Wednesday, July 15, 2015

UKAWA na mgombea wao, MAGUFULI afunguka Urais na shuhuda tukio la uvamizi Polisi…#MAGAZETINI JULY15

Magazeti

UKAWA na mgombea wao, MAGUFULI afunguka Urais na shuhuda tukio la uvamizi Polisi…#MAGAZETINI JULY15

By
MWANANCHI
Mambo yamekuwa mazito. Ndivyo inavyoonekana baada ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kushindwa kutangaza mgombea urais jana badala yake ukatoa ahadi mpya kwamba sasa atatangazwa muda wowote ndani ya siku saba.
Kauli hiyo inayoibua maswali mengi imekuja baada ya viongozi wa umoja huo waliofanya vikao hadi usiku jana bila ya viongozi wakuu wa CUF ambao wameahidi kutoa msimamo wao leo saa 5.00 asubuhi.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye watamtangaza kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo alisema hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na naibu wake wa Bara, Magdalena Sakaya hawakuhudhuria kikao hicho kilichofanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.
Badala yake, Sakaya aliiambia Mwananchi jana jioni kuwa CUF haikuweza kushiriki kikao hicho kwa kuwa kulikuwa na mambo ambayo hawajakubaliana ndani ya chama na kwamba kama wangemaliza mapema, wangekwenda kwenye kikao hicho.
Baadaye usiku, CUF ilituma taarifa kwa vyombo vya habari ikisema kuwa itazungumza na waandishi wa habari leo saa 5.00 asubuhi kwenye ofisi za chama hicho Dar es Salaam kutoa taarifa kuhusu Ukawa.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF jana na habari kwamba chama hicho kitatoa taarifa peke yake leo, kunaweka giza nene mbele ya vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, ambavyo vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF kulisababisha Ukawa kushindwa kumtaja mgombea wake na habari ambazo zilipatikana awali, zilisema huenda vyama hivyo vikatangaza jina la chama kitakachotoa mgombea urais badala ya jina la mgombea.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema hoja kubwa ilikuwa katika suala la mgombea urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye ameshachukua fomu za CUF na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye anaungwa mkono na vyama vyote vinne.
Tayari Profesa Lipumba ameshagombea urais mara nne bila ya mafanikio, wakati Dk Slaa aligombea mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Sakaya alisema jana kuwa CUF haikushiriki kikao cha jana kutokana na kutoafikiana baadhi ya mambo ndani ya chama chake, ikiwa ni pamoja na suala hilo la kusimamisha mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa.
MWANANCHI
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema akichaguliwa kuwa rais, hatamwogopa mtu wala hataacha mtu aonewe, hasa wanyonge.
Dk Magufuli alikuwa akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Zakhem, Mbagala.
Katika mkutano huo ulioandaliwa CCM mkoani Dar es Salaam, Dk Magufuli alikuwa akitoa angalizo kila mara kuwa hawezi kuzungumza sana kwa kuwa wakati wa kampeni haujafika, ingawa katika hotuba yake fupi alitoa ahadi mbalimbali zenye sura ya kampeni.
Aliahidi kuwa atawashughulikia watendaji wa Serikali ambao ni wazembe na kuhimiza utekelezaji wa ilani ya CCM. Aliongeza kuwa hatamwonea haya mtu yeyote atakayekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Taifa.
“Mimi siyo mkali, mimi ni mtu mpole sana lakini nawachukia watendaji wa Serikali ambao ni wazembe, na hao ndiyo nitakao lala nao mbele,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria mkutano huo.
Dk Magufuli alisisitiza kuwa atasimamia ilani ya chama ambayo imezingatia masuala ya kilimo na biashara. Alisema ilani inawalinda wafanyabiashara wadogo na wakubwa, pia kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
“Maendeleo hayana chama lakini maendeleo ya kweli yataletwa na CCM. Wakati wa uchaguzi ukifika mchague wabunge na madiwani wa CCM ili kukamilisha mafiga matatu,”Magufuli.
