Wednesday, July 8, 2015

CCM KANUNI 5 ZA WAGOMBEA U R A IS.

Kanuni 5 bubu za kumpata mgombea urais
wa CCM
Mwandishi Wetu Toleo la 413 8 Jul 2015
More information about text formats
Text format
Ni kanuni zisizoandikwa lakini zenye nguvu
Ni sawa na ‘siri ya mtungi aijuae kata’
HIVI karibuni, kipenga cha mchakato wa kuwania nafasi ya
kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais kilipigwa rasmi na
Halmashauri Kuu ya chama hicho. Kumetokea utitiri wa
wagombea wanaotangaza nia na kuchukua fomu. Watia nia
hawa wamekuwa wakijitapa kuwa wamejipima na
kujiridhisha kwamba wanatosha kuteuliwa kupeperusha
bendera wa Chama hicho. Wako pia waliosema
wamesukumwa na watu kutoka makundi mbalimbali ya
kijamii waliowashawishi kugombea.
Utitiri wa wagombea umezua maswali mengi na gumzo
miongoni mwa wananchi na duru mbalimbali za siasa. Wako
wanaouona utitiri huo kama kielelezo cha kupanuka kwa
demokrasia ndani ya Chama cha Mapinduzi na wako wale
wanaouona utitiri huo kama kituko na fedheha kwa CCM.
Hawa wanahusisha kujitokeza kwa wingi kwa wana CCM
kutangaza nia kama kuidhalilisha na kuishusha thamani
nafasi ya urais.
Kwa wale waumini wa demokrasia, kule tu mwanachama
kuweza kufikiria kuchukua fomu na kuthubutu kufanya hivyo,
ni kielelezo cha afya ya demokrasia ndani ya CCM. Wana
CCM angali ni watu wenye imani kuwa ndani ya Chama
hicho yoyote anaweza kushika nafasi yoyote. Kanuni ya asili
ya demokrasia humpa mtu yeyote nafasi ya kutamani na
uhuru wa kufanya uamuzi wake wa kuomba ridhaa, lakini
kutimizwa kwa tamaa yake hiyo, kunategemea ridhaa ya
wengine, yaani walio wengi. Huu ni utamaduni unaopaswa
kuigwa na vyama vingine.
CCM tofauti na vyama vingine, kimejizatiti kitaasisi na hivyo
kwa kiasi cha kuridhisha kinaendeshwa kwa kufuata katiba,
kanuni na taratibu za Chama hicho. Kama ilivyo kwa
utamaduni wa vyama vya siasa, zipo pia zile kanuni ambazo
hazijaandikwa, yaani kanuni bubu. Kanuni hizi bubu hutumika
sana katika kuchagua mgombea wa urais wa CCM, juu ya
zile sifa 13 zilizoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za
Chama kwa wagombea wa nafasi za uongozi serikalini. Sifa
hizo ni zifuatazo:
i. Awe na uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa kwa kuzingatia
uzoefu wake katika uongozi wa shughuli za serikali, umma
na taasisi;
ii. Awe mwadilifu, asiyetiliwa shaka juu ya matendo ya
uadilifu mbele ya uso wa jamii ya Watanzania na awe
mwenye hekima na busara;
iii. Awe na angalau kiwango cha elimu ya Chuo Kikuu au
elimu inayolingana na hiyo;
iv. Awe mwenye upeo na uwezo mkubwa wa kudumisha,
kuimarisha na kuendeleza Muungano wetu, Umoja wetu,
amani na utulivu wetu na mshikamano wa kitaifa;
v. Awe mtu mwepesi wa kuona mbali, asiyeyumbishwa na
mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara kuhusu
masuala nyeti na muhimu kwa taifa kwa wakati unaofaa;
vi. Awe na upeo mkubwa na usiotiliwa shaka wa masuala ya
kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi yetu na
dunia kwa ujumla;
vii. Asiwe mtu mwenye hulka ya kidikteta au ufashisti, bali
awe mtu anayeheshimu na kulinda Katiba ya nchi, sheria,
utawala bora, kanuni na taratibu za nchi;
viii. Awe mtetezi wa wanyonge, wa haki za binadamu,
mzingatiaji makini wa maendeleo ya raia wote na asiwe na
tamaa ya kujitafutia umaarufu wa mtu binafsi;
ix. Awe mstari wa mbele katika kuzifahamu, kuzielezea,
kuzitetea na kuzitekeleza sera za CCM na ilani ya CCM ya
uchaguzi;
x. Awe mpenda haki na awe mtu jasiri katika kupambana na
dhuluma na maovu yote nchini;
xi. Asiwe ni mtu ambaye anatumia nafasi yake ya uongozi
kujilimbikizia mali;
xii. Kwa ujumla awe ni mtu anayekubalika na wananchi;
xiii. Awe mtu makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji
wa viongozi/watendaji na asiyevumilia uzembe katika
utekelezaji wa majukumu/wajibu waliokabidhiwa ili kuinua
nidhamu ya kazi, tija na ufanisi.
