Sunday, February 21, 2016

ANGELINA MABULA: Mbunge aliyehofiwa na familia kabla ya kampeni...................

ANGELINA MABULA: Mbunge aliyehofiwa na familia kabla ya kampeni


“NIMEYAPOKEA matokeo ya ubunge kwa furaha kubwa moyoni mwangu, nilipambana na changamoto nyingi wakati wa kampeni, lakini namshukuru Mungu nimevuka salama na ninawashukuru kwa namna ya kipekee wananchi wa Ilemela kwa kuniamini. Niseme tu ninalo deni kubwa kwao la kuwaletea maendeleo.” Hiyo ni kauli ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angelina Mabula ambaye amechaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela.
Ametwaa jimbo hilo kutoka kwa Highness Kiwia, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema. Anasema yeye si mgeni katika shughuli za uwakilishi na si mgeni wa utendaji kazi wa mihimili mingine ya serikali. Amewataka wananchi watarajie mabadiliko makubwa ya kiutendaji yanayokwenda sawia na utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Mabula alishinda kiti cha ubunge cha jimbo hilo baada ya kupata kura 85, 424 na kumbwaga Kiwia aliyepata kura 61,679.
Wagombea wengine wa vyama vya siasa waliochuana naye na kura zao kwenye mabano ni Mkiwa Kiwanga wa ACT Maendeleo ( 3,910), Hutu Shaban wa ADC-(626), George Kababu wa CUF (427), Kelvin Mturi-Jahazi (72), Bosco Bukaiga wa UPDP (54) na Clement Masoyi wa DP aliyepata kura 54 pia. Angelina Mabula anasema kwenye ushindani lazima apatikane mshindi na kuwa anawashukuru wana Ilemela kwa kumuamini na kumchagua.
” Wananchi walifanya uamuzi kama wao na niseme walifanya chaguo sahihi, na mimi kazi iliyo mbele yangu ni kuwahudumia wananchi wote bila ya kujali itikadi za vyama vya siasa, dini, rangi au ukabila maana Tanzania yetu ni moja na sisi sote ni wamoja,” anaeleza. Anasema kazi kubwa iliyo mbele yake ni kushughulika na changamoto zinazowakabili wananchi kwa kujenga mazingira wezeshi yatakayowezesha kumfikia kila mmoja wao.
Anaishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushirikiana na vyombo vingine kuendesha na kusimamia uchaguzi ambao umemalizika kwa amani. Uwezeshaji Anasema kipaumbele chake cha kwanza akiwa mbunge wa Ilemela, ni uwezeshaji mkubwa wa uchumi kwa jamii. Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka huu, ilishataangaza neema ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji, hivyo jukumu lake la ubunge ni kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
“Nadhani Ilemela tukipata fedha hizo, tutakuwa wa kwanza kuzipeleka kwa walengwa, na niseme tu jukumu hilo nitalisimamia ili kuhakikisha neema hiyo iliyotangazwa inawafikia watu wenye uhitaji,” anasema. Uzoefu Mabula anakumbuka akiwa mtumishi wa Serikali, baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya (DC) na Rais Jakaya Kikwete, anasema baadhi ya majukumu yake alipokuwa katika nafasi hiyo ya uteuzi na mbunge kwa sasa hayana tofauti kubwa.
“Sioni kuna tofauti kubwa, DC ni mteule wa Rais na mtumishi wa umma, na moja ya kazi yake kubwa ni kusimamia halmashauri, ili zitekeleze majukumu yake... mbunge yeye ni mwakilishi wa wananchi anashughulikia zaidi changamoto za kijamii,” anasema. Anasema atafanya kazi kwa kushirikisha jamii kwa karibu, ili aendelee kubaini changamoto inazokabiliwa nazo na kwa kushirikiana na vyombo vingine ili azitafutie majawabu.
