Wednesday, February 17, 2016

MAWAZIRI WA RAIS MAGUFULI WAANZA KUVURUGA, WAKUMBWA NA HOFU.

MAWAZIRI WA RAIS MAGUFULI WAANZA KUVURUGA, WAKUMBWA NA HOFU.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mpoki Ulisubisya (mbele) akisaidia kuondoa vifaa katika jengo lililokuwa likitumiwa na wafanyakazi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambalo Rais John Magufuli aliagiza litumike kuwa wodi ya wazazi. Picha na Maktaba 

Dar es Salaam. 
Staili za utendaji wa mawaziri na viongozi wengine wa Serikali ya Rais John Magufuli za kujionyesha na wakati mwingine kushiriki kazi ambazo si za kwao zimeelezwa na wachambuzi kuwa zinatokana na hofu na kujikomba. 

Tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana, utendaji kazi wa Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa umekuwa wa aina tofauti na mazoea ya wengi, hivyo kuwalazimu mawaziri hao na watendaji wengine kuiga staili ya kushtukiza na kuongeza mbwembwe za kila aina. 

Baadhi yao wamekuwa wakishiriki kazi kwa vitendo, kufanya ziara za ghafla, kusimamisha na kuwatimua kazi watendaji wa umma, hali inayoelezwa kuwa pia inatokana na kukosekana na mfumo maalumu wa utendaji, badala yake kila mmoja kuiga kadri anavyoweza. 

Katika matukio hayo, baadhi ya viongozi wamekuwa wakijipiga picha na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwa lengo la kuonyesha jinsi wanavyowajibika ‘kutumbua majipu’. 

Baadhi ya wachambuzi walisema wapo mawaziri na watendaji wachache walioonyesha weledi katika kutimiza wajibu wao na matunda ya kazi zao yameanza kuonekana, baadhi wanaiga kwa vituko huku wengine wakiwa kimya. 

Miongoni mwa matukio hayo ni lile lililotokea juzi, wakati wa utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli kubadili matumizi ya jengo la Wizara ya Afya kuwa wodi lililowafanya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wake, Dk Mpoki Ulisubisya kushiriki kubeba samani na hata kufagia. 

Katika tukio jingine la Desemba 18 mwaka jana, Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla aliwafungia geti wafanyakazi wa ofisi ya wizara hiyo waliofika ofisini baada ya saa 1.30 asubuhi na kuwataka waandike barua kueleza sababu za kuchelewa huku akiahidi kufanya kazi hiyo kila siku, lakini hajarudia. 

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Nchemba amefanya ziara za usiku mara mbili Januari 4 na Februari 12 katika mnada wa mifugo Pugu na machinjio ya Vingunguti na Mazizini, Dar es Salaam na kuwatimua baadhi ya watumishi kwa kupindisha taratibu. 

Akiwa Iringa, Nchemba aliwasimamisha kazi viongozi wa vyama vya msingi vya tumbaku mkoani Iringa wanaotuhumiwa kushiriki katika ufisadi wa mkopo wa matrekta kupitia mgongo wa vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku na kujimilikisha wenyewe. 

Mbali na Nchemba, mawaziri wengine kama George Simbachawene wa Tamisemi, Profesa Jumanne (Maghembe wa Maliasili na Utalii), January Makamba (Mazingira na Muungano), Jenista Mhagama (Sera Uratibu, Kazi na Walemavu), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) wametimua watendaji kwa sababu mbalimbali kama wafanyavyo Rais na Waziri Mkuu. 

Watendaji wengine 
Mbali na mawaziri hao, hata watendaji wengine wa ngazi za wilaya na mikoa nao wamekuwa katika mfumo huohuo, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Ponsiano Nyami aliyeagiza kuvuliwa madaraka kwa Mganga wa Kituo cha Afya Byuna, Innocent Magembe kwa kukiuka miiko ya kazi kwa kufanya uzembe na kusababisha mjamzito, Esther Maige kujifungulia nyumbani. 

Pia yumo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Paul Makonda aliwaweka ndani maofisa ardhi 20 kwa kile kilichoelezwa kuchelewa katika eneo la mkutano kusikiliza migogoro ya ardhi. 