Sifa 13 zilizoainishwa kwenye kanuni za uchaguzi za CCM ni
sifa nzuri sana mgombea urais wa chama hicho kuwa nazo.
Hata hivyo, sifa hizo si pekee, wala sio turufu ya kumfanya
mwanachama anayetimiza hizo kuwa mgombea urais wa
chama hicho. Ziko kanuni zingine zisizoandikwa au
zisizozungumzika upenuni ambazo huongoza busara na
hekima ya ngazi za juu za uamuzi za chama hicho katika
kumpata mgombea urais. Kanuni bubu ndio huongoza
mashauriano na maridhiano baina ya wajumbe wa Kamati
Kuu na wazee wa Chama kuhusu nani apeperushe bendera
ya Chama hicho.
Kanuni bubu hizi zimetokana na uzoefu wa CCM kutawala
nchi kwa miongo mitano na zimejaribiwa na kuthibitika
kufanya kazi. Hizi ndizo zinazoifanya CCM kuendelea
kutawala na nchi kuendelea kuwa katika amani na utulivu
tulionao. Kwa lugha nyepesi, Kanuni Bubu ndio sawa na ‘siri
ya mtungi’ au kwa lugha nyingine ‘siri ya jando’ ambayo
huhifadhiwa na hurithishwa kutoka kizazi kimoja cha viongozi
kwenda kingine. Huongoza hekima na busara za viongozi
katika kufikia uamuzi wa nani wa kumkabidhi kijiti. Kanuni
Bubu hizi 5 ni: mpokezano wa dini; nafasi kwa makabila
madogo; usalama wa Rais na Mwenyekiti anayeondoka;
kukubalika nje ya nchi; na kukubalika na vyombo vya ulinzi na
usalama.
Mpokezano wa Dini
Historia ya nchi yetu tangu harakati za kusaka uhuru hadi
sasa ni historia ya mtifuano na vuguvugu kati ya dini mbili
zenye waumini wengi nchini, yaani ukristo na uislamu.
Mtifuano huu ulitokana na sera mbovu za kijamii za serikali
za kikoloni ambazo zilitoa upendeleo kwa zile jamii
zilizoukubali ukristo.
Sera hizo ziliwapa fursa zaidi wakristo kupata elimu
iliyotolewa na wamisionari kwa niaba ya serikali ya kikoloni
huku zikibagua wale wasiokuwa wakristo. Sera hizi ndizo
zilizosababisha jamii ya wakristo kuendelea zaidi kuliko ile ya
waislamu. Kutokana na ukweli huo, harakati za uhuru katika
hatua zake za awali zilibeba taswira hiyo hiyo ikiwemo kuwa
na jumuiya za kiislamu, au baadhi kuzichukulia harakati za
awali za uhuru kama harakati za waislamu.