“Mimi naamini zaidi katika kufanya kazi kwa mfumo wa ushirikishaji jamii, natarajia kuwa na jukwaa na makundi mbalimbali ya kijamii ili tujadili kwa pamoja na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya jimbo letu na Taifa kwa ujumla,” anasema. Anavyomuona Dk Magufuli Anasema Tanzania imepiga hatua muhimu ya ukuaji wa demokrasia nchini, baada ya kumpata Dk John Magufuli, kuwa Rais wa Awamu ya Tano katika uchaguzi wa huru wa haki na uliofanyika kwa amani na utulivu mkubwa.
Anamuelezea Dk Magufuli kuwa ni mchapakazi na kuchaguliwa kwake kuwa Rais, watumishi wa umma wazembe ni lazima wabadilike kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa, ili waendane na kasi yake. “Tunaingia katika awamu ya tano ya uongozi wa nchi tukiwa na Dk Magufuli ambaye ni mtu ambaye hana masihara katika kazi,” anasema na kuongeza; “Watanzania wenye kupenda maneno mengi bila vitendo walitambue hilo na njia nzuri ya mtu kuimarika kiuchumi ni kufanya kazi, maendeleo hayawezi kuja kwa mtu ambaye hafanyi kazi,” anasema.
Anasema hatamuangusha Dk Magufuli, anaahidi pia kusimamia utungaji wa sheria bungeni, ili zisiwe kandamizi kwa mwananchi wa kawaida. “Nitajitahidi na wenzangu bungeni kupitia sheria zote ambazo ni kandamizi ili ziondolewe na kuleta usawa wa kila mmoja nchini,” anasema. Anavyomuona Rais Kikwete Mabula ambaye ni mama wa watoto wanne David, Dianna, Dorothy na Jackline, anasema atamkumbuka daima Rais Jakaya Kikwete kwa ushirikishaji wake vijana kwenye uongozi wa nchi.
Anasema Rais ametumia vyema mamlaka yake ya kikatiba kuteua vijana wengi kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Mabula anasema uteuzi huo ulimgusa yeye mwenyewe baada ya Rais Kikwete kumteua kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Wilaya wa Kwanza wa Wilaya mpya ya Butiama, iliyoko mkoani Mara alikozaliwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. “Namshukuru Rais Kikwete kwa kuniteua nimsaidie katika nafasi ya ukuu wa wilaya mpaka hapo nilipoamua kuondoka mwenyewe.
Nimefanya kazi kwa uaminifu mkubwa,” anasema. Anawaomba Watanzania waendelee kudumisha upendo, umoja na mshikamano wa pamoja na kuhakikisha siku zote wanaanza na Mungu na kumaliza na Mungu.
*Changamoto ya u-DC
Anasema changamoto aliyokumbana nayo akiwa DC, ni alipotoa maelekezo ya kisheria yaliyoonekana kama ni kuwakandamiza wananchi. “Ingawa ukiwa kiongozi ni lazima uongoze kwa kufuata taratibu za kisheria, pale nilipotekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa sheria, watu wengine walidhani ninawaonea. “Mara nyingi wananchi wanataka ‘short cut’, mtu anapochukua njia ya mkato na wewe unasimamia sheria, inaonekana kama wewe unamnyanyasa, lakini ukiwa mtumishi wa umma ni lazima usimamie sheria za nchi,” anasema.
Anasema Rais Kikwete katika awamu zake mbili za uongozi, amefanya mambo mengi makubwa, ameimarisha michezo, ameshughulikia malipo ya pensheni kwa wazee na ameruhusu uhuru mpana wa watu kujieleza na kufanya uamuzi. “Rais amekuwa mwanadiplomasia aliyepitiliza, alitoa uhuru mkubwa wa vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao jambo ambalo ni la kupigiwa mfano, vimekuwa na ushiriki mpana katika shughuli zake za kiserikali ambazo zimekuwa ni za mafanikio makubwa,” ameeleza.
Matarajio yake Anasema katika kipindi chake cha ubunge, atafanya kazi na makundi yote katika jamii na hatawaangusha wana Ilemela kwenye shughuli za maendeleo. “Nitaimarisha huduma za kijamii, afya nikijikita katika afya ya mama na mtoto, maana akinamama ndio waathirika na wahitaji wakubwa wa huduma za afya, maji na miundombinu imara,” anasema.
