Sunday, February 21, 2016

‘Wenye migogoro ya ardhi kuweni watulivu’................

‘Wenye migogoro ya ardhi kuweni watulivu’


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula. 
By Aidan Mhando, Mwananchi amhando@mwananchi.co.tz
Sengerema. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amewataka wakazi wa wilaya za Magu na Sengerema ambao wana migogoro ya ardhi na wawekezaji kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kuitatua kwa kufuata sheria.
Akizungumza katika mkutano mkoani Mwanza juzi, Mabula alisema anatambua kuna watu wamekuwa wakiwakandamiza wananchi kwa kupora maeneo yao.
Alisema Serikali ipo macho na haitakubali kuona wananchi wakionewa.
“Nawaagiza wakuu wa wilaya kuzungumza na watumishi wa ardhi kukutana na wananchi wenye migogoro ya ardhi na kero hizo zimalizwe mara moja,” alisema Mabula na kuongeza:
“Ile migogoro ya ardhi ambayo ipo mahakamani naomba tuiachie Mahakama ifanye kazi yake na hapo itakapomalizika, tutatekeleza uamuzi wake.”
Aliwataka wananchi wasifanye fujo kwa kuwa vyombo vya sheria vipo na vitafanya kazi yake.
Baadhi ya wakazi wa wilaya za Magu na Sengerema waliokuwa katika mkutano huo, walimueleza hali za migogoro ya ardhi katika wilaya zao.
Wananchi hao waliwatuhumu wakuu wa wilaya hizo kushindwa kusimamia masuala ya ardhi na kumuomba kuingilia kati migogoro iliyopo kwenye maeneo yao.
Mkazi wa Kijiji cha Ihayabuyaga, Wilaya ya Magu, Paulo Mathayo alisema katika kijiji chao kuna wawekezaji wanaoingia mikataba na wananchi lakini huwa hawatekelezi mambo wanayokubaliana.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Zainabu Terack alisema Serikali ipo kwa ajili ya wananchi na itahakikisha inatafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi ambayo ipo katika wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment