Saturday, July 11, 2015

Baadhi ya kazi za zitto Bunge.

Baadhi ya kazi za Zitto Bungeni
Kwa uzito na mahala unapofanyika mkutano huu, naomba
niwaletee kwa muhtasari kabisa baadhi ya kazi ambazo
Ndugu Zitto Kabwe amezifanya katika kusukuma mbele
guruduma la maendeleo katika nchi yetu.
1. MABADILIKO SEKTA YA MADINI
Zitto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge
mwaka 2005 akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini
ambalo halina mgodi hata mmoja wa madini ukiachana na
wachimbaji wadogo wa udongo wa Pemba ambao una
soko kubwa hapa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo
ajenda inayomtambulisha Zitto Kabwe kwa Taifa ni ajenda
ya mabadiliko makubwa aliyoanzisha katika sekta ya
Madini nyakati ambayo hakuna mwanasiasa aliyethubutu
kukosoa sera za uwekezaji kwa namna aliyofanya. Baada
ya kudokezwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini
Bwana Nazir Karamagi amesaini mkataba mpya wa Madini
akiwa hotelini nchini Uingereza, Zitto alimtaka Waziri
kujieleza ndani ya Bunge kuhusu mkataba huo na masharti
yake ya kikodi. Waziri huyo aliposhindwa Zitto aliwasilisha
Hoja Binafsi Bungeni (akiwa mbunge wa kwanza kufanya
hivyo katika Bunge la Tisa na la Nane kwa pamoja). Hoja
ya Buzwagi ilisababisha Zitto kusimamishwa ubunge kwa
miezi 4. Hata hivyo mnamo Septemba 10, 2007 alitangaza
Azimio la Songea lililomshinikiza Rais Jakaya Kikwete
kuunda Kamati ya Bomani ili kupitia mikataba yote ya
Madini nchini.
Kutokana na kazi yake hiyo leo Tanzania ina Sera mpya ya
Madini na Sheria mpya ya Madini ambayo imeboresha
nafasi ya Tanzania kufaidika na Madini, imeruhusu kisheria
Serikali kuwa na hisa kwenye migodi ( na hivi
tunavyoongea, kwa mfano, sasa Serikali inamiliki 50% ya
Mgodi wa TanzaniteOne). Makampuni ya Madini ambayo
yalikuwa yanatangaza hasara kila mwaka leo yanalipa kodi
ya Mapato na Halmashauri zenye migodi zinalipwa ushuru
wa huduma wa mabilioni ya fedha. Huyu ndiyo Kiongozi
wetu wa ACT Wazalendo. Hawa ndio Viongozi Taifa hili
linawataka. Viongozi wanaotenda na kutoa majawabu ya
changamoto za nchi. Sio Viongozi wanaolaumu tu eti
wakisubiri kushika dola ndio watende. Nani anayebisha
rekodi hii?
2. KUZUIA UBINAFSISHAJI WA SHIRIKA LA BIMA LA
TAIFA (NIC)
Zitto Kabwe alikuwa Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi
mwaka 2006 wakati Shirika la Bima la Taifa likiwa kwenye
mchakato wa Ubinafsishaji. Wafanyakazi wa TUICO Tawi
la Bima walimfuata wakielezea kwa ushahidi namna mali
za Shirika zilivyopangwa kuuzwa na wajanja wachache
kutaka kujiuzia Shirika na Mali zake hasa jengo la kitega
uchumi kwa bei ya kutupwa. Zitto aliwakilisha hoja hiyo
kwenye Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya
Mwenyekiti wake Ndugu Abdallah Kigoda na kuishawishi
Kamati kukataa ubinafsishaji wa NIC na badala yake
kuunda kikosi kazi cha kurekebisha Shirika na liendelee
kuwa Mali ya Umma.
Mwezi Novemba Mwaka 2006 Baraza la Mawaziri
lilikubaliana na hoja za Zitto alizotoa kwenye Kamati ya
Bunge na ndani ya Bunge na kuamua kuliondoa Shirika
kwenye mchakato wa ubinafsishaji na leo hii Shirika
limebaki kuwa la Umma na limeanza kurudi kwenye hali
yake. Aliendelea kulisaidia Shirika la Bima kwa kuagiza
(akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali ) kuwa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma
yaweke Bima kupitia Shirika la Bima la Taifa na agizo hilo
kutekelezwa na Mashirika mengi ikiwemo Benki Kuu ya
Tanzania.
Sio Bima tu, Zitto akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Mashirika ya Umma aliagiza kuondolewa
katika orodha ya ubinafsishaji Shirika la STAMICO ili liweze
kushiriki kikamilifu katika sekta ya Madini na liliondolewa.