Anasema atashiriki kikamilifu kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa kwa ngazi zote za uongozi, ili mwananchi wa kawaida apate haki yake kwa wakati. “Elimu zaidi itatolewa, maana katika ngazi ya mitaa na kata, kuna baadhi ya wananchi hawana uelewa wa sheria na elimu ya uraia,” anasema na kuongeza; “Nitasimamia utekelezaji wa sheria na kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, ili tukienda kwenye shughuli za maendeleo kila mtu awajibike,” anasema.
Anasema haoni kama kitu anakipoteza baada ya yeye kuchaguliwa kuwa mbunge, na kuiacha nafasi yake ya ukuu wa wilaya aliyokuwa nayo awali. “Sioni kama kuna kitu nakikosa, unapokuwa mwakilishi wa Rais wewe ni msimamizi wa mambo yote wilayani, tofauti ya majukumu ya DC na ya mbunge ni kwenye uamuzi, mbunge hana nafasi ya kufanya uamuzi kama DC,” anasema.
Anasema atatumia uzoefu wake kufanya kazi serikalini kwa kushirikiana na watumishi wengine wa umma, ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. *Wanaomvutia Viongozi wanawake anaowapenda hapa nchini kwa mujibu wa Mabula ni Gertrude Mongela na Dk Asha Rose Migiro. “Mongela anapenda sana kushirikisha wanawake wenzake na Dk Asha Rose Migiro nina wivu wa kimaendeleo kwake, akifanya uamuzi wake huwa hauna papara na ukiiga utendaji kazi wake, huwezi kukwaruzana na mtu yeyote yule,” anasema.
Anaona mfume dume ni kikwazo kingine cha wanawake wanaonesha uthubutu katika jamii, hali ambayo anasema bila ya kujali dhana hiyo ya ukandamizi, wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Anaishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi kwa kuwezesha uchaguzi wa mwaka huu kumalizika kwa amani na utulivu, ingawa kulikuwa na watu waliojenga fikira za kuhamasisha vurugu.
“Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na wasiwasi mkubwa na hamasa kubwa ya vijana ambapo asilimia 60 ya watu waliojiandikisha, walikuwa vijana na baadhi ya vyama vya siasa viliamini kuwa haki insingetendeka lakini uchaguzi umemalizika kwa amani,” anasema. Ameishukuru NEC kwa kufanya kazi nzuri ingawa kulikuwa na dosari ndogo kwenye uchaguzi huo na kutangaza matokeo kwa muda muafaka.
Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia afya njema, hadi kumuwezesha kuomba nafasi hiyo ya ubunge. *Familia “Niishukuru familia yangu ambayo awali nilipoeleza nawania ubunge, walipata kigugumizi kidogo, wazazi wangu hawakunielewa kabisa, waliniambia mimi ni Mkuu wa Wilaya na kwanini niiache nafasi hiyo nikawanie ubunge, lakini hatimaye walinielewa,” anasema.
Wakati anaingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge, anasema hakuwa na hofu kwa kuwa aliamini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na ya wa-nanchi angeshinda na ndivyo ilivyokuwa. “ Nilimtanguliza Mungu kwa chochote nilichokifanya...nichukue fursa hii kuwatia moyo wanawake wenzangu wajitokeze nao kuwania nafasi mbalimbali za uongozi,” anasema.
Anaushukuru uongozi wa CCM Mkoa na Wilaya kwa kumpa nafasi pana iliyomuwezesha kuingia kwenye mchakato huo, anashukuru makundi mbalimbali ya jamii, vijana, akina mama na wazee kwa kumuunga mkono katika jitihada zake hizo. “Makundi yote hayo niliyafikia na kusema nayo ...kwakweli niwashukuru wote hao,” anasema na kuushukuru uongozi na watumishi wa Halmashauri ya Ilemela kwa ushirikiano wanaompatia.