Katika miaka ya mwanzo ya ujenzi wa taifa letu baada ya
uhuru, uongozi wa TANU na Serikali ya Mwalimu Nyerere
vilijaribu sana kurekebisha kasoro hiyo ya kihistoria. Sehemu
kubwa ya uamuzi ulifanyika ikiwemo utaifishaji wa shule
zilizokuwa zikimilikiwa na makanisa. Yote hayo yamesaidia
kupunguza joto wakati serikali ikiendelea kurekebisha kasoro
hizo za kihistoria ambazo zitachukua muda mrefu kuondoka,
ikizingatiwa kuwa zilijengwa kwa muda mrefu sana. Hadi
sasa tumeendelea kuziona hisia hizo zikikamata moto kila
tukikaribia uchaguzi mkuu.
Katika kuiweka nchi kwenye hali ya utangamano na amani,
kumekuwa na makubaliano yasiyo rasmi, na kanuni bubu
kuwa uongozi wa juu ya nchi hubadilishwa kwa kushikiliwa
na mtu wa dini nyingine kila baada ya miaka 10. Ukiuangalia
mtiririko wa marais wetu kuanzia Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere hadi Rais Jakaya Kikwete, ni rahisi kuhitimisha kuwa
mazingira na uzoefu unaelekeza Rais ajaye lazima awe
mkristo. Hili halijaandikwa popote lakini limo akilini na
mioyoni mwa wadau wa siasa. Hivyo, wagombea walio
wakristo, wanayo nafasi zaidi ya kupitishwa na CCM katika
uchaguzi wa ndani ya chama chao mwaka huu.
Nafasi kwa makabila madogo
Nchi yetu ina makabila yasiyopungua 129. Kati ya hayo, yapo
makabila makubwa na yale madogo na hata yale
yasiyojulikana. Ni ukweli pia kuwa ukubwa wa yale makabila
makubwa hautokani tu na wingi wa watu wake, bali nguvu
yao ya kiuchumi na kirasilimali watu. Ndio kusema, katika
hali ya kawaida, bila kuwepo na mkakati wa kuyapa nafasi
makabila madogo katika uongozi wa nchi, ni rahisi sana
makabila hayo kutojiona kuwa ni sehemu ya keki ya taifa, na
pengine kuachwa pembezoni. Kabila kama la wazanaki
lisingeweza kujulikana na kuonekana katika ramani ya nchi
yetu kama lisingemtoa Rais wa kwanza Mwalimu Nyerere.
Vivyo hivyo kwa kabila la wamakua kumtoa Rais Benjamin
Mkapa na kabila la wakwere kumtoa Rais Jakaya Kikwete.
Makabila kama wasukuma, wahaya, wachaga hata bila kutoa
Rais ni makabila yenye heshima, nafasi na ukubwa wa
kiuchumi usiopuuziwa.
Tanzania ni nchi ambayo haionekani na kutambuliwa kama
nchi yenye ukabila. Hata hivyo, virusi vya ukabila bado
havijatokomea kabisa nchini. Zimefanyika juhudi kubwa sana
tangu uhuru za kurekebisha tofauti za ukabila na kujenga
mtangamano. Sera ya elimu ya kusomesha wanafunzi nje ya
maeneo waliyozaliwa na kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga
Taifa kuliwezesha kwa kiasi kikubwa kuleta makabila karibu
na hatimaye makabila kuingiliana na kuoleana. Hata hivyo,
bado yapo makabila haswa makubwa ambayo yamekuwa na
ukakasi katika kuchanganyana na mengine, na kutukuza
ukabila wao. Bado yako manung’uniko juu ya makabila fulani
yanapopata madaraka kupendeleana na kupendelea makwao.
