Saturday, July 18, 2015

Maneno ya Makamba kuhusu Kingunge, Udiwani na Ubunge CCM Arusha kisa ni Lowassa?

Maneno ya Makamba kuhusu Kingunge, Udiwani na Ubunge CCM Arusha kisa ni Lowassa?


Today
MWANANCHI
Naibu Waziri January Makamba amemtolea uvivu mshauri wa zamani wa Siasa wa Rais Jakaya Kikwete, Kingunge Ngombale-Mwiru kwa kuupinga mchakato wa uteuzi wa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM na kusema anakivuruga chama.
Kingunge kumpigania mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amekuwa akitoa matamko mbalimbali kuhusiana na mchakato huo akisema haukutenda haki hasa baada ya kuenguliwa jina la Lowassa ambapo baada ya mchujo wa majina likapatikana jina la mgombea mmoja, Dk John Magufuli.
Mzee Kingunge ni mtu mzima, ninamuheshimu sana, ni mkongwe katika siasa, lakini anakivuruga chama… Ndani ya chama kuna wazee wenye busara ambao waliangalia vitu vingi hadi kumteua mgombea kwani unaweza kuwa mtendaji mzuri lakini ukawa na kasoro nyingi hivyo, unaweza vilevile kuonekana ukashindwa kukivusha chama kwenye ushindi”—January Makamba.
Mimi ninamuheshimu sana Mzee Kingunge, lakini siwezi kukubaliana naye anavyokandia mchakato. Mimi ninaamini ulikuwa sahihi, kila mtu ameridhika na ndiyo maana kura zilipigwa”—January Makamba.
Katibu Mkuu Mstaafu wa chama hicho, Mzee Yusuph Makamba alisema kwamba watu wanaoendelea kulalamikia mchakato wa kumpata mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, wana masilahi binafsi na siyo kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho.
Mwanzoni mwa wiki, Katibu huyo wa zamani wa halmashauri kuu ya CCM Mzee Kingunge alisema Kamati ya Usalama na Maadili iliteka majukumu ya Kamati Kuu baada ya kuamua kuchuja majina ya makada waliojitokeza kuwania urais hadi kufikia watano, akisema jitihada hizo zilifanywa kwa kuvunja kanuni na zililenga kumuengua Lowassa kuwania kuingia Ikulu.
MWANANCHI
 Wazee wa Kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai (Malaigwanan) kutoka Wilaya ya Monduli wamemuomba Mbunge Edward Lowassa kubaki na kuendelea kuwa kada wa CCM kwa sababu ndicho kilichomlea na anakijua.
Sote Monduli tumesononeka kwa jinsi vikao vya chama vilivyomtendea mbunge wetu. Bado tunampenda kama ambavyo tunakipenda chama chetu. Tunaamini ataendelea kubaki CCM na kupigania ushindi wa chama katika uchaguzi ujao,”– alisema Mzee  Mesopiro mwakilishi wa wazee hao.
Mzee mwingine Julius Laizer kutoka Kata ya Moita, alisema licha ya mizengwe iliyotawala vikao vya uteuzi vya CCM vilivyomalizika mjini Dodoma bado anaamini chama hicho kitaendelea kubaki imara hata kama baadhi ya watu watakihama.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Lepurko wilayani Monduli, Njoput Alami alibeza taarifa za kushawishi watu kuhama CCM kwa kisingizio Lowassa kukatwa akiziita ni kelele za wapambe wanaohofia kukosa fursa walizozitarajia iwapo Lowassa angeteuliwa kuwa mgombea wa CCM.
Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro alikiri baadhi ya wanachama kuchana kadi na kuchoma bendera za chama hicho, lakini akasema ni idadi ndogo ikilinganishwa na wanachama waliopo wilayani humo.
Kuna taarifa za kadi na bendera za CCM kuchomwa moto katika baadhi ya maeneo kama Migungani, Mto wa Mbu, Makuyuni na Nalaarani. Tunaendelea kukusanya taarifa sahihi na kufanya tathmini ya matukio hayo,”– Elisante Kimaro.
NIPASHE
Kufuatia kusuasua kwa uchukuaji fomu za Udiwani na Ubunge jimbo la Monduli, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro amesema kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa kililazimika kuketi jana kutafuta ufumbuzi.
Katika hali inayoonyesha kupata kigugumizi, Kimaro alikataa kuyataja mambo ambayo walikaa kwa ajili ya kujadili akisema hayapaswi kutangazwa.
Tumekutana na kujadili mambo mengi kwa kina, tumefikia muafaka lakini yapo mambo ambayo bado yanahitaji utekelezaji, haya ni mambo ya ndani tunayafanyia utekelezaji,”– Elisante Kimaro.
Hata hivyo, alisema wajumbe wote 16 wa kamati hiyo wamekubaliana kuendelea kuwahamasisha Wanachama kuchukua fomu za kugombea nafasi za Udiwani na Ubunge kabla ya Julai 19, mwaka huu siku ambayo ni ya mwisho kuchukua fomu na kuzirejesha.
Katibu huyo alisema kumekuwa na kasi ndogo ya wanachama kuomba nafasi za Udiwani na Ubunge hali ambayo inatokana na kusuasua kwa wanachama hao baada ya kukatwa kwa jina la Mbunge Edward Lowassa katika kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM

No comments:

Post a Comment