Thursday, July 9, 2015

Mani atakaye beba kirungu cha Jakaya?

Nani atakaye mrithi Kikwete katika
CCM?
Wiki hii maskio yote ya
Watanzania yanaelekezwa mjini
Dodoma, mji mkuu wa Tanzania
ambapo chama tawala nchini
humo Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kinamchagua mtu mmoja
atakayepeperusha bendera ya
chama hicho katika uchaguzi
mkuu wa wabunge na rais
unaotarajiwa kufanyika tarehe 25
Oktoba 2015.
Vikao vya mchakato huo vinaanza
rasmi Jumatano huku
vikitanguliwa na kikao cha Kamati
ya Ulinzi na Usalama ambayo
kimsingi pamoja na mambo
mengine kitapitia wasifu wa watia
nia wote lakini pasipo kupunguza
jina lolote.
Siku ya Alhamisi (09 Julai),
Kamati Kuu ya chama yenye
wanachama takribani 32 itakutana
na hapo ndipo upungazaji wa
majina utafanyika hadi kufikia
majina matano tu.
Baada ya hapo, Halmashauri kuu
ya chama itakutana siku ya
Ijumaa tarehe 10 Julai ambapo
itachuja majina hayo matano hadi
kufikia matatu kupitia mtindo wa
kupiga kura. Majina haya matatu
ndiyo yatakayokwenda katika
Mkutano Mkuu wa Chama ambao
ndio utakaochagua jina moja la
huyo mgombea urais kwa tiketi ya
chama
Mkutano Mkuu huu unajumisha
takribani wanachama 2100 ikiwa
ni pamoja na Wabunge wa CCM
Tanzania bara na wawakilishi
wengine kutoka Zanzibar lakini
pia wawakilishi wa chama kutoka
ngazi mbalimbali hadi zile za
chini.
Mkutano huu umepangwa
kufanyika tarehe 11 hadi 12 Julai
Uteuzi waibua hisia Tanzania
Wakati watu wakingojea kwa
hamu ni nani atapenya katika
mchujo huo na kuibuka kidedea,
tangu mwanzo wa zoezi zima la
kutafuta nafasi hiyo kwa
wanachama wa CCM kumeibua
hisia kubwa na za tofauti
miongoni mwa Watanzania.
Kwa mara ya kwanza katika
historia ya CCM na nchi kwa
ujumla, idadi ya wanachama
waliojitokeza kuchukua fomu na
kusaka ridhaa ya kuteuliwa kuwa
mgombea urais wa chama hicho
ilifikia 42.
Idadi hii ilijumuisha makada
kutoka kila aina ya haiba.
Walikuwemo waliokuwa mawaziri
wakuu wa zamani, maofisa wa
ukachero wastaafu na hata
mwanachama mmoja ambaye
elimu yake inasemekana kuwa ni
ya shule ya msingi tu. Hata hivyo
orodha hii ilisheheni jinsia ya
kiume zaidi huku idadi ya
wanawake waliojitokeza kuchukua
fomu ikiwa ni wane tu.
Mchakato huu wa CCM kuelekea
uteuzi wa mgombea wao wa urais
ni wa muhimu sana kwa chama
hicho na unafuatiliwa kwa karibu
sana na wapenzi lakini hata
wapinzani wa chama hicho kwa
sababu mwisho wake unatarajiwa
kutoa picha ya mwelekeo wa
chama hicho kikongwe nchini.
Umuhimu wa mchakato
Kwa mfano, huu ndio msimu wa
kwanza ambapo chama hicho
kitamteua mgombea urais pasipo
baraka za moja kwa moja za
mwasisi wa chama hicho na taifa
kwa ujumla Mwalimu Julius
Nyerere.
Hata kama vyombo husika vya
uchaguzi na utaratibu mzima wa
kumpata mgombea umekuwepo
tangu kitambo, Mwalimu Nyerere
alifanyika mshawishi mkubwa
katika kuwapata wagombea hasa
wa nafasi nyeti kama ya urais wa
nchi ambao hatimaye kweli
walipata kuwa marais.
Kwa upande mwingine baadhi ya
wanaosaka kuteuliwa kuwa
wagombea wa chama chama
hicho wamehusishwa na kashfa
kadhaa za matumizi mabaya ya
madaraka na rushwa
vilivyoisababishia serikali hasara
kubwa na kuzua mjadala mzito
miongoni mwa Watanzania
CCM inaonekana kuwa na kazi
ngumu ya kuwahakikishia
wanachama wake lakini pia
wapinzani wake kwamba ina
uwezo wa kumuweka kando
mtuhumiwa yeyote kwa usalama
wa chama. Kwamaneno mengine,
kuthibitisha kwamba chama
ndicho kinachotangulia halafu
mgombea anafuata.
Lakini wakati CCM inapiga hesabu
ya kuruka kihunzi hicho, bila
shaka inapiga hesabu nyingine
pia ya namna gani itahakikisha
chama kinabaki imara hata baada
ya kuwanyima fursa hiyo
wanachama hawa wanaonekana
kuwa na madoa
Ikumbukwe kwamba hao
wanaoshutumiwa ni makada
wenye ushawishi wa hali ya juu
na wafuasi wengi ndani ya chama
ambao bila shaka wanauwezo wa
kuhatarisha umoja na uhai wa
chama ikiwa wagombea wao
watanyimwa fursa hiyo.
Mwaka jana CCM ilionesha
makeke yake baada ya
kuwasimamisha makada wake
sita kwa muda wa takribani miezi
17 ambao walibainika kukiuka
kanuni za uchaguzi cha chama.
Ni nani ataaminiwa kupewa
dhamana ya kupeperusha
bendera ya CCM? Na ni nini
mustakabali wa chama hicho
baada ya mchakato wa kumpata
mgombea huyu wa tiketi ya
chama? Maswala haya na
mengine mengi bila shaka yapata
majibu yake baada ya kikao cha
chama hicho.BBC

No comments:

Post a Comment