Historia Mabula alianza safari yake ya uongozi mwaka 1981, baada ya kuhitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, iliyoko jijini Mwanza. Mwaka 1983 alitunukiwa Cheti cha Uhasibu kutoka Chuo cha Uhasibu Kurasini Jijini Dar es Salaam. Mwaka 1984 alipata Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa katika Kambi ya Oljoro JKT na kuhitimisha safari ya mafunzo hayo katika Kambi ya JKT, Kitengo cha Operesheni Nguvu Kazi.
Safari yake ilizidi kupamba moto ambapo mwaka 1990 alitunukiwa Stashahada ya Juu ya Uhasibu kutoka Chuo cha IFM kilichopo Jijini Dar es Salaam na mwaka 1991 Stashahada ya Uzamili kutoka Chuo cha IFM Dar es Salaam. Ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo mwaka 2000 alitunukiwa Shahada ya Uhasibu na mwaka 2007 alihitimu Stashahada ya Maendeleo na Uongozi kutoka Taasisi ya Coady International ya nchini Canada na mwaka 2014 akahitimu Shahada ya Uzamili katika Maendeleo ya Jamii na Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mchango wake wa uongozi umedhihirika zaidi baada ya kuonesha ujasiri wa kuwania nafasi za uongozi, ambapo aliwahi kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Ilemela, *Utumishi wa umma Machi mwaka 2009 hadi 2012, aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na mwaka 2012- 2015, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya wa Kwanza wa Wilaya mpya ya Butiama iliyoko mkoani Mara.
Mwaka 2015 hadi sasa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa mkoani Iringa nafasi aliyokuwa nayo hadi pale alipojiuzulu kwa hiari nafasi hiyo na kwenda kugombea ubunge. Mabula ni mmoja kati ya wanasiasa vijana hapa nchini wanaopenda mabadiliko ya kuwakomboa vijana wa kike na kiume kutoka fikra hasi kwenda fikra chanya.
Anaamini vijana ndiyo nguvu kazi na rasilimali ya taifa na kwamba ujana kwake ni harakati na uzee kwake ni maono, akiwa na nia ya kuutumia vizuri uwezo alio nao wa kuongoza kuwakomboa wananchi wa Ilemela kiuchumi kulingana na wakati na mazingira. Kila la heri Angelina Mabula.

Dec 10 Rais wa awamu ya tano Dr.John Pombe Magufuli aliteuwa rasmi baraza la mawaziri, miongoni waliotajwa ni mbunge wa Ilemela Angelina Mabula ambaye aliteuliwa katika nafasi ya naibu waziri wa Ardhi.
Sasa mbunge huyo amefanya exclusive interview na ripota wa millardayo.com baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo ya kuwa naibu waziri…’Kwanza namshukuru Mungu…pili namshukuru Rais wa awamo ya tano kunichagua katika nafasi ya unaibu kwa wana ilemela niseme tu kwamba nawashukuru tu wao kwasababu wasingenipa nafasi ya ubunge nisingefika hapa nilipo kwahiyo ningependa kuwaambia kwamba tupo bega kwa bega’ – Angelina
‘Naomba nikuhakikishia kwamba mimi sio kati ya wale wanaojisahahu kwasababu  dhamana hii niliyopewa ya unaibu waziri ina mikono ya wana ilemela kwahiyo niseme kwamba nitakuwa pamoja maana unapokuwa waziri au naibu waziri kuna vipindi ambavyo vipo unatakiwa kuwa jimboni…sikutarajia nafasi ya kuwa naibu waziri ila kwasababu Mh Rais kuniaminia ndio maana akanipatia hiyo nafasi’ – Angelina Mabul
a
Angelina-Mabula
Angelina Mabula (Mbunge wa Ilemela, Mwanza na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi)
Angelina anatoka katika familia ya wanasiasa. Baba yake alikuwa ni diwani na pia Mkuu wa Wilaya. Angelina anasema: “Historia hii bila shaka imekuwa na ushawishi katika safari yangu ya kisiasa.”