Huo ndio Ujamaa wa kidemokrasia ambao Chama chetu
cha ACT-Wazalendo kinautangaza, na huyo ndio Kiongozi
wetu ambaye ana uzalendo wa dhati kwa mali za
Watanzania. Nani anayebisha rekodi hii?
3. SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Mwaka 2008/2009 Zitto Kabwe aliweka rekodi nyingine ya
kuwa Mbunge wa kwanza kuzungumzia mabadiliko ya
sheria ya viongozi wa umma ili kuipa meno secretariat ya
maadili ya viongozi na kutengenisha biashara na siasa.
Alipeleka Bungeni Muswada Binafsi wa Sheria ili kufanya
mabadiliko makubwa ya Sheria Maadili. Hata hivyo
muswada ule ulizuiwa na Serikali kuingia Bungeni licha ya
kukamilisha kila hatua iliyopaswa.
Leo hii Chama chetu kinazungumzia kurejesha Miiko ya
Viongozi kuna watu wanadhani Zitto kaanza haya hivi
sasa, la hasha. Huu ni mwendelezo wa yale aliyokuwa
anaamini miaka kadhaa iliyopita na kwa kuwa yeye
anapenda kutembea anayoyasema alitushawishi wenzake
kufanya Miiko ya Viongozi kuwa sehemu ya Katiba ya
Chama chetu. Yeye ni Kiongozi wa kwanza wa kisiasa
kuweka hadharani Mali na Madeni yake hapa nchini. ACT
Wazalendo ni chama pekee cha siasa hapa nchini
ambacho Viongozi wake wanatakiwa kikatiba kutangaza
Mali zao, Madeni yao na Maslahi yao ya kibishara. Nani
anabisha rekodi hii?
4. UKAGUZI WA MAHESABU WA VYAMA VYA SIASA
Katika kuhakikisha kuwa kila senti ya fedha ya umma
inakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya
Serikali, Ndugu Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni
mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria namba 5
ya Mwaka 1992 na kuwezesha CAG kukagua fedha za
vyama ambazo zinatoka Serikalini kama ruzuku. Sheria ya
Vyama vya siasa inataka kila Mwaka Serikali kutenga
kiwango kisichozidi asilimia mbili (2%) ya Bajeti ya Serikali
kama ruzuku kwa vyama vya siasa. Vyama hupewa
wastani wa Shilingi bilioni 20 kila mwaka na kugawana
miongoni mwao lakini fedha hizi zilikuwa hazikaguliwi
kinyume na Sheria za Fedha.
Baada ya Sheria hiyo kupitishwa na Bunge mwaka 2009,
Zitto alisimama kidete kuhakikisha inatekelezwa jambo
ambalo lilimletea uhasama mkubwa sana na viongozi
wenzake katika chama chake cha zamani akiwa Naibu
Katibu Mkuu. Zitto alipigana kwa kushirikiana na
Wazalendo wenzake katika Kamati ya Bunge ya PAC na
kufanikiwa na hivi sasa vyama vyote vinakaguliwa na
kuweka rekodi nyingine katika nchi nyingi za Afrika. Kwa
kazi hii iliyotukuka Zitto Kabwe amedhibiti fedha za umma
kwa vyama vya siasa na hivi sasa taarifa za mahesabu ya
vyama ipo wazi, na tumeona vyama vyote vikiwa na hati
chafu, vikiwemo vyama vya upinzani vya zamani. Ni wajibu
wa wanachama wa vyama hivyo kuwawajibisha viongozi
wao wanaogeuza fedha za ruzuku kuwa ni fedha zao
binafsi. Nani anabishia rekodi hiyo ya Kiongozi wetu?
5. KUFUFUA ZAO LA MKONGE
Mwaka 2012 Zitto Kabwe aliweka rekodi nyingine tena
akiwa mbunge wa kwanza katika Bunge la 10 kuwasilisha
Hoja Binafsi. Aliwasilisha Hoja Binafsini Bungeni akitaka
Serikali kufufua Kilimo cha Mkonge kwa kuwanyanganya
wawekezaji wakubwa mashamba waliyobinafsishiwa na
kuyaacha bila kulimwa na badala yake mashamba yale
wapewe wakulima wadogo. Zitto alitaka kubadilisha
mfumo wa kulima Mkonge kutoka mashamba makubwa
yanayomilikiwa na tajiri mmoja na kulimwa na manamba
mamia na kwenda kwenye mfumo ambao wakulima
wadogo wadogo wanalima Mkonge na hivyo kushirikisha
wananchi wengi zaidi kwenye uchumi wao.