“Ukiwa na tochi inayotumia betri tatu, wewe ukaweka betri mbili halafu katikati ukaweka gunzi, hiyo tochi itawaka?” Dk Magufuli aliuliza makutano ambao nao walimjibu kwa pamoja “haiwaki”.
Dk Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata kuanzia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) hadi viwanja vya Zakhem, Mbagala.
Alisema yeye na mgombea mwenza watahakikisha wanalipa fadhila kwa vitendo, endapo watashinda Uchaguzi Mkuu ujao na kuongoza Serikali.
“Ninawashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kuweka pembeni kambi zenu na kujitokeza kutupokea wagombea wenu. Tulikuwa wagombea 42 wenye sifa sawa, na kila mmoja alikuwa na kambi yake. Kuwa na kambi siyo kosa. Lakini wote wamevunja kambi zao na kuniunga mkono ili kukipa ushindi Chama cha Mapinduzi,” alisema.
MWANANCHI
Siku moja baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kuvamia kituo cha Polisi Stakishari kuua na kupora silaha, mmoja wa walionusurika katika tukio hilo askari Gaston Shadrack amesimulia hali ilivyokuwa.
Askari huyo aliyejeruhiwa bega la kulia na kifua kwenye uvamizi huo juzi usiku alisema alikuwa kwenye lindo kituoni hapo kabla ya wanaume wanane kufika na kudai wamedhulumiana.
“Ilikuwa saa 4 kuelekea saa 5 usiku. Lilikuja kundi la wanaume wanane wakiwa wamevaa makoti makubwa lakini hawajafunika nyuso. Walikuwa wakilalamika, “haiwezekani unidhulumu’ huku wakielekea ndani ya kituo.”
Aliongeza kuwa: “Utaratibu wetu ni lazima mtu akifika apite getini kwa mlinzi kwa ajili ya kupewa maelekezo ili aende ndani. Ila wao walitaka kwenda moja kwa moja,” alisimulia Shadrack ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Kutokana na utaratibu huo wa kuanzia getini, aliwaita watu hao kwa ajili ya kupata maelekezo ya kwenda ndani. Wakati huo akiwa na askari wenzake wanne hapo nje.
“…Kitendo cha kuwaita na kuwauliza mnakwenda wapi, wale jamaa waligeuka na kuvua makoti kumbe ndani walikuwa na bunduki. Wakaanza kutushambulia mimi na askari wenzangu ambao walianguka chini huku wengine wakifyatua risasi juu, nikageuka haraka na kulalia tumbo lakini wakati nageuka jambazi mmoja alinipiga risasi ikanipata kwenye bega la kulia na kifuani,” alisema Shadrack huku akionyesha majeraha hayo.
Alisema baada ya hapo majambazi hao waliingia kituoni na kuendelea kufyatua risasi lakini mmoja wao alibaki nje ya kituo.
“Nilitumia mwanya huo kunyanyua bunduki niliyokuwa nayo na kumfyatulia risasi akandondoka na mimi nikakimbia.”
Katika hatua nyingine, mmoja kati ya askari polisi wanne waliouawa katika tukio hilo, atazikwa siku moja na mama yake ambaye alifariki dunia baada ya kusikia kifo cha mwanaye, Koplo Gaudin.
Mkuu wa Polisi Ukonga, Mrakibu Mwandamizi, Jiliyo Simba alisema, mama wa askari huyo, alipoteza maisha baada ya kupokea habari za msiba wa mwanaye.
“Mama wa Koplo Gaudin alikuwa mgonjwa na alipopokea taarifa za kifo cha mwanaye naye alifariki dunia,”.
UHURU
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Kagame kati ya Yanga na Gor Mahia.
Dk Magufuli aliyepitishwa na mkutano mkuu wa chama hicho, Jumatatu mjini Dodoma amepewa heshima hiyo ikiwa ni kutambua mchango wake katika maendeleo wakati akiwa waziri.