Katika kuepusha kustawi kwa siasa za ukabila na ukanda,
kama ambavyo imeshaanza kujiridhisha katika uchaguzi huu,
kanuni bubu inataka mgombea urais wa CCM atokane na
kabila au jamii ndogo au mkoa ulioko nyuma au kusahaulika
ili kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya Chama na
miongoni mwa Watanzania. Ni namna ya kuamsha
matumaini kwa Watanzania wote kuwa kila eneo linaweza
nalo kufaidika na keki ya taifa na kupata dhamana ya
kuliongoza taifa. Hivyo, mtangaza nia kutoka katika kabila
dogo au jamii dogo anayo nafasi kubwa katika uchaguzi
ndani ya Chama kuteuliwa kuwa mgombea urais. Maana
hataweza kuwa na uwezo wa kujaza kabila lake zima katika
serikali wala kuwapendelea katika uteuzi kwa kuwa hanao wa
kutosha wenye elimu, ujuzi wa kujaza nafasi zote za Serikali.
Usalama wa Rais na Mwenyekiti anayeondoka
Sifa moja kubwa inayoifanya Tanzania kuwa nchi yenye
amani na utulivu ni utaratibu wa marais kung’atuka wakati
wa kufanya hivyo unapofika. Tofauti na nchi nyingi za
kiafrika, hatujawahi kushuhudia hapa nchini mwetu Rais
akitaka kuongeza muda wa kukaa madarakani. Aidha,
tumeshuhudia marais wakikabidhi madaraka na kwenda
kujipumzikia. Marais wastaafu wamekuwa wakiheshimiwa,
wakipatiwa huduma za kiitifaki na stahili zao na wakienziwa
na kutumika kwa ushauri na kwenye shughuli mbalimbali.
Kumekuwepo na utamaduni wa marais wastaafu kuheshimu
Rais aliyeko madarakani na kutowaingilia katika uamuzi na
uendeshaji wa serikali. Hali kadhalika, Rais anayekuwa
madarakani, hatumii madaraka yake kumnyanyasa wala
‘kumshughulikia’ Rais aliyepita. Vivyo hivyo katika nafasi ya
uenyekiti wa CCM. Ni kwa mantiki hii, Mwalimu Nyerere
alipong’atuka urais, akang’atuka na Uenyekiti wa Chama ili
kumpa nafasi na hatamu Rais Mwinyi kuwa pia Mwenyekiti
wa Chama na kuepusha migongano. Imekuwa hivyo kwa
viongozi wote waliofuatia.
Nchi nyingi za kiafrika zimeingia katika machafuko kutokana
na kutokuwa na utamaduni huu wa kuheshimu na kuwaenzi
marais wao waliopita. Tumeona marais wakitoka madarakani
katika nchi nyingine wakifukua makaburi na kuwafunga
marais waliowatangulia. Tumeona Zambia ambako Rais
Frederick Chiluba alimuweka ndani Rais Keneth Kaunda,
naye akawekwa ndani na Rais Levy Mwanawasa, na hata pale
Rais Rupia Banda alipoanguka katika uchaguzi, Marehemu
Rais Michael Sata naye akamfungulia kesi Rais Banda. Marais
walionusurika kufunguliwa mashtaka Zambia ni Rais
Mwanawasa na Rais Sata pekee maana walifariki kabla ya
mwisho wa awamu zao za uongozi. Hali hii huwafanya pia
marais walioko madarakani kutaka kung’ang’ania madaraka
na kuongeza muda kwa kuogopa kushughulikiwa na
kunyanyaswa mara watakapotoka madarakani kwa hiyari, au
kwa kumaliza mihula yao ya uongozi.
Tumeshuhudia katika nchi yetu mfano mzuri wa kuheshimu
viongozi waliopita. Wakati tu alipoingia madarakani Rais
Kikwete, kulikuwepo na harakati kubwa kutoka kwa
wanasiasa na wanaharakati kutaka Rais Mkapa ashitakiwe
mahakamani. Shinikizo hili halikuweza kumyumbisha Rais
Kikwete na alilivunja pale aliposema, ‘Mwacheni Mzee Mkapa
apumzike’. Kule Zanzibar, shinikizo kama hili lilielekezwa kwa
Rais Dk. Mohamed Shein wakimtaka amshughulikie Rais
mstaafu Amani Karume naye hakufanya hivyo. Hawakufanya
hivyo kwa kutambua kuwa uongozi ni dhamana kubwa
ambayo inaambatana pia na kufanya makosa, tena mara
nyingi bila kudhamiria na kukusudia.
