kuyaandika na kusambaza ila hakuna ukweli wowote,” alisema.
Alisema Lowassa atazungumza na waandishi wa habari kama alivyokuwa amepanga, lakini ni baada ya kukamilisha baadhi ya mambo na kwamba kila chombo cha habari kitajulishwa.
Tangu kutangazwa kwa mgombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho, Dk. John Magufuli, Julai 12, mwaka huu, Lowassa hajajitokeza mbele ya umma kuzungumza lolote, tofauti na wagombe wengine ambao tayari wametangaza kuunga mkono mgombea aliyepitishwa.
Katika mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma, Dk. Magufuli alimtangaza Mgombea mwenza ambaye ni Samia Suluhu Hassan.
 Lowassa ni kada aliyetangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM kupeperusha Bendera ya chama hicho, lakini jina lake lilienguliwa katika hatua za awali za Kamati Kuu ya chama hicho ambayo ilitoa majina matano.
Baada ya Kamati Kuu kumaliza kazi yake majira ya saa 6 usiku na majina matano kujulikana, wajumbe watatu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Adamu Kimbisa na Sophia Simba, walizungumza na waandishi wa habari kupinga maamuzi ya kamati hiyo na kwamba hawahusiki nayo.
Aidha, Julai 11, mwaka huu, Halmashauri Kuu ya CCM, ilikutana na kutoa majina matatu, huku katika mitaa mbalimbali kukiwa na maandamano ya wafuasi wa Lowassa, wakitaka jina lake kurejeshwa na kuwa miongoni mwa wanaoomba ridhaa ya chama hicho.
Shinikizo hilo lilisababisha majina matatu kutotajwa haraka, na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, alipoingia ukumbi wa mkutano alipokelewa na nyimbo za kushinikiza jina la Lowassa kurejeshwa miongoni mwa majina yanayotakiwa kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano huo.
Kikwete alishindwa kuendelea na mkutano huo na kuahirisha kwa kile kilichoelezwa ni kutoa nafasi kwa wajumbe kwenda kupata chakula cha mchana, na waliporejea hali ilikuwa tofauti kwani hakukuwa na nyimbo zozote.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeongeza majimbo 26 mapya ya uchaguzi Tanzania Bara, huku ikibadilisha majina ya majimbo 10.
Kati ya majimbo hayo, limo Jimbo la Ubungo linaloongozwa na John Mnyika (Chadema), Jimbo la Nzega ambalo Mbunge wake ni Dk. Hamis Kigwangwalla (CCM- Nzega) na Jimbo la Bunda linaloongozwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (CCM) yakimegwa na kuwa majimbo mawili.
Hata hivyo, majimbo manne yaliyoongezeka visiwani Zanzibar na kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), hayatakuwa na wabunge kwa kuwa Nec haijayaidhinisha kutokana na kukosa muda wa kurekebisha sheria ya uchaguzi kuruhusu mgawanyo huo.
Akitangaza majimbo hayo mapya Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema ongezeko la majimbo hayo limetokana na vigezo kadhaa ikiwamo ongezeko la watu na kuanzishwa kwa halmashauri mpya.
Jaji Lubuva alitaja majimbo yaliyoanzishwa kwa kuzingatia idadi ya watu ni Mbagala na Kibamba ya Dar es Salaam.
Majimbo mengine ni Manonga na Ulyankulu (Tabora), Mlimba (Morogoro) na Vwawa (Mbeya).
Jaji Lubuva alitaja majimbo 20 ambayo yameanzishwa ili kurekebisha mipaka kutokana na kuanzishwa kwa Halmashauri mpya ni Handeni Mjini (Tanga), Newala Mjini, Nanyamba na Ndanda (Mtwara), Makambako (Njombe) na Mafinga Mjini (Iringa), Butiama, Bunda Mjini na Tarime Mjini (Mara).
Mengine ni Tunduma (Mbeya), Nsimbo na Kavuu (Katavi), Geita Mjini (Geita), Kahama Mjini na Ushetu (Shinyanga).
Jaji Lubuva alitaja majimbo mengine kuwa ni Nzega Mjini (Tabora), Kondoa Mjini (Dodoma); Madaba na Mbinga Mjini (Ruvuma) na Mbulu Mjini (Arusha).
“Ongezeko la majimbo 26 kwa Tanzania Bara linaongeza majimbo ya uchaguzi kuwa 265 Tanzania nzima,” Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva alisema Nec imebadilisha majina ya majimbo 10 akitaja kuwa Rungwe Mashariki sasa ni Busekelo wakati Rungwe Magharibi litaitwa Rungwe.
Alisema Urambo Mashariki limebadilishwa na kuwa Urambo wakati Urambo Magharibi litaitwa Kaliua. Lingine ni Njombe Magharibi ambalo litaitwa Wanging’ombe na Njombe Kusini sasa ni Lupembe.
Bariadi Mashariki litaitwa Itilima na Bariadi Magharibi litaitwa Bariadi; wakati Kondoa Kaskazini litaitwa Kondoa na Kondoa Kusini litaitwa Chemba.
UHURU
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, amesema baadhi ya majukumu aliyopewa na wananchi hajayakamilisha, hivyo anasubiri uamuzi wa chama kuhusu hatima yake ya kuteuliwa tena kuwania ubunge.
Sugu alitoa kauli hiyo juzi wakati wa mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Ruanda, Nzovwe kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo baada ya kuwawakilisha bungeni kwa miaka mitano.
Pamoja na kuelezea mambo aliyofanya, Mbilinyi alitumia nafasi hiyo kuwaonya wapinzani wake wanaotaka kumpinga kwenye jimbo hilo.
“Nawashukuru watu wangu wa  Mbeya kwa kunipa heshima hii kubwa. Kujitokeza kwenu kunipokea kwa wingi inadhihirisha wazi  sikuwaangusha,” alisema na kuongeza: “Kuna mambo bado sijayamaliza, nahitaji kipindi kingine ili niweze kumalizia.”
Akifafanua Mbilinyi aliwataka wananchi kuwachagua madiwani wa upinzani ili wapate maendeleo.
Kwa upande wao, viongozi wa Chadema wilaya, Mkoa wa Mbeya na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, waliwataka makada wenye nia ya kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali, waelekeza dhamira kwenye majimbo yanayomilikiwa na CCM.
Mratibu wa Chadema kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema kuna majimbo 34, lakini ni majimbo manne yaliyokuwa yakishikiliwa na upinzani.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija alisema kitendo watu cha kujitokeza kwa wingi kumpokea mbunge wao ni ishara kwamba hakutakuwa na shida kumpata mgombea.

No comments:

Post a Comment