Hilo litakuwa kusanyiko la kwanza kwa mwanasiasa huyo ambaye hakuwahi kujiainisha kwenye ushabiki wa soka, hasa kwa klabu kubwa, Simba na Yanga.
Wakati hayo yakiendelea, Shirikisho la Soka Tanzamia (TFF) limeahidi kuweka ulinzi maalumu wakati wa mashindano hayo.
Shirikisho hilo limeahidi usalama na ulinzi wakati wakati wote mashindano hayo kwa mashabiki na timu zote zitakazoshiriki.
Hakikisho hilo la TFF limekuja siku chache kufuatia kuibuka kwa matukio ya uhalifu jijini Dar es Salaam yanayohusisha uvamizi wa vituo vya polisi kwenye maeneo kadhaa.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na TFF ni kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimeombwa kutoa ulinzi maalumu kwa timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo.
Ulinzi huo kwa timu utahusisha misafara, hoteli zote ambako timu hizo zitafikia huku mikakati kiulinzi, ikiwa pia kwa mashabiki kwenye viwanja vitakavyotumika, Karume na Taifa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF, Baraka Kizuguto alisema kuwa pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama, pia wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha hakuna matukio ya aina yoyote yanayoweza kuvuruga au kuhatarisha amani kipindi chote cha michezo hiyo.
“Tunawahakikishia wapenzi wa soka na Watanzania kwa jumla kuwa kutakuwa na usalama wa kutosha kwani vyombo husika tayari vimeshachukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kuwa hakuna aina yoyote ya uvunjifu wa amani na ulinzi utakuwa ni wa uhakika, hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi,”  Kizuguto.
Katika hatua nyingine, Alhamisi kutakuwa na mtihani maalumu kwa waamuzi, Cooper Test ambako wale wakatakaofuzu ndiyo watachezesha mashindano hayo.
NIPASHE
Wakati bado hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa kufuatia tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi cha Stakishari, jijini Dar es Salaam, imefahamika kuwa bunduki zilizoibwa ni 20, huku Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP ), Ernest Mangu, akitangaza bingo ya Sh. milioni 50 kwa mtu atayekatoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa majambazi waliofanya tukio hilo.
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walikivamia kituo hicho usiku wa kuamkia Julai 12, mwaka huu na kuwaua askari polisi wanne, raia watatu na kisha kupora silaha kadhaa na kutokomea nazo kusikojulikana.
Kwa nyakati tofauti, IGP Mangu wa idadi ya silaha zilizna Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, kila wanapoulizoporwa na majambazi hayo, wamekuwa wakishikwa kigugumizi kusema.
Hata hivyo, taarifa zilizothibitishwa na baadhi ya askari wa kituo cha Stakishari zimeeleza kuwa jumla ya silaha zilizoporwa katika kituo hicho ni 20 ambazo ni aina ya Sub Machine Gun (SMG).
“Kisingi majambazi waliovamia kituo chetu siyo majambazi wa kawaida hawa ni magaidi, wamepora SMG 20…Hali inatisha, “alisema askari polisi mmoja wa kituo hicho .
Wakati hayo yakiendelea, Mkuu wa jeshi hilo, Mangu ametangaza zawadi ya Sh. milioni 50 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa majambazi waliovamia  kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo wamelichukulia kwa uzito wa kipekee  na wanafanya jitihada za kufa na kupona kuhakikisha wahalifu waliohusika wanakamatwa.
Kamishna Kova alisema katika kukabiliana na majambazi wanaovamia vituo vya polisi, zitafungwa kamera za CCTV katika vituo vyote vya polisi nchini.
Aliongeza: “IGP ameamua kutoa fedha hizo ili kumzawadia atakayefanikisha kupata taarifa za wahalifu, fedha hizo zipo tayari na tunawahakikishia kwamba tutamlinda mtoa taarifa na zawadi yake tutamkabidhi kimya kimya kama ambavyo tumekuwa tukifanya vipindi vilivyopita.”
Alisema hadi sasa bado hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kuhakikisha wahalifu wanatiwa mbaroni.