Rais anayestaafu, anastahili kupimwa kwa yale mema
aliyolifanyia taifa si makosa madogo madogo yaliyotokea
katika utawala wake, maana hatuchagui malaika. Kutokana
na ukweli huu, mgombea urais atakayepewa nafasi kubwa na
Chama lazima awe mtu anayeaminika, na anayeonekana
kuweza kulinda heshima ya Rais na Mwenyekiti mstaafu wa
Chama, si yule mwenye kuonekana na kisasi au nongwa na
Rais anayeondoka madarakani.
Tukirejea uchaguzi wa ndani ya CCM mwaka 2010 kule
Zanzibar somo hili linajitokeza. Inasemekana, moja ya
sababu kubwa ya Makamu wa Rais Mohammed Ghalib Bilal
kutopitishwa kugombea Urais Zanzibar pamoja na ushawishi
wake mkubwa, ni hofu ya Rais Karume juu ya usalama wake
ikiwa Ndugu Bilal angekuwa Rais. Kamati Kuu ya CCM
ilifanya uamuzi wa kumkata Ndugu Bilal na kumpooza kuwa
kumteua kuwa Mgombea Mwenza. Hivyo, haitashangaza
kuwa CCM haitampa nafasi mtu yeyote anayeonyesha
dhahiri yeye mwenyewe au wapambe wake kuwa na dhamira
mbaya na Rais anayeondoka madarakani. Ni busara ya
kawaida tu kuwa huwezi kumkabidhi adui yako kisu cha
kukuchinjia.
Kukubalika Nje ya Nchi
Tanzania ni nchi ambayo usalama wake na utajiri wa
rasilimali zake unaathiriwa sana na jiografia yake. Nchi yetu
imepakana na nchi 8 za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi,
DRC, Zambia, Malawi na Msumbiji. Jiografia hii kwetu ni
fursa lakini pia changamoto kubwa. Ni fursa nzuri ya kufanya
biashara na kukuza uchumi ikitumika vizuri hali kadhalika ni
changamoto kubwa kwa usalama na amani yetu ambayo kwa
kweli ndio msingi wa maendeleo.
Kutokana na ukubwa wa eneo la nchi yetu yenyewe, urefu wa
mipaka yetu inakadiriwa kuwa na urefu wa kilometa 3,402,
sawa na urefu wa kusafiri kwa barabara kutoka Dar es
Salaam hadi Johannesberg, Afrika Kusini unaokadiriwa kuwa
ni km 3,533. Aidha, mipaka na nchi hizo ni mipaka mirefu
yenye kupenyeka. Mpaka wa Burundi peke yake ni kilometa
451, yaani umbali wa Dar es Salaam hadi Lindi. Isitoshe
baadhi ya nchi tunazopakana nazo ni nchi zenye mienendo
isiyotabirika na historia ya uvamizi, na madai ya mipaka
yasiyokwisha yanayosukumwa na tamaa ya kujipanua.
Nyingine ziko kwenye migogoro ya kisiasa isiyokwisha na
hata vita. Kwa upande wa bahari, nchi yetu ina pwani yenye
urefu wa kilometa 1,424, yaani urefu wa barabara kutoka Dar
es Salaam hadi Nairobi kupitia Namanga. Katika ukanda huu
wa bahari, tumegundua pia gesi asilia jambo ambalo
linazalisha changamoto nyingine ya kiusalama. Yote haya
kwa ujumla, yanaifanya nchi yetu kuwa na changamoto
pekee ya kiusalama.