Lakini mafanikio yake bila shaka yaliwezeshwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wake ambao walimtia moyo katika masomo na uwezo wa kujiamini.
Mbali ya historia yake hiyo ambayo ilimpa mwanga wa kisiasa, Angelina anasema: “Nina hulka ya kupenda kufanya kazi na jamii katika ngazi za chini.” Fursa yake ya kwanza kufanya kazi na jamii ilikuwa wakati alipofanya kazi na shirika la misaada la kimataifa Caritas akiwa mhasibu na mratibu wa Jinsia na Maendeleo. Anasema alisukumwa na kuguswa baada ya kushuhudia kiwango cha umaskini katika jamii na kugundua kuwa ni kwa namna gani sehemu ndogo ya msaada wenye ubunifu unavyoweza kuwezesha jamii hizi kujiendesha na kujikwamua.
Ni wakati huo alipoamua kuacha kazi yake ya kitaaluma na kujiunga na siasa mwaka 2000 alipojitosa kuwania nafasi ya udiwani na kushinda. Baadaye alionekana anafaa na kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkuu wa Wilaya.
“Hii ilikuwa fursa muhimu kufanya kazi na watu kwa ukaribu na kusimamia rasilimali zao kwa maendeleo yao,” anasema.
Lakini Angelina hakukaa muda mrefu kwenye nafasi hii, alitaka kuendelea mbele kwenye nafasi za juu za utawala na uamuzi ili kupaza sauti yake na kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya watu. Mwaka 2010 alitaka kuingia bungeni kupitia viti maalumu lakini kwa sababu kadhaa, hakufanikiwa katika azma yake hiyo. Lakini mwaka huu, alijaribu tena bahati yake kupitia siasa za ushindani wa uchaguzi wa kuchaguliwa kupitia jimbo na kufanikiwa kushinda. Pia, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Sababu zilizochangia mafanikio ya Angelina
Haiba binafsi
Kinachoakisi mafanikio yake ni ari yake ya kutaka kuleta mabadiliko katika jamii na kutokukata tamaa. Sifa hii imekuwa kichocheo na wakati mwingine kumwezesha kuvumilia kutukanwa na washindani wake wa kisiasa. Hata hivyo, anasema uungwaji mkono kutoka kwa wanawake wenzake, marafiki na hata watu ambao hakuwajuwa kwa ujumla ulichochea ari yake katika harakati hizi. “Wanawake wenzangu walikuwa nami wakati wote. Wakati mwingine wapinzani wangu waliamua kuwa na mapambano ya kunikashifu binafsi na mbinu nyingine zisizo za kistaarabu,” anasema.
Angelina ni mwanasiasa mwenye haiba ya kipekee na mwenye uhusiano mzuri na watu na sifa hizi zilichangia kufifisha mashambulizi ya kisiasa kutoka kwa washindani wake.
Ukusanyaji wa rasilimali za kampeni
“Kampeni ni gharama sana,” anasema Angelina. Anashauri zichukuliwe hatua za haraka kudhibiti hali hiyo ya gharama vinginevyo itakuwa vigumu kwa wanawake kumudu gharama za kampeni. Kwa kutambua hilo, Angelina alipanga bajeti ya uchaguzi mapema kutoka vyanzo vyake binafsi, marafiki na chama chake ambacho kilimsaidia vifaa vya matangazo. Kwa ujumla, anadokeza kwamba alitumia karibu Sh52 milioni. Kiasi hiki kilimwezesha angalau kukidhi gharama husika na anasisitiza kuwa hakujihusisha na vitendo vya kutoa rushwa kwa wapigakura kama inavyodaiwa kukithiri kwa vitendo hivi kwenye uwanja wa siasa hasa wakati wa uchaguzi. Ujumbe wake kwa wapigakura ulikuwa “Thamani ya kura yako au Sh5,000 kwa miaka mitano ijayo.” Anasema baadhi ya wapigakura walielewa ujumbe wake lakini wengine walimpuuza na kuita timu yake “timu ya lofa.”