Kova alitaja baadhi ya namba  za Makamanda wa Polisi watakaokuwa wanapokea taarifa za watoa taarifa za watuhumiwa kuwa ni 0754 034224 ya kwake mwenyewe, Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba (0713 631667) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani 0715 323444.
NIPASHE
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Isaya Mungurumi, amewataka wafanyabiashara waliovamia viwanja vya Jangwani kuondoka mara moja kutokana na kujimilikisha maeneo hayo kinyume cha sheria.
Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa Manispaa ilikubaliana na Serikali kutenga sehemu ndogo katika viwanja hivyo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili kupunguza msongamano katika soko la Kariakoo.
Aidha, alisema kitu cha kushangaza ni kuwa kabla ya manispasa kuanza ugawaji wa maeneo hayo kwa wafanyabiashara wadogo, kuna watu walijitokeza na kuwauzia wafanyabiashara wengine kinyume cha sheria na kusababisha kero kubwa.
“Nimeandaa timu ya kuwashughulikia watu hao, hivyo naomba waondoke eneo hilo mara moja kabla sheria haijachukuliwa dhidi yao, hatuwezi kuruhusu watu kuanza shughuli zao za kibiashara katika maeneo ambayo hayajaandaliwa na kuwekwa huduma muhimu za kibinadamu,” Mngurumi.
Aliongeza kuwa baada ya maeneo hayo kutengwa na kuwa katika hali ya usafi, vitawekwa vyoo vya kuhamisha ili vitumike kwa wafanyabiashara na watu wote watakaotembelea maeneo hayo.
Mungurumi alisisitiza zaidi kuwa eneo litakalotumika ni moja na kubainisha kuwa maeneo yaliyopo karibu na ofisi za Dart hayaruhusiwi kuguswa na kuongeza kuwa utaratibu maalum utatumika kuyagawa maeneo yaliyopangwa kwa wafanyabiashara na siyo kuwamilikisha ili kutumika katika kipindi hiki cha kiangazi.
Kadhalika, alisema Manispaa imeamua kutumia eneo hilo kutokana na wafanyabiashara wengi wadogo kupanga bidhaa zao barabarani hasa katika soko la Kariakoo hivyo kusababisha kero kwa watembea kwa miguu na wakati mwingine kufunga barabara kabisa na kusababisha msongamano wa magari.
Alisema wakati wakiwatafutia hifadhi ya muda wafanyabiashara hao, manispaa inajiandaa kujenga masoko matatu ili wawe na maeneo sahihi ya kufanyia shughuli zao.
Masoko yatayojengwa ni Kisutu, Mchikichini na Buguruni na kwamba mazungumzo yameanza na benki kwaajili ya kutoa mkopo kufanikisha mkakati huo unaotarajia kuanza mapema iwezekanavyo.
NIPASHE
Wadau wa mawasiliano mkoani hapa,  wameiomba Mamlaka ya Mawasiliano  Tanzania (TCRA), kudhibiti matumizi mabaya ya simu za mkononi na mitandao hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba 25, mwaka huu.
Wadau hao walitoa rai hiyo juzi mjini hapa, kwenye warsha iliyotolewa na TCRA kwa lengo la kuwakumbusha wananchi manufaa ya mawasiliano.
Wadau hao walisema kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia, ndivyo ujumbe wa kupigana  vijembe kwa lengo la kuchafuana kisiasa zinazidi kukithiri na kuendelea kuwachanganya wananchi.
Akizungumza kwenye warsha hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, Edward Mgaya,  aliwataka wananchi wasitumie simu zao vibaya kwa kuchafuana au kufanya malumbano kwenye mitandao ya kijamii hasa wakati huu wa uchaguzi.
“Ndugu zangu wananchi wa Njombe ninawaombeni kipindi hiki cha uchaguzi tumieni simu zenu vizuri msichafuane ili muweze kufanya uchaguzi kwa amani na mpate kiongozi atakayewatatulia changamoto zenu, ”alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohuduria warsha hiyo, walitoa tahadhari ya matumizi ya simu kifamilia kwa kutopokea picha zinazoweza kuhatarisha au kuvunja ndoa zao.