Maumbile na jiografia ya nchi yetu, inazifanya Sera ya Mambo
ya Nje ya nchi kuwa na umuhimu wa kipekee sana katika
uongozi wa nchi yetu. Diplomasia ya Tanzania ina mchango
mkubwa sana katika amani na usalama wa nchi yetu. Ndio
sababu, moja ya msingi mkuu wa Sera yetu ya nje ni ujirani
mwema. Ujirani mwema huepusha uwezekano wa nchi
kupigana vita na kuhasimiana na hivyo kupunguza kutumia
fedha nyingi sana katika ulinzi wa mipaka au katika vita.
Fedha hizi zinazookolewa na diplomasia yetu ndizo
zinazowezesha Serikali kujiendesha na kutoa huduma za
jamii na ujenzi wa miundo mbinu. Sote tunafahamu gharama
kubwa tuliyoingia kutokana na vita vya Uganda ambavyo
viliturudisha nyuma kimaendeleo na uchumi, ambapo
tumeanza kuinuka tena miaka 10 iliyopita.
Diplomasia yetu nayo inatusaidia sana katika kukaa vizuri na
nchi zingine za nje, wadau wa nje na mashirika ya kimataifa.
Hawa nao kwa pamoja wanao uwezo mkubwa sana wa
kuvuruga siasa za ndani ya nchi kwa uamuzi wao wa kisera
dhidi ya nchi nyingine. Tumeona uamuzi wa mataifa
makubwa kama Marekani yalivyoukandamiza uchumi na
uhuru wa Cuba kwa miaka 50. Aidha tumeona pia nchi kama
Iran na Zimbabwe zikiwekewa vikwazo vya kiuchumi
ambavyo vimeathiri sana wananchi wa nchi hizo. Historia pia
inayo mifano mingi ya nchi jirani zilizopiganishwa kwa
maslahi ya nchi kubwa. Mathalani, ingekuwa hatuna
mahusiano mazuri na nchi kubwa duniani, mgogoro wa
kisiasa uliojitokeza kati ya Tanzania na Rwanda au ule wa
mpaka na Malawi ungeweza kutumiwa dhidi yetu.
Ni dhahiri kuwa, pamoja na kuwa tunachagua Rais wetu,
kimkakati Chama kitapaswa kujiridhisha na uwezo wa Rais
huyo kulinda na kudumisha maslahi yetu nje. Tanzania
inategemea soko la nje, uwekezaji na pia misaada kutoka nje.
Zipo pia siasa za kikanda ambazo nazo zinahitaji umakini wa
hali ya juu sana kukabiliana nazo. Tumeona namna ambavyo
Rais Kikwete amefanikiwa sana kuvuna marafiki, fursa na
kupanua maslahi ya nchi yetu nje. Kufanikiwa kwa Rais
Kikwete hakujatokana tu na usahihi wa sera, bali pia
ukomavu na haiba yake ambayo imemfanya kuwa mtu
anayekubalika kimataifa. Wadau wote hawa wa nje wanayo
matarajio juu ya Rais wa Tanzania atakayechaguliwa.
Hawategemei CCM ichague mgombea urais anayefanana na
rushwa na ufisadi au dikteta maana atatoa mashaka pia juu
ya uwekezaji wao na matumizi ya fedha zao za maendeleo
wanazoleta nchini.
Kwa bahati mbaya, haya si masuala ambayo wananchi
wanayafahamu wala wanampima nayo mgombea urais
pengine kwa sababu mambo nchini kwetu yamekuwa
yakienda vizuri katika eneo hili. Tunachosahau ni ukweli
kuwa mambo kwenda vizuri ni matokeo ya jitihada na uamuzi
sahihi si kudra. Wenzetu Kenya, kwa kushindwa kuweka
sawa uhusiano na Somalia kumesababisha kufanya uamuzi
wa kwenda Somalia na unawagharimu sana uchumi na
usalama wao. Tishio na matukio ya kigaidi yameongezeka
ndani ya Kenya, watalii wameacha kwenda na gharama za
kuendesha vita huko Somalia nazo zinautafuna uchumi
wake.