Hoja hiyo ilipingwa na Wabunge kutoka Tanga lakini
iliungwa mkono sana na wananchi wa mkoa huo na hivyo
kumwona Zitto kama mwakilishi wao licha ya kwamba
alikuwa akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Katika Chama chetu ajenda ya kumilikisha Ardhi wananchi
ni ajenda kubwa na ACT Wazalendo kimekua chama cha
kwanza nchini kutangaza kinagaubaga kuwa kitazuia
uporaji wa Ardhi na kumilikisha wananchi ardhi yao
wenyewe. Nani anabishia rekodi hiyo?
6. KURASMISHA KAZI ZA SANAA NA BURUDANI
NCHINI
Kwa muda mrefu sana wadau wa tasnia ya sanaa na
burudani nchini walikuwa wanalalamika kazi zao kutokuwa
rasmi na hivyo kuibiwa na mchango wao katika uchumi
kutotambuliwa. Mwaka 2012 Zitto Kabwe akiwa Waziri
Kivuli wa Fedha alifanya kampeni maalumu ya kuhakikisha
kuwa wasanii hawanyonywi na kazi zao kutambuliwa
rasmi. Aliwasilisha Bungeni mabadiliko ya Sheria ya
Ushuru bidhaa ili kutambua rasmi kazi za sanaa na
burudani na kuhakikisha kuwa wasanii wanalipwa
wanavyostahili katika biashara ya miito ya simu.
Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge na Mamlaka ya Mapato
Tanzania ikaanza kutoa stempu rasmi katika CDs za kazi
za sanaa ili kudhibiti wazalishaji kuwanyonya wasanii.
Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015
tasnia ya Sanaa na Burudani imekuwa sekta rasmi ya
Uchumi na imeripotiwa kuwa sasa ina thamani ya shilingi
270 bilioni kama mchango wake katika Pato la Taifa. Hivi
sasa Wasanii wanafaidika maradufu kwa kazi zao kuuzwa
kama miito ya simu na wengine wanapata mamilioni ya
shilingi na kuboresha maisha yao kwa jasho lao. Nani
anabisha rekodi hii?
7. KUDHIBITI UKWEPAJI KODI NA MISAMAHA YA
KODI
Wawekezaji kutoka nje wamekuwa wakiibia nchi yetu kwa
kubadilisha badilisha majina ya makampuni yao na kubadili
wamiliki bila ya kulipa kodi hapa nchini. Watanzania
mnakumbuka jinsi majina ya mahoteli makubwa
yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka Sheraton
kwenda Moevenpick na kwenda Serena sasa. Makampuni
ya Simu yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka
Mobitel kwenda Buzz kwenda Tigo.
Vile vile kutoka Celtel kwenda Zain na kwenda Airtel. Haya
yamekuwa yakitokea kwenye maeneo mengi zaidi ya haya.
Yote haya yalitokea bila ya Serikali kupata kodi yeyote.
Kwenye mauzo ya Zain kwenda Airtel Serikali ilipoteza dola
za Kimarekani 312 milioni ( zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa
bei za sasa za dola ). Kwa uchungu kwa nchi yake Zitto
Kabwe aliwasilisha Bungeni muswada wa sheria wa
kurekebisha sheria ya kodi ya Mapato na kuanzisha tena
kodi ya ongezeko la mtaji ( Capital Gains Tax ).
Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge kupitia Sheria ya
Fedha ya mwaka 2012 na mwaka huo huo Tanzania ilipata
mapato ya shilingi bilioni 50 kwa mauzo ya Kampuni ya BP
kwenda PUMA. Mwaka 2014 Tanzania ilipata dola za
kimarekani 222 milioni ( zaidi ya tshs 450 bilioni )kwa
mauzo ya sehemu ya vitalu vya gesi asilia vya kampuni ya
Ophir kwenda kampuni ya Pavilion ya Singapore.
Zaidi ya hapo Zitto na wazalendo wenzake katika Kamati
ya PAC walitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa Misamaha ya
kodi yote inakaguliwa na ukaguzi wake kuwekwa wazi ili
kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania CAG
anakagua misahamaha ya kodi na PAC iliweka wazi taarifa
ya kwanza ya ukaguzi wa misamaha ya kodi. Nani
anabishia rekodi hizi?
