Wednesday, February 17, 2016

Kadi za Kiiza, Juuko zaivuruga kambi Yanga

Kadi za Kiiza, Juuko zaivuruga kambi Yanga

HAMISI-KIIZA.jpgMchezaji wa Simba, Hamisi Kiiza.
HAMISI-KIIZA.jpg
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

TIMU za Simba na Yanga zitashuka uwanjani, Jumamosi hii kuonyeshana ubabe katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati homa ya mechi hiyo ikizidi kupamba moto, mapya yameibuka katika kambi ya Yanga iliyopo kisiwani Pemba baada ya baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kudai kuwa Simba nayo imepata pigo kubwa kama ilivyokuwa kwao ambao watamkosa Kelvin Yondani kwenye mechi hiyo.

Yondani anatumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu kutokana na kitendo chake cha kumdunda daktari wa Coastal Union ya Tanga.

Taarifa zinasema kuwa viongozi wa Yanga wamewaeleza wachezaji wao kuwa kuna wachezaji wanne wa Simba wana kadi tatu za njano na wataukosa mchezo wa Jumamosi.

 

Wachezaji waliotajwa ni Hamisi Kiiza, Juuko Murshid, Hassan Kessy na Ibrahim Ajib.

Jambo hilo liliwachanganya baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao waliona kuwa ni jambo geni kwao na kujikuta wakitumia muda wao mwingi kutafuta ukweli wake.

Hata hivyo, baada ya Championi Jumatano kupata taarifa hizo lilimtafuta Meneja wa Simba, Abbas Ally, ili kujua ukweli wake ambapo alisema kuwa timu hiyo haina mchezaji yeyote mwenye kadi tatu za njano isipokuwa ina wachezaji sita wenye kadi mbili za njano.

 

“Hatuna mchezaji yeyote mwenye kadi tatu za njano ila tuna wachezaji kama sita waliokuwa na kadi mbili za njano ambazo walizipata kabla ya mechi yetu na Stand United,” alisema Abbas na kuwataja wachezaji hao kuwa ni Kiiza, Juuko, Kessy, Ajib, Mwinyi Kazimoto na Abdi Banda.

Kama haitoshi gazeti hili lilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura naye alisema kuwa anatafuta takwimu hizo lakini hadi tunakwenda mtamboni hakupokea simu.

Baada ya wachezaji hao wa Yanga kupewa taarifa hizo walilipongeza Championi kwa kuwaambia ukweli juu ya jambo hilo na kudai kuwa: “Jamaa walitaka kutuingiza chaka, hivyo tunashukuru kwa mchango wenu wa kutuambia ukweli na sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi hiyo.”

No comments:

Post a Comment