Haya ni mazingatio mahsusi ambayo Kamati Kuu ya CCM
huyazingatia inapopitisha wagombea wa urais kwa usalama
wa nchi yetu na ustawi wake. Hii ni sehemu ya kanuni bubu
ambayo haijaandikwa kokote. Wagombea wenye uelewa na
uzoefu wa masuala haya ya kimataifa wanayo nafasi kubwa
ndani ya CCM kuteuliwa kuwa mgombea wa urais ukizingatia
kuwa Rais wa Tanzania, kwa nafasi yake ndio Mkuu wa Nchi,
yaani mwanadiplomasia nambari wani.
Kukubalika na vyombo vya ulinzi na usalama
Rais wa Tanzania nje ya majukumu yake ya Ukuu wa Nchi na
Ukuu wa Serikali, jukumu lake lingine kubwa ni Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Huu ni mhimili
muhimu katika kumkamilisha Rais kuweza kuongoza na
kutawala. Rais wa nchi lazima akubalike na vyombo vya ulinzi
na usalama na vimtii. Vyombo hivi vina mchango mkubwa
sana kwa amani ya nchi na vimechangia sana katika kuiweka
nchi salama. Wakati Tanzania imepata uhuru mwaka 1961 na
imekuwa na marais wanne tu, Nigeria iliyopata uhuru mwaka
1960 imetawaliwa na marais 15, marais 8 kati ya hao ni
wanajeshi walioingia madarakani kwa njia za mapinduzi.
Tanzania imefanikiwa kuepuka mapinduzi na uasi wa majeshi
kutokana na menejimeti nzuri ya uhusiano kati ya serikali na
majeshi yetu. Itakumbukwa kuwa mwaka 1964, lilitokea
jaribio la uasi dhidi ya Rais wa wakati huo Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tangu funzo lile,
kumekuwepo na sera madhubuti za menejimenti ya uhusiano
mzuri kati ya jeshi letu na serikali na miongoni mwa vyombo
vya ulinzi na usalama ambavyo vinashirikiana kwa karibu na
kufanya kazi kama timu yenye utii uliotukuka kwa Amiri Jeshi
Mkuu na Rais wa Tanzania.
Haitashangaza kuwa Kamati Kuu ya CCM na vikao vingine
vya juu vitakapokuwa vinachambua wagombea, vitajiridhisha
kuwa huyo mgombea anayeteuliwa ni mtu mwenye sifa na
haiba ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Sina shaka kuwa
watajiridhisha na uwezo wa mgombea huyo mteule
kuwianisha na kuoanisha Sera yetu ya Ulinzi na Sera ya Nje
ambazo kwa asili zinakwenda pamoja kama ‘chanda na pete’.
Hii ni kwa sababu, kufeli kwa sera moja, kuna athari ya moja
kwa moja kwa sera nyingine, na hususan kwa sera ya ndani
ya nchi. Mfano, kufeli katika menejimenti ya uhusiano wa nje,
huweza kuzalisha uhasama na vita, ambayo itaathiri maisha
ya watu na uchumi kwa kulazimu rasilimali kubwa
kuelekezwa kwenye ulinzi na ununuzi wa silaha badala ya
maendeleo.
Jambo lingine ambalo linapaswa kuzingatiwa ni kuwa,
vyombo vya ulinzi na usalama haviko tu kwa ajili ya
kupambana na kupigana bali pia kuepusha vita. Hivyo,
havipendelei, na havitapendelea kuona aina ya mgombea
ambaye atatawala vibaya na kuvuruga amani ya nchi na
uhusiano nje maana huyu anawapeleka vitani. Vyombo hivi
hupenda tu kwenda vitani ikiwa ndio hatua ya mwisho, yaani
kuwe hakuna jinsi. Hawa ni wajumbe wa kudumu wa Baraza
la Usalama wa Taifa ambalo Mwenyekiti wake ni Rais na
Amiri Jeshi Mkuu. Kwa sababu hiyo, navyo vina maslahi na
michakato ya urais wa vyama vyote, hususan mchakato wa
chama tawala. Maana hili si jambo dogo la kuachia
wanasiasa peke yake.