Katika tukio jingine, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla alipiga marufuku likizo za wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa idara kwenye mkoa wake ili kutekeleza kwa vitendo hotuba na maagizo ya Rais Magufuli. 

Pia limo tukio la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk Nikson Itogolo na katibu wa hospitali ya wilaya hiyo, Michael Ndalahwa kuondolewa kwenye nafasi zao kwa kushindwa kusimamia majukumu yao ya kazi. 

Wasemavyo wasomi 
Akizungumza staili za utendaji huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema baadhi ya viongozi hao hawatumii weledi isipokuwa wanatekeleza wajibu wao kwa hofu. 

“Binafsi naona nchi yetu sasa inaongozwa kwa hofu, wengine hawatumii weledi, wanahofia vibarua vyao kupotea, ndiyo maana siku hizi imekuwa kama vituko, ni mwendo wa kutoa siku kadhaa, kutimuana, kukurupuka na kikubwa ni matumizi ya mitandao ya kijamii,” alisema. 

Sanga aliongeza: “Hawana namna, hasa mawaziri kwa sababu walishaambiwa wazi kwamba, ikiwa hawatoshi watatimuliwa na yule atakayetosha ataendelea. 


Kila mtu anajitahidi kutosha hata kama hajui afanye nini.” Alisema hakuna sera iliyoelezwa kuwa ndiyo inayotekelezwa, isipokuwa kila kiongozi anaiga utendaji wa Rais kulingana na matukio hata kama eneo lake linahitaji ubunifu. 

Wakati Sanga akisema hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Benson Bana alisema mawaziri hao kushiriki kazi wa vitendo siyo mbaya, bali ubaya unakuja pale wanapofanya kwa shinikizo, kujionyesha au nidhamu ya woga. 

“Siyo vibaya kiongozi kufanya kazi akaonyesha mfano, hata Baba wa Taifa alifanya hivyo, lakini huwa hainiingii akilini pale ninapomwona waziri anahangaika baada ya Rais kuagiza, ina maana haijui wizara yake? Nidhamu ya woga haina tija,” alisema. 

Aliwataka kusoma mazingira na ripoti za wizara zao kisha kubuni vitu vipya vitakavyosaidia kuleta mabadiliko ili kuondoa kero lukuki zinazowakabili wananchi. 

Alisema ikiwa watasoma vizuri majukumu yao, kujua changamoto za wizara zao ukiwamo upungufu, watapata njia nzuri za kuyatatua. 

“Wasingoje Rais afanye ndipo nao waige, siyo kwamba kazi bila kamera haiwezekani, wakitimiza wajibu wao ipasavyo watang’aa tu,” alisema. 

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema viongozi hao wanatekeleza wajibu wao huku njia pekee ya kuonekana ikiwa ni kutumia vyombo vya habari. 

Alisema wengi wanaongozwa kwa hofu na imefikia hatua kila mmoja anaogopa na hivyo kujitahidi kazi atakayofanya inaonekana. 

Alisema kinachowatia hofu zaidi wakuu wa wilaya na mikoa ni kuwapo au kutokuwapo kwenye uteuzi ambao bado haujafanywa. 

“Bahati mbaya kwa wakuu wa wilaya, aliyetolewa mfano ni Makonda ambaye anaweza kucheza na vyombo vya habari, tutarajie kwamba hizi ‘drama’ zitaendelea mpaka pale uteuzi wake (Rais) utakapokamilika,” alisema Mbunda na kuongeza: 

“Pale linapotokea jambo linalogusa jamii moja kwa moja, walau nafarijika kwamba linashughulikiwa haraka, japo matokeo ya staili hii haiwezi kuonyesha matokeo ya haraka.” 

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Muhas), Dk Ave Maria Semakafu alisema wakati wa kutoa maagizo ya uongo bila ufuatiliaji umepita. 

Alisema kinachowaumiza viongozi hao ni kwamba wanaongoza wakati kukiwa na uozo mwingi. 

“Kubadilisha fikra za binadamu ni vigumu hasa wakati huu ambao mabadiliko yanahitajika. Utendaji kazi wa vitendo na ziara ni mzuri kuliko ule wa kukaa ofisini na kusubiri taarifa,” alisema.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment