Thursday, July 9, 2015

Kisu cha Ccm kuchinja 33Leo

kikali cha Kamati Kuu ya CCM (CC) leo kitaondoka na
vichwa 33 kati ya 38 vya walioomba kuteuliwa
kupeperusha bendera ya chama hicho kumrithi Rais
Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Ndugu Philip
Mangula.
Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika kwa kikao
cha Kamati ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huku kikitawaliwa na
usiri mkubwa, kuhama ukumbi na kila dalili za kubadili
ratiba iliyopangwa awali ili kuvuruga mipango ya kambi za
wagombea.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kulikuwa na
uwezekano wa kubadili ratiba ili vikao vya Kamati ya
Maadili na CC ama vifuatane au vifanyike usiku ili
kuyanyima makundi nafasi ya kujipanga.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Alipoulizwa jana kuhusu vikao hivyo, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alidai kuwa hata yeye
hakuwa na uhakika wa lini na muda gani hasa kikao cha
Kamati ya Maadili kingefanyika.
Awali, vifaa vya ukaguzi wa wajumbe vilikuwa vimewekwa
katika Makao Makuu ya CCM, White House lakini baadaye
jioni viliondolewa na hapakuwa na taarifa zozote
zilizotolewa.
Habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kikao hicho cha
Maadili kilitarajiwa kufanyika Ikulu ya Dodoma kuanzia saa
nne usiku wa jana.
Haya yanajitokeza wakati macho na masikio ya Watanzania
yakiwa hapa Dodoma kusikiliza namna kazi ya kuchuja
wagombea itakavyofanyika na kujua ni watu gani 33
watakaoanza kulambwa na kisu cha CC, hasa kwa majina
makubwa yanayotazamwa na wengi, mara tu baada ya
kujadiliwa na Kamati ya Maadili.
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana.
Kazi za Kamati Kuu leo
Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni
kufikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC), majina yasiyozidi matatu ya walioona kuwania
urais wa Zanzibar ambayo imeombwa na Rais wa sasa, Dk
Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa mapendekezo
kwa NEC majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania
urais wa Muungano na kuandaa mkutano wa NEC.
Vigezo vya maadili
Kulingana na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo la 2012
kifungu cha 4(ii), kuhusu taratibu za kuomba uongozi,
wanachama wanaogombea uongozi ambao uteuzi wao
hufanywa na vikao vya kitaifa, watachunguzwa kwanza
uadilifu wao na chombo cha maadili cha CCM kwa
ushirikiano na vyanzo vingine.
Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba
uongozi katika ngazi yoyote, itikadi na mwenendo wake
vitachunguzwa kwanza na Kamati ya Usalama na Maadili
inayohusika, ndipo maombi hayo yaliyoambatanishwa na
mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele ya
kikao chenye madaraka ya kutoa uamuzi.
Ikiwa mwanachama hakupendekezwa kwa sababu ya
kukiuka Katiba ya CCM, Kanuni za CCM na sheria ya nchi,
hatakuwa na haki ya kukata rufaa kwa mtu yeyote au kikao
chochote. Lakini ikiwa mwanachama atakataliwa
kugombea kwa sababu ya madhambi yake katika chama,
basi ni wajibu wa Kamati ya Usalama na Maadili
kumjulisha makosa yaliyomnyima haki ya kugombea, naye
anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa haki zake kikatiba.
Mtu yeyote anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya Usalama
na Maadili ya ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana
na maadili au nidhamu ya chama atasomewa na kutakiwa
kuzijibu tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo
ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi, lakini
hataambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama
imekwishajulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao,
vyombo vya sheria au vyombo vya habari.
Kanuni ya maadili inaendelea kusema kuwa uchambuzi wa
tuhuma hizo utafanywa kwa kutumia njia mbalimbali
pamoja na mashahidi watakaopatikana.
Uchunguzi utakapokamilika na endapo itadhihirika
kwamba tuhuma zina uzito, mtuhumiwa ataitwa mbele ya
kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi
inayohusika, kama ni lazima, ili apate kuhojiwa ana kwa
ana.
Pia, kanuni inasema Kamati ya Usalama na Maadili ya
ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu suala
hilo kwenye kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa
atapewa nakala ya uamuzi kwa maandishi.
Wagombea wanne kukosa CC
Katika kikao cha CC kinachofanyika leo, wajumbe wanne
ambao ni miongoni mwa majina 38 yatakayojadiliwa katika
mchujo huo watalazimika kukaa kando ili kukwepa
mgongano wa masilahi.
Wajumbe hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa
Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Makamu wa Rais,
Dk Mohamed Ghalib Bilal na Waziri wa Kilimo na Chakula,
Stephen Wasira.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM
katika Vyombo vya Dola, Toleo la Pili – Februari, 2005,
ukurasa wa 25, kifungu cha 21 (3); wajumbe wa vikao vya
uchujaji na uteuzi wa wagombea kwa ngazi inayohusika
hawaruhusiwi kuendelea na kazi ya uchujaji na uteuzi
iwapo wao ni wagombea katika ngazi hiyo.
Kanuni hiyo pia imetoa miiko ya shughuli za uchujaji na
uteuzi wa wagombea na wajumbe wote wanatakiwa na
kanuni kuzingatia maadili na nidhamu ya chama katika
kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi.
Kanuni hizo zinasema ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa
maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata
kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya mwingine, kutumia
au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo
analoishi au anakotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Pia, ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa
nafasi ya uongozi au mwanachama yeyote aliyekabidhiwa
dhamana ya usimamizi au uangalizi au uratibu wa kura za
maoni, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo vya ukiukwaji wa
kanuni.
Kuhusu misaada, kifungu cha tano (a) kinasema ni
marufuku kwa mgombea yeyote mtarajiwa au wakala
wake, kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri
kuwa ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi
anayoitafuta kabla ya muda rasmi wa uongozi unaohusika
haujamalizika.
Kanuni imetoa adhabu kwa watakaovunja miiko hiyo na
kwa kiongozi atakayethibitika kuivunja atavuliwa uongozi
na kwa mwanachama anayeomba kugombea nafasi yoyote
atakayethibitika kuivunja hiyo hatateuliwa kugombea nafasi
anayowania.

No comments:

Post a Comment