8. MABILIONI YA USWISS
Mwaka 2012 mwezi Novemba Zitto Kabwe aliwasilisha
Bungeni Hoja Binafsi kuhusu mabilioni ya Uswisi ikiwa na
lengo la kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu Watanzania
wanaoficha fedha nje ya nchi kinyume cha sheria. Bunge
lilipitisha hoja hii binafsi na kuitaka Serikali kufanya
uchunguzi kuhusu Watanzania wanaotorosha fedha
kwenda nje na kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Tanzania iliingia katika rekodi ya kuwa nchi ya kwanza
katika nchi za Jumuiya ya SADC kupitisha Azimio la Bunge
kuhusu suala la utoroshaji wa fedha. Licha ya kwamba
Serikali haijatoa taarifa yake miaka miwili sasa toka Azimio
la Bunge namba 9 la mwaka 2012, na baada ya danadana
ya muda mrefu kutoka vyombo vinavyohusika Kiongozi
wetu Zitto Kabwe ameamua leo kupasua jipu la hoja hiyo
kwa kuweka wazi orodha ya kwanza ya Watanzania 99
wenye akaunti katika Benki ya HSBC ya Uswiss. Uongozi ni
umakini, na sio kukurupuka na kujitafutia sifa za
harakaharaka. Ilikuwa ni muhimu Ndugu Kabwe kufuata
taratibu zote kabla ya kuanika majina hayo hadharani. Sasa
leo baada ya kujiridhisha pasipo shaka atayaanika majina
hayo hadharani na wale waliokuwa wanambeza kwamba
kashindwa wanyamaze milele! Huyo ndio Zitto, mwenye
uvumilivu na ujasiri usio kifani. Anatenda anayosema. Nani
anabisha rekodi hii?
9. KUWAJIBISHA MAWAZIRI
Katika historia ya Tanzania ni Wabunge wawili tu
walioweza kutoa hoja zilizopelekea Mawaziri wengi
kuondolewa madarakani kwa mpigo. Ni Zitto Kabwe na
Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye aliongoza kamati teule
ya Bunge iliyochunguza Mkataba wa kampuni feki ya kufua
umeme ya Richmond. Hoja hii ilipelekea Waziri Mkuu
kuwajibika kwa kujiuzulu na hivyo kumlazimisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano kuunda upya Serikali kwa kuteua
Waziri Mkuu mwingine.
Zitto ana rekodi ya kipekee. Kwanza mwaka 2012 baada ya
Taarifa ya CAG kuonyesha madudu katika matumizi ya
fedha za umma, Zitto alikusanya sahihi za wabunge 75 na
kuandika hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Shinikizo hili lilipelekea Rais kufukuza kazi mawaziri 8
ambao Wizara zao zilitajwa kuwa na mahesabu machafu.
Pili mwaka 2013 baada ya Kamati ya Mali Asili na
Mazingira kutoa taarifa yake Bungeni kuhusu Operesheni
Tokomeza, Zitto alisimama ndani ya Bunge na kubadilisha
mjadala kwa kutaka Mawaziri wote ambao watendaji wao
walitesa wananchi kuwajibika. Mawaziri 4 waliwajibika.
Tatu, mwaka 2014 katika Taarifa Maalumu ya Kamati ya
PAC kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow
ya Benki ya Tanzania, Zitto na wazalendo wenzake wa
kamati hiyo walipelekea Mawaziri wawili maarufu kama
mawaziri wa Escrow na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kuwajibika. Uwajibikaji umekuwa ni ajenda kubwa ya
Kiongozi wetu na amekuwa hana aibu hata kwa watu
anaowaheshimu na rafiki zake. Alitaka wawajibike huku
akiwatazama usoni. Ni Viongozi wachache sana wenye
ujasiri wa aina hii. Huyu ndio Kiongozi wa chama chetu
cha ACT Wazalendo. Nani anabisha rekodi hii?
10. KUKATAA POSHO ZA KUKAA
Mwaka 2010 chama chake cha zamani waliweka katika
Ilani yao ya Uchaguzi kupinga posho kama hatua ya
kubana matumizi ya Serikali. Wakakubaliana kuwa
wabunge wa chama chao hawatapokea posho ya kukaa
(sitting allowance). Hata hivyo, ilipokuja katika utekelezaji
wenzake wote wakagwaya na Ndugu Zitto Kabwe ni
mbunge pekee aliyepinga posho za vikao na kuzikataa kata
kata kwa miaka mitano (5) mfululizo, ambazo ni takribani
shilingi milioni 21 kila mwaka. Katika kipindi hicho cha
miaka mitano Zitto alikaa kuchukua jumla ya Shilingi
Milioni Mia Moja na Tano (105,000,000)!! Kukataa pesa
yote hii kwa sababu ya ‘principle’ tu ni jambo nadra sana
kutokea katika mazingira yetu. Zitto anatembea maneno
yake. Zitto anatenda anayonena. Sasa kwa yote hata kwa
nini wasimchukie wenye roho zao za kwa nini?
Ndugu Wananchi,
Huyu ndio Kiongozi wa Chama chetu. Tunachoomba
Watanzania mumhukumu Zitto kwa rekodi zake na si kwa
propaganda za mahasimu wake.

No comments:

Post a Comment