Kwa upande wake  Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana, aliwataka wakazi wa Njombe kutumia mawasiliano ya simu kutafuta masoko ya mazao yao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, aliitaka Mamlaka hiyo kupunguza gharama za simu.
Mkuu wa Kitengo cha  Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi,  amewaondoa hofu wananchi wanaoishi karibu na minara ya mawasiliano kuwa haina madhara kwao.
Mungi alisema hakuna mionzi yoyote inayoweza kuwadhuru wananchi kwa sababu minara hiyo imefungwa vifaa muhimu na vyenye kiwango vya kimataifa.
HABARILEO
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limesema Raia wa India, Amit Kevalramani mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam aliyekamatwa na Sh milioni 772 katika Hoteli ya St Gasper Mjini Dodoma wiki iliyopita hana hatia yoyote, kwani hakuna tuhuma zozote za rushwa zilizothibitika.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema hakuna tuhuma zozote za rushwa zinazomhusisha moja kwa moja na masuala ya uchaguzi.
“Katika tukio hili na uchunguzi tulioufanya, tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwani hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo,” alisema.
Akielezea mazingira ya tukio hilo, Misime alisema Julai 11, mwaka huu katika Hoteli ya St. Gasper ya mjini Dodoma, wananchi walitoa taarifa majira ya saa 10:00 jioni kuwa kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia, amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, polisi walifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.
“Askari walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia akiwa na fedha kiasi cha milioni 722.5 na alipohojiwa alisema alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka,” alisema.
Misime alisema kwa mujibu wa mtu huyo, alifika Dodoma Julai 10, mwaka huu majira ya asubuhi na kufikia Hoteli ya St. Gasper na siku iliyofuata Julai 11, aliamua kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya vurugu.
Misime alisema mtu huyo akiwa katika harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli ya St. Gasper, walimtilia shaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa Polisi.
“Mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa na mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe,” alisema.
Alisema taarifa za aina hiyo, hata Jeshi la Polisi lilikuwa limepokea bila uthibitisho. Alisema Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliothibitisha vinginevyo, amerejeshewa fedha zake.
HABARILEO
Mkongo wa Taifa wa mawasiliano unaounganisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi na Zambia, umehujumiwa miundombinu yake na baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo yanayopitiwa.
Meneja wa Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), Ekaeli Manase alisema hayo jana wakati akizungumza ukaguzi wa maeneo yaliyo karibu na yanayopitiwa na mkongo huo mkoani Dodoma.
Alisema jamii ina nafasi kubwa kufichua wanaohujumu miundombinu hiyo kwa faida ya taifa.
Manase alisema kwa mkoa wa Dodoma pekee, zaidi ya Sh milioni 30 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa kwa ajili ya kuunganisha nyaya zilizokatwa na kuibiwa na wananchi.
Manase alisema jamii ina nafasi kubwa kufichua wanaohujumu miundombinu hiyo kwa faida ya serikali, kutokana na umuhimu wake unaochangia kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma bora za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) zenye ufanisi kupitia kuboreshwa kwa huduma za miundombinu hiyo.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Polisi Tarafa ya Dodoma, Ramadhan Mambea, aliwataka wananchi kushirikiana na vikosi vya ulinzi shirikishi kwa ajili ya kuulinda mkongo huo wa mawasiliano, ambao ni muhimu katika mawasiliano ndani ya nchi na nje.
Alisema Jeshi la Ulinzi shirikishi limejipanga kutumia vikundi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanalinda mkongo huo kwa kuwafichua na kuwakamata wahalifu.
Faustina Bendera, mkazi wa Chinyoya, akizungumza kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo, aliishauri serikali kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuwepo kwa mkongo huo, ambao umekuwa ukihujumiwa na watu kutokana na kukosa elimu.

No comments:

Post a Comment