Itakumbukwa kuwa baada ya kufariki ghafla kwa aliyekuwa
Rais wa Malawi, Hayati Bingu wa Mutharika, ripoti ya Tume
ya Uchunguzi ya Yaliyotokea Kati ya Kufariki kwa Rais
Mutharika na Kuapishwa kwa Rais Banda, inaonyesha
kuelezea namna ambavyo kulikuweko na mashauriano
makubwa kati ya Serikali, Chama tawala na Wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama vya Malawi. Hali hii hutokea
pia katika nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani kutokana na
umuhimu na unyeti wa nafasi ya Rais.
CCM inao uzoefu wa kutosha wa kutawala na kuendesha
nchi. Kuwepo na amani na utulivu nchini kwetu tangu uhuru
ni ushahidi wa ukomavu huo. Katika nyakati hizi ambazo hali
ya usalama imekuwa tete kidogo kutokana na changamoto za
ugaidi na genge la uhalifu wa dawa za kulevya, usalama wa
shaka katika nchi jirani zinazotuzunguka na ule ukweli kuwa
utajiri wa rasilimali kama gesi asilia huja na changamoto za
kipekee za kiusalama kama tuonavyo Nigeria na kwingineko,
ni dhahiri kuwa chaguo la mgombea wa CCM litazingatia
haya. Ndio kusema, mgombea mwenye uelewa au historia ya
majeshi ya ulinzi na usalama anaweza kuwa na nafasi kubwa
sana katika uchaguzi huu kushinda wakati mwingine wowote
katika historia ya nchi yetu.
Hitimisho
Kama niliyosema awali, CCM inazo sifa 13 za mgombea
urais wa CCM. Sifa hizi nzuri zinaweza kufikiwa na
wagombea wengi waliojitokeza. Katika hali hiyo, upo ulazima
wa kuwa na sifa za ziada juu ya sifa hizo 13 kwa kuwa
hatimaye lazima Kamati Kuu iwapendekeze wagombea
watano tu kati ya wengi ili waweze kufikishwa kwenye
Halmashauri Kuu ya Taifa. Kamati Kuu na Kamati ya Maadili
ya Kamati Kuu kwa muundo na taswira yake ndiyo ngazi ya
kimkakati zaidi kuliko ngazi nyingine yoyote ya uamuzi ndani
ya CCM. Ndio chombo kinachoangalia maslahi mapana ya
chama na taifa kwa ujumla. Uamuzi wa chombo hiki kwa
kiasi kikubwa ndio uamuzi wa Chama katika ngazi nyingine.
Hivyo, umakini mkubwa huwekwa hapo kwa kuzingatia kuwa
kukosea kwa Kamati Kuu kunaweza kusababisha kukosea
kwa ngazi nyingine zote za uamuzi.
Ni ukweli ulio wazi kwamba si rahisi kumpata mgombea
mwenye kukidhi sifa zote 13 kwa kiwango cha kutukuka na
pia kutimiza vigezo vya Kanuni Bubu 5. Akiwepo huyo mtu
basi atakuwa na sifa za kimalaika. Kamati Kuu itatarajiwa
kuwapendekeza wagombea ambao kwa kiasi kikubwa na cha
kuridhisha, anakidhi sehemu kubwa ya sifa na vigezo hivyo.
Aidha, mgombea ambaye wakilinganishwa na wale
watakaochujwa, wawe wanawazidi kwa vigezo hivyo. Kwa
vyovyote vile, mgombea atakayechaguliwa mwishoni, si
lazima awe yule tunayempenda sana au tuliyemtarajia, lakini
anayetafutwa ni mgombea wa CCM na hatimaye Rais wa
Tanzania. Tujiandae kwa matokeo tusiyoyatarajia.
Mwandishi wa makala hii, Mashauri Chachika
amejitambulisha kuwa ni Mchambuzi wa Masuala ya Siasa
na Stratejia na msomaji wa gazeti la Raia Mwema

No comments:

Post a Comment