Wednesday, February 24, 2016

Tuzo ya pili ya Komla Dumor yatangazwa

Shirika la habari la BBC linamtafuta mwanahabari nyota kutoka Afrika mwenye kipaji cha kipekee atakayetuzwa tuzo ya pili ya Komla Dumor.
Mshindi wa tuzo hii atapata fursa katika shirika la BBC kupata ujuzi wa kazi na kusimulia taarifa kuhusu Afrika kwa dunia nzima kwa kipindi cha miezi mitatu akiwa mjini London.
Mshindi wa kwanza Bi Nancy Kacungira, alisema kuwa anahisi "kuthaminiwa kama mwanahabari mwenye asili ya Afrika na kuwezeshwa kusimulia habari kuhusu Afrika kote duniani kupitia macho ya mwanahabari Mwafrika''.
Maombi ya kushiriki kwenye mashindano hayo yatafungwa tarehe 23 Machi 2016 saa tisa kamili usiku saa za Afrika Mashariki (23:59 GMT).
Shirika la habari la BBC lilizindua tuzo kwa heshima ya aliyekuwa mtangazaji wake Komla Dumor, mwaka wa 2014 baada ya kifo chake akiwa na umri wa miaka 41.
Image captionMshindi wa kwanza Bi Nancy Kacungira
Bi Kacungira, ambaye ni mtangazaji wa runinga ya KTN nchini Kenya alichaguliwa kati ya wanahabari 200 waliotuma maombi.
"Ni jambo la kujivunia kuweza kusimulia habari za bara la Afrika kwenye jukwaa la kimataifa - ripoti zangu zilienea kwenye mitandao ya BBC kwenye runinga ya dunia na pia kwenye redio,'' alisimulia tajriba yake.
''Mtazamo wangu wa kuweza kusimulia yanayotokea katika bara la Afrika pasi na kuegemea upande wowote kwa uadilifu na kwa haki uliwiana vyema na sera na kanuni za shirika la habari la BBC zinazomhitaji mwandishi asiegemee upande wowote popote alipo duniani,'' aliongezea bi Kacungira.
Naibu mkurugenzi wa habari katika shirika la habari la BBC Fran Unsworth alimmiminia sifa Komla.
"Komla Dumor alikuwa mwandishi na mtangazaji mwenye kipaji cha kipekee. Alisifika sio Ghana pekee bali kote barani Afrika na duniani.''
"Weledi wake wa kuelezea habari za Afrika kwa kujitolea uliwashawishi wengi kuiga mfano wake na hivyo akaibuka kupendwa sio tu na waandishi wenzake bali kote barani Afrika.''
''BBC imejitolea kuendeleza kazi aliyoianza Komla na hivyo kwa mwaka wa pili mfululizo tunamtafuta mwanahabari mwenye kipaji kama chake na mwenye kujitolea kama Komla.''
Image captionKomla Dumor
Komla Dumor alikuwa mwandishi na mtangazaji mwenye kipaji cha kipekee kutoka nchini Ghana.
Alisimulia bara la Afrika kama bara lenye kujiamini na lenye wajasiriamali wengi, sio tu bara linalozongwa na matatizo chungu nzima.
Kupitia kwa kazi yake ya uandishi na kusimulia taarifa kwa wengi, Komla alifanya kazi kwa kujitolea sana kutoa taswira tofauti kuhusu Afrika kwa dunia nzima.
BBC imejitolea kuendeleza kazi aliyoianza Komla.
Kwa maelezo zaidi na jinsi ya kushiriki tembeleabbc.com/komladumor

No comments:

Post a Comment