 Matokeo ya mafunzo ya FOS Awamu ya Pili
Angelina hakushiriki mafunzo haya moja kwa moja. Wakati mafunzo yanendelea alikuwa ametingwa na maandalizi ya kampeni yake lakini aliamua kumtuma meneja wake wa kampeni ambaye alishiriki kikamilifu kwenye mafunzo hayo. Angelina alihudhuria sehemu ya mafunzo yaliyoandaliwa na Oxfam yaliyoangazia hatua na mchakato baada ya uchaguzi.
Pia, alihudhuria baadhi ya mafunzo yaliyoendeshwa na taasisi ya Hansen Foundation. Kwa Angelina, mafunzo ya kujengewa uwezo kwa wanawake ni muhimu katika kufikia malengo yao.
Stadi muhimu za mafunzo hayo ni kama vile mbinu za kukusanya fedha za kampeni na mbinu za mawasiliano ya umma ikiwamo namna bora ya kushirikiana na vyombo vya habari. Kwenye mafunzo hayo, alijifunza kuongeza mfumo wa mtandao wake wa kumuunga mkono ambao ni muhimu kwa wanawake katika siasa za ushindani.
Changamoto
Anaona utamaduni hasi na mbaya wa matusi na lugha za kudhalilisha wagombea wanawake unaashiria kuwajengea wanawake na vijana kwa ujumla hofu ya kuingia na kushiriki katika siasa za ushindani.
Suala la gharama za kampeni pia ni changamoto kubwa na linahitaji hatua za kulidhibiti. Hatua za uwezeshaji kama elimu ya uraia haipo katika mipango ya muda mrefu na endelevu.
Nini Kifanyike?
Anataka kuwepo usimamizi zaidi wa sheria ambazo zitazuia matendo ya udhalilishaji katika michakato ya uchaguzi na hasa lugha za udhalilishaji ya hadhi na utu wa wagombea. Anashauri pia mipango ya uwezeshaji ilenge kuwa ya muda mrefu na mwisho, vyama vya siasa vibuni vyanzo vya fedha kudhamini wagombea wanawake kwenye siasa za ushindani.
Kuhusu Mradi wa Fahamu Ongea Sikilizwa 
Fahamu Ongea Sikilizwa (FOS) ni mradi wa awamu ya pili kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mradi huu ulitekelezwa katika mikoa kadhaa Tanzania Bara na Zanzibar. Mradi ulikuwa na malengo ya kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wakiwa wapigakura, wagombea na waangalizi wa uchaguzi.
Mradi huu ulifanikiwa kukusanya, kama moja ya majukumu yake, makala hizi ukiwa ni ushuhuda wa baadhi ya wanawake walioamua na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za ubunge, udiwani na urais. Wanawake sita walikubali kuhojiwa na kuelezea uzoefu wao ili jamii kwa ujumla, hususan wanawake, waweze kujifunza na kuhamasika kushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Uzoefu wao kwenye chaguzi hizo pia unatazamiwa kutoa uelewa kwa wadau mbalimbali katika mchakato wa uchaguzi kama vile vyama vya siasa, vyama vya kijamii na taasisi za usimamizi wa uchaguzi ili kuimarisha umuhimu wa kujenga uwanja wa kugombea ulio sawa na mtazamo chanya kuhusiana na umuhimu wa usawa wa jinsia katika uongozi.
Taarifa na maelezo zaidi juu ya ushiriki wa wanawake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 zitapatikana kwenye Ripoti ya Utafiti wa Fahamu Ongea Sikilizwa Awamu ya Pili, itakayochapishwa Januari 2016 na Mradi wa Haki za Jinsia (Gender Justice Programme) ya Oxfam, Tanzania. Ripoti ya utafiti huo itasambazwa kwa wadau waliotekeleza mradi huu, walengwa wa mradi na pia wadau muhimu ambao walishiriki katika utafiti huo. Nakala ya utafiti pia zitawekwa katika mitandao mbalimbali kama vile ukurasa wa Facebook wa Fahamu Ongea Sikilizwa na vyombo vingine vya habari.

No comments:

Post a Comment